Kubemenda Mtoto: Maana, Sababu na Jinsi ya Kuepuka

4 Min Read

Baada ya kujifungua, mwanamke hushauriwa kutokushiriki tendo la ndoa na mumewe ili kuepusha kumbemenda mtoto.

Aidha, kufanya mapenzi na mwanamme asiye baba halisi wa mtoto ni sababu nyingine inayotajwa kuwa kiini cha kubemendwa kwa watoto.

Nadharia hizi mbili husisitiza kuwa shahawa anazomwaga mwanamme baada ya kufika kileleni huchanganyikana na maziwa anayonyonya mtoto hivyo huleta athari hasi kwenye ukuaji wa mtoto.

Maana

Kiufupi, kubemenda ni kudumaa kwa mtoto, kimwili na kiakili. Hutokea kwenye siku 1000 za mwanzo wa uhai wa mtoto.

Watoto wenye udumavu huwa na kimo kifupi kuliko kawaida, na mara nyingi huwa na uwezo mdogo wa kufikiri na kutenda. Pia, udumavu huu huwaweka kwenye hatari kubwa ya kupatwa na magonjwa sugu hasa kisukari, shinikizo kubwa la damu na viribatumbo.

Uhalisia Kisayansi

Udumavu wa mtoto ambao kwa lugha nyingine huitwa “Kubemendwa kwa mtoto” husababishwa na maambukizi ya mara kwa mara ya magonjwa, lishe duni na uwepo wa mazingira duni ya kiuchumi na kijamii yanayozunguka ukuaji wa mtoto.

Sababu zingine kama vile uwepo wa upungufu wa damu na matatizo katika chembe za damu, kuzaliwa na uzito mdogo sana, kuwa njiti pamoja na mapungufu kwenye vinasaba vya urithi zinaweza kusababisha udumavu wa mtoto.

Hivyo, ushiriki wa tendo la ndoa kwa namna yoyote ile na baba wa mtoto, au mwanamme mwingine asiye baba wa mtoto hauwezi kusababisha udumavu wa mtoto kwa kuwa shahawa za mwanamme hazina uwezo wa kuingia kwenye maziwa ya mama, kisha kunyonywa na mtoto kama jinsi ambavyo madai yake husisitiza.

Msingi wa Hoja za Wazee

Tunajaribu kufikiria chanzo cha nadharia hii, mawazo yetu yanatupa picha kuwa pengine wazee wa zamani waliibua hoja hii ili kuwakinga wanawake wasipate ujauzito wa mapema baada ya kujifungua pamoja na kuepusha tabia ya uzinzi au uasherati ili kumlinda mtoto asije kuambukizwa magonjwa ya zinaa.

Kisayansi, baada ya kujifungua, mwanamke hushauriwa kusubiria walau kwa wiki 6 kabla hajaanza tena kushiriki tendo la ndoa. Muda huu huruhusu uponaji wa vidonda vya uzazi pamoja na kukoma kwa uchafu na majimaji ya uzazi yanayotoka kwenye uke.

Husaidia kuzuia maambukizi kwenye kizazi cha mwanamke kwa kuwa huwa bado kipo wazi sana.

Hata hivyo, baadhi ya wanawake husubiri muda mrefu zaidi ya huu na wengine huwahi zaidi. Yote hutegemea utayari wa mwanamke kisaikolojia na kimwili katika kuhimili tendo husika.

Kinga

Ni muhimu kumpatia chakula bora mtoto kulingana na umri wake, kumfanyia uchunguzi na tiba za mara kwa mara za magonjwa pamoja na kujisafisha kila baada ya kushiriki tendo la ndoa ili kutunza usafi.

Kwa watoto wenye umri chini ya miezi 6, maziwa ya mama ndio chakula pekee kinachofaa. Kwa walio na umri zaidi ya miezi 6, maziwa ya mama pamoja na vyakula vingine mbadala hufaa sana.

Pia, epuka kumuanzishia mapema mtoto vyakula mbadala kabla ya muda wake.

Muhtasari

Kubemenda mtoto ni nadharia potofu isiyo na uthibitisho wowote wa kisayansi. Kitaalam, tendo hili tunaweza kuliita kama udumavu wa mtoto.

Hali hii haihusiki kwa namna yoyote na ushiriki wa tendo la ndoa, bali husababishwa na maambukizi ya mara kwa mara ya magonjwa, lishe duni na uwepo wa mazingira duni ya kiuchumi na kijamii yanayozunguka ukuaji wa mtoto.

Kujitunza ni siha njema kwa mwanamke. Epuka ushiriki wa tendo la ndoa na wanaume tofauti ili ujilinde pamoja na kumlinda mtoto.

Umewahi kuona mtoto wa tajiri kabemendwa?

Share This Article