Bamia: Virutubisho na Faida kwa Afya

6 Min Read

Bamia ama Okra, Gumbo au Ladies finger ni mboga za majani zinazopatikana kwenye jinasi ya Malvaceae. 

Inaaminika kuwa jamii za Abyssinia ndio zililima mboga hizi kwa mara ya kwanza duniani, hujumuisha Ethiopia, sehemu ndogo ya Eritrea kisha baadae ilienea maeneo ya Misri.

Kwa sasa mboga hii hulimwa sehemu nyingi za dunia kama zao la biashara na chakula.

Virutubisho

Rejea za USDA zinabainisha kuwa bamia hubeba maji, nishati, protini, wanga, nyuzilishe, aina mbalimbali za sukari pamoja na madini chuma, sodium, calcium, copper, manganese, zinc na selenium.

Pia, aina mbalimbali za vitamini muhimu kwa afya kama vile vitamini B12, B6, K, A, E na C pamoja na aina mbalimbali za viondoa sumu.

Mahitaji ya virutubisho hivi hutofautiana kulingana na umri, jinsia, aina ya kazi na unitaji wa nishati.

1. Mifupa

Udhoofu wa mifupa huwapata watu wenye umri zaidi ya miaka 40, huwa na athari kubwa zaidi kwa wanawake kuliko wanaume.

Ulaji wa vyakula vyenye utajiri wa vitamini K kama bamia huimarisha afya ya mifupa, kukinga tatizo kupungua kwa ujazo wake pamoja na kuongeza uimara ili isivunjike kirahisi. (1,2,3)

Kwa mujibu wa tafiti, mwanamme 1 katika kila kundi la wanaume 5 wenye umri wa zaidi ya miaka 50 yupo kwenye hatari ya kupatwa na changamoto ya udhoofu wa mifupa huku takwimu hizo zikionesha kuwa mwanamke 1 katika kila kundi la wanawake 3 wenye umri zaidi ya miaka 50 huwa na hatari ya kupatwa na ugonjwa huu.

Chukua tahadhari mapema.

2. Mfumo wa Damu

Vitamini K hutoa mchango mkubwa katika kuzuia upotezaji wa damu nyingi baada ya kupatwa na jeraha, ni mojawapo ya vitu vinavyohitajika kwenye kugandisha damu mwilini. (4,5)

Bamia ni chanzo kizuri cha Vitamini K, ni chaguo sahihi kwa watu wenye changamoto ya kupoteza damu nyingi baada ya kupatwa na majeraha.

3. Mfumo wa Chakula

Nyuzi lishe husaidia kuzuia na kutibu tatizo la ugumu wa choo, maarufu zaidi kama constipation. (6,7)

Tafiti za afya zinabainisha pia faida ya nyuzi lishe katika kukinga dhidi ya saratani ya utumbo mpana. (8,9,10)

Mboga hii inaweza pia kuwasaidia watu wanaotaka kupunguza uzito wa miili yao kwa kuwa nyuzi lishe huhusishwa na kupunguza hamu ya kula, hivyo kudhibiti wingi wa nishati inayoingizwa mwilini kupitia mlo.

4. Wanawake Wajawazito na Wanyonyeshao

Kila mwanamke mwenye umri wa kupata ujauzito hushauriwa kutumia walau 400 micrograms za folate kila siku ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za ujauzito anazoweza kuzipata.

Baadhi yake ni kujifungua mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi.

Vitamini hii huhitajika pia kwa ukuaji bora wa afya ya mtoto hasa upande wa ubongo, hivyo mwanamke anayenyonyesha hushauriwa kupata walau 500 micgrograms kila siku. Watoto huipata kupitia maziwa ya mama.

Unaweza kuipata pia kwenye mboga zingine za majani hasa spinach, broccoli, parachichi, matunda yenye uchachu na karanga.

5. Viondoa Sumu

Bamia huwa na viondoa sumu vingi vinavyofaa kwa afya. Husaidia kuondoa sumu zinazoweza kuhatarisha uhai wa seli za mwili ambazo ndio kiini cha uhai wa viumbehai vyote.

Kwa kiasi kikubwa, bamia huwa na viondoa sumu vya Polyphenols hasa flavonoids na isoquercetin, pia vitamini A na C. (11,12,13)

Huzuia kuzeeka mapema kwa ngozi, huboresha afya ya ubongo kwa kuchelewesha changamoto za uzee hasa zile za kupoteza kumbukumbu, huzuia uvimbe joto pamoja na kupunguza hatari ya kuganda kwa damu kwenye mishipa ya damu.

Tumia bamia uimarishe afya yako.

6. Magonjwa ya Moyo

Magonjwa yanayohusisha mfumo wa damu na moyo hugharimu maisha ya watu takriban milioni 17.9 kila mwaka.

Pia, Shirika la Afya Duniani linaonya kuwa idadi hii inaweza kuongezeka zaidi kama jitihada na nguvu kubwa haitawekwa kwenye kujikinga.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Moyo ya Marekani (AHA), ulaji wa vyakula vyenye nyuzilishe nyingi husaidia kuharibu lehemu mbaya kwenye mishipa ya damu inayoweza kusababisha magonjwa ya moyo.

Vyakula hivi hupunguza pia hatari ya kupatwa na Kiharusi, viribatumbo na Kisukari. Aidha, hupunguza ukubwa wa tatizo kwa watu ambao tayari wanayo magonjwa ya moyo.

Matunda, mboga za majani na nafaka zisizo kobolewa huwa na nyuzilishe za kutosha.

7. Saratani

Tafiti nyingi zilizofanyika kwa wanyama zinazonesha uwezo wa Bamia katika kudhibiti ukuaji wa seli za saratani. 

Pia, utafiti mwingine uliofanyika maabara unaonesha bamia inaweza kudhibiti ukuaji wa saratani ya matiti. Hii inatokana na uwepo wa protini aina ya Lectin. (14)

Tafiti za ziada zinahitajika ili kuthibitisha madai haya ambayo yanaweza kuwa na faida kubwa katika kuokoa uhai wa waathirika wengi wa saratani.

8. Hushusha Sukari

Takriban watu nusu bilioni duniani wanakabiliwa na changamoto ya ugonjwa wa Kisukari. Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Tafiti zilizofanyika kwenye panya unaonesha uwezo wa bamia kwenye kushusha sukari kwa kupunguza ufyonzwaji wake kwenye mfumo wa chakula hivyo kuufanya mwili utunze kiasi cha kufaa kisichozidi uhitaji. (15,16)

Tafiti za ziada zinahitajika pia kuthibitisha taarifa hizi.

Muhtasari

Sahau kejeli zote zinazotajwa zikiihusisha mboga hii. Vitu vizuri siku zote ndivyo hushambuliwa bila huruma.

Ni mboga inayopatikana kirahisi, kwa bei nafuu. Jitahidi uitumie kila mara unapopata nafasi.

Share This Article