Mojawapo ya Maswali yanayoulizwa sana na wanawake hasa wale waliopata ujauzito wa kwanza ni lini wanaweza kufahamu jinsia ya mtoto aliyeko tumboni.
Hauhitaji sayansi ya masafa marefu kujua hamu kubwa inayotawala nafsi za wanawake ambao hushindwa kuzuia hisia zao kwenye kutafuta majawabu ya swali hili.
Kutokana na uwepo wa ombwe kubwa la taarifa sahihi, upotoshaji mkubwa huwepo ambao huwafanya wahusika washindwe kuelewa wasimame wapi.
1. Kwa Ultrasound
Ultrasound ni kipimo kinachoweza kusaidia upatikanaji wa taarifa anuai zinazohusu afya ya mama na mtoto.
Kwa mama anayepanga kufanya baby shower ya mwanae huku akijua jinsia yake, anaweza kufanya chaguo la kuitafuta huduma hii mapema ili imsaidie kuondoa mtanziko wa kimawazo.
Kwa mujibu wa tafiti, kufanya kipimo cha Ultrasound wiki ya 14 ya ujauzito hubeba asilimia 75 ya kutoa majibu sahihi kuhusu jinsia ya mtoto. Hii inamaanisha kuwa kuanzia wiki ya 14 ya ujauzito, mwanamke anaweza kupima jinsia ya mwanae.
Hata hivyo, kutokana na uchanga wa ujauzito ambao humfanya mtoto asiwe na mkao mzuri unaoweza kuleta majibu tarajiwa, madaktari wengi hushauri upimaji huu ufanyike kuanzia wiki ya 18-21 ili kupata majibu sahihi zaidi.
Hutengeneza wepesi kwenye uchunguzi wa muonekano wa via vya uzazi vya mtoto ambavyo ndio hutafsiri majibu ya kipimo.
2. Njia za Kijenetiki
Matumizi ya mbinu mbadala ya kuchunguza changamoto za kijenetiki kutoka kwenye kijusi, maarufu zaidi kama Chorionic villus sampling (CVS) inaweza pia kusaidia kwenye utambuzi wa jinsia ya mtoto.
Katika mazingira ya kawaida, kipimo hiki hufanyika kati ya wiki ya 10-13.
Kipimo kingine chenye jina la amniocentesis ambacho hufanyika kati ya wiki ya 16-20 kinaweza kusaidia utambuzi wa jinsia ya mtoto.
Changamoto ya njia hizi mbili ni kukufanya usubiri walau kwa wiki mbili ndipo upate majibu, hii ni tofauti na ultrasound ambayo hutoa uhakika wa papo kwa hapo.
3. Upandikizaji Mimba, IVF
Urutubishaji wa mimba nje ya kizazi cha mwanamke ambao huambatana na upandikizaji wa kiini tete kwenye mji wa uzazi unaweza kusaidia utambuzi wa jinsia ya mtoto.
Ikiwa muundo wa kijenetiki utafanyika kwenye kubaini chembeuzi za jinsia wakati wa kupandikizwa kwa mimba, uhakika wa utambuzi wa jinsia za mtoto husika utafanikishwa kwa asilimia nyingi, karibia 100.
Muhtasari
Jinsia za watoto huanza kutengenezwa kuanzia wiki ya 6 ya ujauzito, ni muda ambao via vya kike na kiume haviwezi kutofautishwa kwa kuwa hufanana sana.
Kusubiri walau wiki ya 14 huzifanya sehemu hizo zionekane kirahisi zaidi hivyo kusaidia upatikanaji wa majibu sahihi.