Madafu: Virutubisho, Faida na Tahadhari kwa Afya

6 Min Read

Madafu ni maji yanayopatikana kwenye nazi changa ambayo baada ya kukomaa hugeuka kuwa tui.

Virutubisho

Kwa mujibu wa tafiti, asilimia 95 ya madafu huwa ni maji. Hata hivyo, kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), madafu huwa na mjumuiko wa nishati, wanga, protini, nyuzi lishe pamoja na madini chuma, Calcium, Magnesium, Zinc, Phosphorus, Manganese na Selenium. 

Pia, huwa na vitamini muhimu kwa afya, choline pamoja na viondoa sumu.

Faida za Madafu

Kwa Tanzania, Madafu hutumiwa zaidi na watu wanaopatikana ukanda wa Mwambao wa Pwani na Bahari ya Hindi ambako upatikanaji wake huwa ni mwingi. Hata hivyo, sehemu nyingi duniani hutumia maji haya.

1. Chanzo cha Maji

Asilimia 95 ya madafu huwa ni maji. Huupa mwili uwezo wa kurudisha kiasi cha maji yanayopotea kila siku mwilini hasa kwa watu wenye changamoto ya kuhara pamoja na wale wanaofanya mazoezi magumu.

2. Huupa Mwili Chumvi Muhimu

Madafu ni chanzo kizuri cha madini ya Potassium ambayo pamoja na kazi zingine, hutumiwa na mwili kwenye kuwezesha usafirishwaji wa taarifa pia kuimarisha mfumo wa misuli ya mwili hasa ile ya damu na moyo.

Huupa mwili uwezo wa kurudisha chumvi zinazopotea kila siku hasa kwa watu wenye changamoto ya kuhara pamoja na wale wanaofanya mazoezi magumu.

Hii inathibitishwa na utafiti, ambao unaeleza kuwa madafu yanaweza kutumika kama chanzo cha sukari na chumvi muhimu kwa watoto wanaopatwa na ugonjwa wa kuhara.

3. Moyo na Mfumo wa Damu

Huboresha afya ya moyo na mishipa ya damu kwa kupunguza shinikizo kubwa la damu. 

Utafiti mwingine unabainisha kuwa madafu yanaweza kulinda moyo kwa kupunguza nafasi ya kuugua magonjwa mbalimbali yanayouhusisha.

4. Kuondoa Sumu

Sumu ni kitu chochote kilicho na uwezo wa kuathiri mwili na mifumo yake kwa namna isiyofaa.

Tofauti na jinsi ambavyo watu wengi huamini, chakula, maji, sukari pamoja na vitu vingine vyovyote anavyotumia binadamu kila siku kwa nia njema, ikiwa vitatumika pasipo kujali kiasi, hugeuka kuwa sumu.

Uwepo wa sumu mwilini hufupisha uhai, husababisha uzee wa haraka, kusinyaa kwa ngozi pamoja na kupunguza kinga ya mwili hivyo kusababisha magonjwa sugu kama vile Saratani.

Tafiti nyingi huelezea faida za madafu katika kuondoa na kuharibu sumu mwilini. (1,2)

Tumia kinywaji hiki uboreshe afya yako. 

5. Kupunguza Tatizo la Kisukari

Mwili huhitaji sukari ili uweze kujiendesha, pasipo sukari maisha yanaweza kuwa hatarini.

Hata hivyo, kuzidi kwa sukari kuliko kiasi cha kawaida kinachotakiwa huleta athari kubwa kwa afya, hali inayotoa hitimisho la kutambua ugonjwa wa Kisukari.

Tafiti zimethibitisha uwezo wa madafu kwenye kushusha sukari hasa kwa watu wenye ugonjwa huo. Pia, hupunguza usugu wa mwili pamoja na vimeng’enya vinavyohusika katika kuweka sawa kiwango cha sukari. (3,4)

Lakini, mgonjwa anapaswa kwanza kuzungumza na daktari wake kabla hajaanza kutumia maji haya kama sehemu ya tiba kwani baadhi ya viambato vyake vyenye asili ya wanga huwa na uwezo wa kubadilishwa kuwa sukari. 

6. Figo

Figo husaidia kuchuja na kutoa uchafu, vimiminika vya ziada, asidi pamoja na chumvi za mwili.

Kuharibika kwa kiungo hiki chenye umbo linalofanana na harage huhatarisha afya hivyo mhusika hupaswa kupata huduma za usafishaji wa damu kwa kutumia mashine ya nje ambazo kiuchumi huwa ni ghali sana, huhitaji walau fedha za kitanzania milioni 1 kila wiki.

Utafiti wa mwaka 2018 unaonesha kuwa madafu husaidia kuharibu mawe kwenye figo, pamoja na kukinga yasitegenezwe.

Changamoto za ugonjwa wa figo huathiri takriban asilimia 12 ya idadi ya watu wote duniani hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari mapema kwenye kujikinga.

7. Ngozi

Pasipo kujali unakunywa au unatumika kujipaka mwilini, madafu husaidia kulainisha ngozi, kuondoa makunyazi na kuzuia isizeeke mapema.

Pia, husaidia uponaji wa haraka wa vidonda, kupambana na bakteria wanaoathiri ngozi pamoja na kutibu chunusi. (5,6)

Wewe ni mtu unayependa urembo wa ngozi? Madafu ni rafiki yako mzuri.

Tahadhari Zake

Watu wenye ugonjwa wa figo hawashauriwi kutumia kinywaji hiki sababu ya wingi wa Madini ya Potassium ambayo figo hushindwa kuyatoa yote kupitia mkojo.

Hali hii inaweza kusababisha tatizo la kukusanyika mwilini kwa Potassium, hali ambayo kitaalam huitwa Hyperkalemia ambalo lisipodhibitiwa vizuri, pamoja na athari zingine, huufanya moyo uzalishe mapigo yasiyo na mpangilio maalum, kudhoofu kwa misuli ya mwili na kupooza.

Kwa mantiki hii, hiki ni kinywaji kisichofaa kwa watu wenye ugonjwa wa figo.

Muhtasari

Madafu ni kinywaji kinachofaa kwa watu wa umri na rika zote isipokuwa kwa wale wenye ugonjwa wa figo.

Hupatikana kwa gharama ndogo isiyolingana na wingi wa faida ambazo mwili huzipata naada ya kutumia.

Usiwaze mara mbili kuhusu usalama wake kwa afya, tumiak kila unapopata nafasi.

Share This Article