Mbinu 12 za Kupunguza Maumivu ya Hedhi

8 Min Read

Umri wa kuvunja ungo hutofautiana miongoni mwa mabinti.

Huu ndiyo mwanzo wa hedhi ambayo hudumu kwa walau miongo mitatu hadi minne mbele.

Katika utafiti mmoja, ilibainika kuwa wastani wa idadi ya hedhi ambazo mwanamke hupata kwenye kipindi cha umri wake wote wa uhai wa afya ya uzazi ni hedhi 451.

Hii ni sawa na wastani wa hedhi 13 kila mwaka, kwa miaka 35 mfululizo.

Sababu za Maumivu

Tendo hili la kiasili na kibaiolojia halijawahi kuwa rafiki kwa wanawake wengi.

Hutawaliwa na uwepo wa maumivu makali, pamoja na mambo mengine yanayohusu mabadiliko ya hali na tabia za mwili.

Chanzo cha kwanza na kikuu cha maumivu ya hedhi ni uwepo wa vichocheo vingi vya prostaglandins ambavyo huzalishwa wakati huu.

Vichocheo hivi huuamuru mji wa uzazi ujivute na kuvunja kuta zake, pamoja na kuibana mishipa ya damu ili isiendelee kupeleka damu na virutubisho.

Maumivu haya hutokea baada ya misuli ya mji wa uzazi kukosa hewa. (1,2,3)

Baadhi ya njia zinazoweza kutumika kwenye kupunguza maumivu ni hizi.

1. Maji ya Moto

Kujikandia maji ya moto ya wastani wa 104 au degree F (40 degree C) sehemu ya chini ya tumbo, nyonga, kiuno na mgongo husaidia kupunguza maumivu haya.

Hupanua mishipa ya damu na kuongeza usambazwaji wa hewa kwenye mji wa uzazi.

Kuna vifaa maalumu vinavyoweza kusaidia kukamilisha zoezi hili, lakini taulo au kitambaa kinaweza pia kutumika. (4)

Kwa kuwa maji ya moto yanaweza kuunguza mwili, kusababisha vidonda au kusababisha maumivu ni muhimu sana kufanya jambo hili kwa tahadhari kubwa.

2. Chai za Mitishamba

Hauwezi kubeza mchango wa tiba asili na tiba mbadala katika kupunguza maumivu ya hedhi.

Ni muhimu kama mwanamke atakuwa anatumia aina hii ya chai kila siku ili kuandaa mazingira rafiki ya kupunguza maumivu kwenye wakati muafaka.

Baadhi ya mitishamba iliyobainishwa na tafiti kuwa na uwezo wa kupunguza maumivu ya hedhi ni mdalasini, tangawizi, binzari manjano, chai ya rangi, majani ya mti wa mpera pamoja na shamari. (5,6,7)

Aidha, aina hii ya chai inaweza pia kutumika siku mbili hadi tatu kabla ya hedhi, au zinaweza kutumika siku hiyo hiyo ya hedhi.

3. Yoga

Yoga ni mazoezi jumuishi yanayohusisha mwili na akili.

Asili yake ni nchi ya India zaidi ya miaka 5000 iliyopita. (8)

Mazoezi ya yoga hupunguza wasiwasi, huongeza kujiamini, huongeza usambazwaji wa damu kwenye viungo vya mwili pamoja na kupunguza maumivu ya hedhi. (9,10,11)

Kama unataka kujua aina mbalimbali za mazoezi haya soma hapa.

4. Dawa

Dawa za kuondoa maumivu husaidia kwenye kuikabili changamoto hii.

Matumizi ya dawa kama ibuprofen, naproxen, mefenamic acid hufaa sana zikitumika wakati huu. (12,13)

Hata hivyo, kila dawa huwa na athari kwa afya hasa inapotumika pasipo kufuata masharti sahihi.

Ni muhimu kuongea na mfamasia au daktari kabla haujaamua kutumia dawa hizi ili kujiepusha na madhara makubwa yanayoweza kutokea kwa afya.

5. Massage

Tafiti za afya zinathibitisha kuwa kufanyia massage sehemu ya chini ya tumbo kwa kutumia mafuta ya mimea husaidia kupunguza maumivu ya hedhi.

Baadhi ya mafuta hayo ni lavender, mti wa chai ya rangi, mkaratusi, mdalasini, chamomile, rose na mkarafuu. (14,15)

Ili massage hii iweze kuleta majibu chanya inapaswa kufanyika walau mara 4 kwa siku.

6. Mlo na Vinywaji

Mlo ambao mwanamke hutumia wakati wa hedhi pamoja na vinywaji huchangia kwenye kupunguza au kuongeza ukubwa wa maumivu ya hedhi.

Kuacha au kupunguza matumizi ya vyakula vinavyojaza gesi na kubakiza maji mengi mwilini hasa vile vyenye mafuta mengi mfano chips na unywaji wa pombe hufaa sana wakati huu. (16,17,18)

Aidha, ni muhimu pia kupunguza matumizi ya vyakula vyenye sukari na chumvi nyingi kwa kuwa huhusishwa kwenye kuongeza ukubwa wa maumivu ya hedhi.

7. Sex

Ushiriki wa tendo la ndoa wakati wa hedhi huamuliwa na sababu nyingi zikiwemo za kiimani na kimazingira.

Hakuna ushahidi wa moja wa moja unaothibitisha kuwa kushiriki tendo la ndoa wakati wa hedhi husaidia kupunguza maumivu hayo, lakini kuna misingi ya kisayansi inayoweza kutumika kwenye kuonesha uhusiano wa tendo hili na kupunguza maumivu.

Tendo la mwanamke kufika kileleni huleta faida kwa mwili mzima.

Huamuru ubongo uzalishe kemikali na vichocheo vya furaha ambavyo hufanya pia kazi ya kupunguza maumivu ya mwili.

Mfano, utafiti wa mwaka 1985 unaonesha kuwa msisimko wa kihisia unaoanzia kwenye uke huongeza mara mbili zaidi uwezo wa mwanamke kuvumilia maumivu.

8. Virutubisho

Mafuta ya omega 3 husaidia kupunguza maumivu ya hedhi.

Matumizi ya virutubisho hivi huongeza ufanisi wa dawa za kupunguza maumivu.

Mfano, kwenye utafiti mmoja ilibainika kuwa wanawake wanaotumia mafuta ya omega 3 walipona maumivu yao kwa kutumia dozi ndogo zaidi za dawa za ibuprofen kuliko wale ambao hawakutumia virutubisho hivyo. (19)

Utafiti mwingine unaonesha kuwa matumizi ya mafuta ya samaki yanafaa zaidi kutuliza maumivu kuliko dawa za ibuprofen. (20)

Aidha, matumizi ya zinc na magnesium husaidia pia kutatua changamoto hii.

9. Pata Vipimo

Kuna makundi mawili ya maumivu ya hedhi.

Kundi la kwanza huwakilisha aina ya maumivu ambayo sababu za kutokoea kwake huwa zipo wazi na hayachangiwi na uwepo wa aina yoyote ya mapungufu, au uwepo wa ugonjwa wowote kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamke. (21)

Kundi la pili huwakilisha aina ya maumivu ambayo sababu za kutokea kwake huhusishwa na uwepo wa changamoto kadhaa kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamke hasa uvimbe wa aina yoyote na mvurugiko wa homoni. (22)

Ni muhimu kwa mwanamke kufanya uchunguzi wa afya yake ikiwa maumivu haya ni makubwa sana ili chanzo sahihi cha maumivu kiweze kushughulikiwa.

10. Ongeza Maji

Kama mwili wako hauna maji ya kutosha, uwezekano wa kupatwa na maumivu makali sana huwa ni mkubwa.

Kuongeza unywaji wa maji kufikia walau glasi 8 kwa siku huhusishwa na kupungua kwa siku za kutoka kwa damu ya hedhi pamoja na kupungua kwa maumivu. (23)

11. Uzazi wa Mpango

Kama mbinu mbadala hazisaidii, na ikiwa matumizi ya dawa za kawaida hayaleti majibu tarajiwa, unaweza kuzungumza na daktari wako ili akuruhusu utumie njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Njia hizi hutumika kwa kuwa nyingi hutengenezwa kwa kutumia vichocheo vya asili ambavyo hufanana na vile ambavyo mwili wa mwanamke huvizalisha.

Ikiwa maumivu hayo yanasababishwa na changamoto fulani za vichocheo, njia kama majira, depo provera, vijiti na kitanzi zinaweza kusaidia.

12. Mazoezi

Tafiti za afya zinabainisha kuwa kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia kupunguza maumivu ya hedhi. (24)

Mazoezi hupunguza pia changamoto zingine za hedhi kama tumbo kujaa gesi, uchovu na hasira.

Muhtasari

Kikombe cha hedhi, pedi au tampon zinaweza kutumika kujisitiri wakati wa hedhi kutokana na jinsi ambavyo mwanamke mwenyewe ataona inafaa.

Kutokana na uwepo wa maumivu makali, ni muhimu kuchagua njia ya kujisitiri itakayokuwa rafiki zaidi ili kutokuongeza maumivu hayo.

Share This Article