Sehemu hii inaelezea kwa ufupi viungo tofauti vinavyounda mfumo wa uzazi wa mwanamke.
Kwa uelewa wa kawaida kabisa, tunaweza kuugawa mfumo huu kwenye sehemu kuu mbili ambazo ni sehemu ya ndani ya mwili pamoja na sehemu ya nje ya mwili.
1. Sehemu ya Ndani
Sehemu hii huundwa na vifuko vya mayai, mirija ya uzazi, mji wa uzazi na uke.
Kila sehemu ya mfumo huwa na muundo maalumu wenye lengo la kufanikisha kazi zake kikamilifu.
Ovary
Hivi ni vifuko vya mayai.
Kabla ya kuvunja ungo, kuta za vifuko hivi huwa na ngozi nyororo lakini baada ya kuvunja ungo na kuanza jukumu kubwa la kutoa mayai ya uzazi kila mwezi, ngozi yake hukomaa na kuwa ngumu.
Huwa na wastani wa urefu wa 3-4 cm, upana wa 1.5-3 cm na unene wa 1-1.5cm.
Hufanya kazi ya kutoa mayai ya uzazi pamoja na kuzalisha vichocheo vya kike.
Mirija ya Uzazi
Huwa na wastani wa urefu wa 10 cm na upana wa 1 cm.
Ni mirija midogo sana inayounganisha ovary na sehemu ya juu ya mji wa uzazi.
Kupitia mirija hii, yai husafiri kutoka kwenye ovary kwenda kwenye mji wa uzazi, pia ndiyo sehemu ambayo ujauzito hutungwa.
Hii inatoa maana kuwa, mbegu za kiume huogelea kwenye mirija hii zikilitafuta yai ili lirutubishwe.
Ikitokea yai limerutubishwa husafirishwa kwenda kwenye mji wa uzazi ili lijishikize na kulelewa kama ujauzito.
Uwepo wa mapungufu yoyote kwenye mirija ya uzazi ikiwemo maambukizi ya magonjwa mfano PID, kaswende na kisonono pamoja na kuziba kwa mirija hii husababisha changamoto za uzazi kwa mwanamke ikiwemo ugumba.
Uterus
Hufahamika zaidi kama mji wa uzazi.
Kwa mwanamke asiye na ujauzito, mji wa uzazi huwa na walau urefu wa 6.5-7.5 cm, upana wa 4.5-5.5 cm na unene wa 2.5-3 cm huku uzito wake ukiwa ni 30-40 g.
Wakati wa ujauzito, ukubwa wa mji wa uzazi huongezeka mara 500 zaidi ili kumtunza mtoto.
Kiungo hiki hutengenishwa na uke kwa mfereji mwembamba unaoundwa na mlango wa uzazi.
Uke
Ni mfereji unaotenganisha mji wa uzazi na sehemu za nje za mfumo wa uzazi wa mwanamke.
Ndiyo sehemu inayopokea uume wakati wa tendo na ndoa, pia ni sehemu ya asili inayotumika kutoa damu ya hedhi pamoja na kuuleta uhai mpya duniani wakati wa kujifungua.
Uke umeundwa kwa mishipa mingi ya fahamu, mishipa ya damu pamoja na misuli inayoweza kutanuka na kusinyaa huku ikitunza asili yake.
Urefu wake unafikia 7-14 cm na upana wake ukiwa ni wastani wa 2.5-3 cm huku ukuta wa misuli yake ya mbele ukiwa na wastani wa 4.4-8.4 cm.
Tofauti na jinsi inayoaminika mitaani, umbo la mwanamke pamoja na ukubwa au udogo wa mwili wake haviwezi kutoa ishara ya urefu wa shimo la uke.
Ukubwa wa kiungo hiki huongezeka kadri unavyokwenda ndani yake, ukielekea kwenye mlango wa kizazi.
2. Sehemu ya Nje
Huundwa kwa mashavu ya uke, tezi za bartholin pamoja na kisimi.
Mashavu Makubwa
Hufunika na kulinda sehemu za ndani za mfumo wa uzazi wa mwanamke.
Huwa na tezi zinazozalisha joto na mafuta, pia ni sehemu ambayo nywele huanza kuota pindi mwanamke afikiapo umri wa kuvunja ungo.
Kwa lugha rahisi, hii ni sehemu ambayo hugusana moja kwa moja na nguo ya ndani ya mwanamke.
Mashavu Madogo
Huwa na upana wa walau nchi 2 japo kipimo hiki kinaweza kuwa kidogo au kikubwa zaidi kwa baadhi ya wanawake.
Hupatikana chini ya mashavu makubwa yakizunguka matundu ya uke pamoja na mkojo.
Tezi za Bartholin
Hupatikana kwenye kila upande wa tundu la uke.
Tezi hizi ziligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1677 na Caspar Bartholin Secundus.
Kazi yake kubwa ni kuzalisha majimaji au ute unaosaidia kulainisha uke.
Kisimi
Tunaweza kulinganisha kiungo hiki na uume kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamme.
Hufunikwa na ngozi inayoitwa prepuce ambayo ni sawa na govi kwenye uume.
Kisimi kinaweza kusimama, ndiyo kiungo chenye msisismko mkubwa zaidi kwenye mwili wa mwanamke na kimetengenezwa kwa mishipa ya fahamu zaidi ya 8000.
Muhtasari
Kila sehemu inayounda mfumo huu huwa na maana kubwa sana kwenye afya ya uzazi wa mwanamke.
Uwepo wa mapungufu kwenye sehemu yoyote kunaweza kusababisha changamoto nyingi ikiwemo ugumba, kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi pamoja na maumivu makali wakati wa kushiriki tendo la ndoa.
Kama unapitia changamoto zozote kwenye mfumo wa uzazi, pata msaada wa ushauri na tiba.