Homa kwa Watoto: Chanzo, Dalili na Tiba

4 Min Read

Homa kwa lugha rahisi hutafsiriwa kama ongezeko la joto mwilini linalozidi kiwango cha kawaida. Ni ishara njema inayoonesha kuwa mfumo wa kingamwili upo imara na unapambana kikamilifu kuzuia magonjwa.

Homa kwa mtoto mwenye umri wa miezi chini ya 3 huthibitishwa pale joto la mwili linaposoma kama ifuatavyo kwenye mojawapo ya viungo vyake vya mwili

  • 100.4°F (38°C) au zaidi sikioni au sehemu ya haja kubwa
  • 100°F (37.8°C) au zaidi kinywani
  • 99°F (37.2°C) au zaidi kwapani

Kwa kuwa watoto hutofautiana ukuaji, mazingira wanayolelewa pamoja na uimara wa afya zao, mzazi anapaswa kuchukulia hali joto linalofikia 100.4°F (38°C) au zaidi kama homa, hivyo achukue tahadhari zote za kiuchunguzi na matibabu ili kulinda usalama wa afya ya mtoto.

Sababu za Homa

Homa siyo ugonjwa, bali ni dalili ya ugonjwa. Ni hali inayotokea pindi mwili unapokuwa unapambana dhidi ya aina fulani ya vimelea vya magonjwa hasa bakteria na virusi.

Kwa kiasi kikubwa, virusi ndio husababisha homa kuliko bakteria. Baadhi ya sababu hizo ni maambukizi ya virusi hasa wale wa mafua na mfumo wa upumuaji, maambukizi kwenye sikio, nimonia pamoja na homa ya uti wa mgongo.

Mchafuko wa damu unaosababishwa na bakteria, chanjo, kukaa juani, kuvalishwa nguo nzito sana hasa nyakati za joto na kulia kwa muda mrefu, maambukizi ya njia ya mkojo pamoja na uwepo wa magonjwa mengine mfano Malaria huchangia pia kuleta homa kwa watoto.

    Dalili

    Dalili kuu ni kuongezeka kwa joto la mwili. Pia, watoto wengine huwa wakali, wenye kulia kuliko kawaida, wasio na usingizi, kukataa chakula, kuweweseka, kukauka kwa midomo, ugumu kwenye kupumua, kutokucheza kama kawaida pamoja na degedege.

    Madhara

    Kama tulivyosema tangu awali, homa ni dalili inayoonesha kuwa mtoto anapambana na ugonjwa fulani, au maambukizi ya vimelea vya magonjwa fulani mwilini.

    Ikiwa joto la mwili litafikia 41.67 °C (107 °F), ubongo wa mtoto unaweza kuathiriwa. Pia, baadhi ya watoto wanaweza kupata degedege kwa joto linalofikia zaidi ya 38.3 °C na zaidi.

    Matibabu

    Mwongozo wa American Academy of Pediatrics (AAP) hushauri watoa huduma na wazazi kushughulikia mambo yanayomfanya mtoto atulie kwanza na kujisikia huru kuliko hata kuhangaika na kushusha homa yenyewe. Kuna ushahidi wa kutosha kuwa watoto wanaotulizwa vizuri na kujisikia huru hushusha homa zao pasipo kuhitaji dawa yoyote.

    Mtoto anapaswa kunyonyeshwa maziwa kwa wingi ili kufidia kiasi cha maji kinachopotea kupitoa joto. Aidha, kama ana umri wa zaidi ya miezi 6 anaweza pia kupewa maji na vimiminika vingine.

    Kama mtoto kalala, si vyema kumuamsha ili apewe chakula au dawa. Jambo hili linaweza kufanyika kama kutakuwa na ulazima sana wa kufanya hivyo.

    Dawa nzuri za kushusha homa kwa watoto ni Paracetamol au Ibuprofen. Dawa hizi hupatikana kwenye majina mengi ya kibiashara ambayo yote huwa na kemikali hai zinazofanana. Mtoto asipewe zote kwa pamoja, bali dawa moja kati ya hizo kulingana na upatikanaji wake.

    Kama kavalishwa nguo nyingi au nzito, inapaswa zipunguzwe ili kusaidia joto la mwili lishuke chini kirahisi.

    Katika mazingira machache, dawa kama viuavijasumu (Antibayotiki) na aina zingine zinaweza kutumika baada ya daktari kujiridhisha kuwa changamoto aliyonayo mtoto inahitaji dawa hizo ili kuitatua.

    Tahadhari

    Aspirin ni dawa isiyofaa kutumiwa na watoto kwenye mazingira yoyote yale. Inaweza kusababisha uvimbe kwenye ubongo na ini hivyo kuhatarisha maisha, kitaalam hali hii huitwa Reye’s syndrome.

    Hivyo, wazazi na watoa huduma za afya wanapaswa kuepuka matumizi yake.

    Pia, tofauti na watu wanavyoamini, kuota kwa meno siyo sababu ya mtoto kupata homa kali. Ikiwa hali hii itatokea, apelekwe hospitalini haraka kwa uchunguzi na matibabu.

    Share This Article