Dostarlimab: Dawa Iliyoonesha Mafanikio Asilimia 100 Kutibu Saratani

2 Min Read

Kwa mara ya kwanza kwenye historia ya tiba duniani, Dostarlimab dawa iliyokuwa inafanyiwa majaribio kwenye kutibu saratani ya utumbo mkubwa imeonesha ufanisi kwa asilimia 100 kwenye kufuta kabisa seli za saratani.

Ni ahueni mpya kwa wagonjwa wa saratani duniani.

Baada ya kufanyiwa majaribio kwa miezi 6 ikihusisha wagonjwa 12, majibu yake yamekuwa na ufanisi wa asilimia 100 kwenye kuondoa kabisa ugonjwa huu.

Hii inamaanisha kuwa sasa wagonjwa wa saratani wanaweza kabisa kupona kirahisi kwa dawa pekee pasipo kupitia hatua zingine za matibabu kama mionzi.

Dawa hii inayofahamika pia kwa majina ya kibiashara ya Jemperli au GlaxoSmithKline LLC iliidhinishwa na mamlaka ya udhibiti wa vyakula na dawa FDA mwaka 2021 ili itumike kutibu saratani ya mji wa uzazi.

Tafiti za sasa zinalenga kupanua wigo wa matumizi yake kwenye kutibu aina mbalimbali za saratani zinazo mkabili binadamu.

Kwa mujibu wa chapisho halisi la utafiti huo, wagonjwa wote hawajapata maudhi makubwa yanayozidi kiwango cha tatu cha athari zake.

Ugonjwa huu unaopatikana kwenye aina zaidi ya 200, husababisha vifo vya wastani wa watu milioni 10 kila mwaka.

Hutokana na kukosekana kwa udhibiti wa taarifa wezeshi zinazoongoza ukuaji na vifo vya seli za mwili ambazo ndiyo kitovu cha uhai.

Taarifa za kiuchunguzi zinabainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2040, idadi ya wagonjwa wapya kwa mwaka itaongezeka kufikia watu milioni 29.5 na vifo milioni 16.4

Kwa mujibu wa WHO, sataratani za mapafu, tezi dume, utumbo mkubwa na puru, tumbo na ini ndizo huongoza kwa wanaume huku saratani za matiti, utumbo mkubwa na puru, mapafu, mlango wa kizazi na tezi za thyroid zikiongoza kwa wanawake.

Nchini Tanzania, saratani zinazoongoza kwa kuua ni mlango wa kizazi, koromeo, ini na tezi dume.

Share This Article