Moyo wa Nguruwe Wapandikizwa kwa Binadamu

1 Min Read

Jaribio la pili la kupandikiza moyo wa nguruwe kwa binadamu limefanyika kwa ufanisi mkubwa.

Jaribio hili lilihusisha binadamu wawili ambao kila mmoja aliwekewa moyo mpya wa nguruwe baada ya kufariki, huku wakiendelea kuwepo kwenye mashine maalumu za usaidizi wa kutunza uwezo wa moyo katika kusukuma damu.

Jaribio hili lililodumu kwa siku tatu ni la pili kufanyika mwaka huu baada ya kufariki kwa mgonjwa wa kwanza aliyefanyiwa pandikizi la kwanza kabisa duniani mapema mwaka huu.

Majibu ya jaribio la sasa yanaleta ahueni na matumaini mapya kwenye kuhudumia watu walio na changamoto za magonjwa ya moyo yanayohitaji upandikizaji wa moyo mpya kwa kuwa maambukizi ya virusi vya nguruwe hayakuathiri watu hawa, pia miili yao haikuukataa moyo waliowekewa.

Kwa mujibu wa takwimu za Organ Donor Gov, mwaka 2021 watu 40,000 duniani walipokea viungo kutoka kwa watu wengine ili kuokoa maisha yao.

Aidha, wastani wa watu 17 hufariki kila siku duniani kutokana na kukosa watu wa kuwasaidia viungo ili waendelee kuishi.

Mbinu za kuvuna viungo vya wanyama zinalenga kuokoa maisha ya watu wanaokosa viungo mbadala kutoka kwa binadamu, pia idadi ya watu walio tayari kuchangia imekuwa inapungua kila mwaka.

Jaribio hili limefanyika New York University (NYU)

Share This Article