Hali ya Mtoto wa Jicho hutokea pale lenzi ya jicho inapopata ukungu na kuathiri uwezo wa kuona.
Ni chanzo kikuu cha upofu kwa watu wenye umri wa miaka 40 na kuendelea. (1)
Chanzo
Visa vingi vya tatizo la mtoto wa jicho huhusishwa na mabadiliko ya kawaida ya ukuaji wa binadamu yanayotokea kwenye macho.
Kadri umri unavyozidi kuongezeka, hasa baada ya kufikisha miaka 40, protini zinazopatikana kwenye lenzi za macho huanza kuvunjika na kujikusanya pamoja. Kitendo hiki huifanya lenzi ya macho ipatwe na ukungu hivyo kupunguza uwezo wake wa kuona.
Magonjwa ya kisukari, shinikizo kubwa la damu, ajali inayohusisha macho, uvutaji wa sigara, kukaa muda mrefu kwenye jua pamoja na kutoka kwenye familia yenye historia ya uwepo wa tatizo hili huongeza nafasi ya mtu kupatwa na mtoto wa jicho. (2,3)
Pia, unywaji mkubwa wa pombe na matumizi ya dawa kundi la steroids huhusishwa na kutokea kwa hali ya mtoto wa jicho.
Dalili
Tofauti na magonjwa mengine, tatizo la mtoto wa jicho linaweza lisioneshe dalili zozote kwenye hatua za mwanzo. Hata hivyo, dalili zifuatazo huonekana kadri ukubwa wa tatizo unavyozidi kuongezeka-
- Kupungua kwa uwezo wa kuona hasa nyakati za usiku
- Kuona ukungu badala ya picha na muonekano halisi wa vitu
- Kuona rangi za vitu zikiwa zimefifia
- Kuongezeka kwa msisimko wa macho kwenye kutazama mwanga wa jua au taa
Kwenye hatua ya awali, ukungu huu huathiri sehemu ndogo ya lenzi ya jicho hivyo ni ngumu kutambua uwepo wake. (3)
Kinga
Namna nzuri ya kujikinga na tatizo hili hasa kwa watu wenye umri mkubwa ni kuvaa miwani ya jua ili kupunguza athari ya mionzi.
Pia, kuepuka uvutaji wa sigara, kutumia mlo bora wenye wingi wa viondoa sumu (antioxidants) hasa matunda na mboga za majani pamoja na kutibu vizuri magonjwa ya kisukari na shinikizo la juu la damu husaidia kuzuia kutokea kwa mtoto wa jicho.
Tiba
Hali ya mtoto wa jicho inaweza kutibika kwa kuondoa lenzi yenye ukungu kwa njia ya upasuaji mdogo usiotumia mda mrefu ikiwa uvaaji wa miwani maalumu utashindwa kurekebisha hali hii.