Muda Sahihi wa Mtoto Kuanza Kucheza Tumboni Wakati wa Ujauzito

2 Min Read

Mojawapo ya nyakati muhimu zenye furaha kubwa kwa mama mjamzito ni kuhisi mtoto aliyeko tumboni kaanza kucheza.

Mijongeo hiyo ambayo wakati mwingine huambatana na mateke yenye kuumiza, hutoa maana nzurininayoashiria ukuaji mwema wa mtoto.

Kucheza huku kwa lugha ya kitaalam huitwa Quickening, huanza kuonekana kati ya wiki ya 16-25 ya ujauzito.

Hata hivyo, kwa wanawake wanaoshika ujauzito wa kwanza, tendo hili linaweza kukawia kidogo kuonekana hadi karibia kabisa na wiki ya 25 au hata zaidi ya hapo.

Kwa wanawake wenye historia ya kushika ujauzito kabla, wanaweza kuanza kuhisi mapema hali hii tangu wiki ya 13 ya ujauzito.

Kwa ujumla wake, muda wowote kati ya wiki ya 13-25 ni sahihi kabisa kwa mtoto kuanza kucheza. 

Mambo Yanayoathiri Uchezaji wa Mtoto

Kwa mujibu wa utafiti, kadri ujauzito unavyozidi kuwa mkubwa ndivyo mtoto huongeza kucheza. Kuanzia wiki ya 28 ya ujauzito, wanawake hushauriwa kujenga utaratibu wa kuhesabu mtoto anacheza mara ngapi kwa siku ili isaidie kugundua kirahisi shida yoyote kama mtoto atapunguza kucheza.

Uzito wa mama unaweza kuathiri uchezaji wa mtoto. Tafiti zinabainisha kuwa wanawake wenye uzito mkubwa usioendana na urefu wa miili yao hupunguza kiasi cha kucheza kwa mtoto. (1)

Mkao wa mtoto usio wa kawaida unaweza pia kuathiri uchezaji wake. Hii huchangiwa na upande ambao kondo la uzazi limejishikiza. (2)

Pia, wanawake wanaopitia changamoto mbalimbali kama vile stress, safari za umbali mrefu na kazi ngumu huwa na nafasi kubwa kuripoti kuwa watoto wao wanacheza kidogo, au wamechelewa kuanza kucheza. (3,4)

Muhtasari

Ukiachia furaha anayopata mama kwa kuhisi michezo ya mtoto aliye tumboni, tendo hili ni ishara nzuri inayoonesha kuwa mtoto anakua akiwa na afya njema.

Kuanzia wiki ya 28 ya ujauzito, mama anashauriwa kuanza tabia ya kufuatiliia uchezaji wa mwanae.

Ikiwa kwa namna yoyote ile mama atabaini kuwa mtoto kapunguza kucheza, au hachezi kabisa, anapaswa kufika hospitalini haraka kwa uchunguzi kwani inaweza isiwe ishara nzuri kwa mtoto.

Share This Article