Hufahamika pia kwa jina lingine la pyridoxine.
Hii ni vitamini inayochanganyikana na maji.
Mwili wa binadamu hauna uwezo wa kuzalisha vitamini hii hivyo ni lazima uipate kutoka kwenye vyakula na virutubisho mbadala.
Kwa mujibu wa taasisi ya National Institutes of Health (NIH), kiwango cha mahitahi ya kila siku cha vitamini hii kwa mtu mwenye umri wa miaka 19-50 ni 1.3 g.
Wanawake wajawazito ni 1.9 mg, wanaonyonyesha ni 2 mg na wazee zaidi ya miaka 50 ni 1.7 mg.
Vyanzo
Unaweza kuipata vitamini hii kwa wingi kutoka kwenye nyama, samaki, viazi vya aina zote, maharage ya soya, ndizi na maziwa.
Unaweza pia kuipata kwenye mayai, karoti, spinachi na parachichi.
Vitamini hii huwa na faida kubwa kwa afya.
Baadhi ya faida zinabainishwa na tafiti tulizojadili hapa.
1. Saratani
Watu wasiopata kiasi cha kutosha cha vitamini B6 huwa kwenye hatari ya kuugua aina mbalimbali za saratani mwilini.
Mfumo unaotumika kwenye kukinga saratani haupo wazi sana, lakini inaaminika kuwa pengine uwezo wake wa kuzuia uvimbe joto ndiyo husaidia katika kukamilisha kazi hii. (1,2)
Baadhi ya saratani zinazoweza kukingwa na vitamini hii ni utumbo mkubwa na matiti. (3,4,5,6)
2. Hedhi
Baada ya kuvunja ungo, mwanamke huanza kupata hedhi ambayo hudumu kwa wastani wa miongo mitatu hadi minne mbele.
Tendo hili la kibaiolojia huambatana na dalili nyingi ambazo huwa siyo rafiki kwa wanawake wengi.
Wastani wa wiki moja kabla ya kutokea kwa hedhi, baadhi ya wanawake hukumbwa na tatizo la kubadilika kwa mihemko ya mwili hasa ikihusisha hasira, furaha na huzini, kusahau mambo, kutokwa na chunusi, kuvimba kwa matiti pamoja na tumbo kujaa gesi.
Hizi ni dalili chache tu kati ya nyingi.
Matumizi ya vitamini B6 husaidia kupunguza ukubwa au hata kuzuia kabisa kutokea kwa dalili hizi. (7,8)
Wanawake wanashauriwa kutumia virutubisho hivi ili kupunguza adha hii ambayo wengi huwafanya wasiwe na furaha.
3. Mfumo wa Damu na Moyo
Hupunguza wingi wa kemikali za homocysteine kwenye damu.
Hii ni aina ya protini inayopatikana kwa kiasi kikubwa kutoka kwenye nyama.
Ni chanzo kikubwa cha matatizo mengi yanayohusisha moyo na mfumo wa damu kwa ujumla wake ikiwemo kuganda kwa damu kwenye mishipa. (9)
Vitamini B6 hutumiwa na mwili kwenye kuvunja na kuipunguzia makali kemikali hii ili isilete athari mbaya kwa afya. (10,11)
Ufanisi mkubwa kwenye kazi huu huonekana kama itatumiwa pamoja na foliki asidi.
4. Magonjwa ya Akili
Tafiti zinabainisha kuwa wazee wanaotumia kiasi cha kutosha cha vitamini B6 huwa na uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu kuliko wale wanaopata kiasi kidogo. (12,13)
Husaidia pia kutibu pamoja na kuzuia kutokea kwa magonjwa ya akili pamoja na kuboresha afya ya ubongo. (14,15)
Ili majibu mazuri zaidi yaweze kupatikana ni muhimu kama itatumiwa pamoja na foliki asidi kwa kuwa hushirikiana kwa pamoja kwenye kufanya kazi.
5. Kiungulia na Kutapika
Tatizo la kiungulia na kutapika huathiri asilimia 70-80 ya wanawake wote wanaoshika ujauzito.
Japokuwa changamoto hii inaweza kutokea muda wowote ule wa siku, huwekwa kwenye kundi la matatizo yanayoitwa kwa lugha ya ujumla kuwa ni magonjwa ya asubuhi.
Chaguo la kwanza kwa wanawake wenye changamoto hii ni kumeza vidonge au kutumia virutubisho vyenye vitamini B6. (16,17)
Wagonjwa wenye saratani pamoja na wale ambao husumbuliwa na tatizo la kutapika mara kwa mara wanaweza pia kutumia vitamini hii.
6. Kifua Kikuu
Watu wanaotumia dawa za kutibu kifua kikuu hasa Isoniazid huwa kwenye hatari kubwa ya kuharibikiwa na mishipa ya fahamu inayopatikana nje ya ubongo na uti wa mgongo.
Mfumo wa usambazwaji wa taarifa za mwili huingiliwa na uwezo wa mwili kwenye kusambaza taarifa kuelekea sehemu mbalimbali hupungua hupungua.
Tatizo hili kitaalamu huitwa Peripheral Neuropathy.
Miongoni mwa dalili chache za uwepo wa tatizo hili ni maumivu, kuwaka moto pamoja na kufa ganzi kwa miguu na mikono.
Matumizi ya vitamini B6 husaidia kuzuia kutokwa kwa changamoto hii pamoja na kupunguza ukubwa wake kwa wale ambao tayari wameshaathirika. (18,19)
7. Degedege
Tatizo la degedege na kifafa husababishwa na uwepo wa mapungufu kwenye ubongo ambayo hufanya uzalishwe umeme mkubwa kuliko kiwango cha kawaida kinachotakiwa.
Tatizo hili linaweza kutokea wakati wa kuzaliwa, au kwenye kipindi chochote cha uhai wa binadamu.
Upungufu wa vitamini B6 huhusishwa na kutokea kwake hasa kwa watoto kuliko watu wazima. (20,21)
Ni muhimu kama watoto watapatiwa vyakula na virutubisho vyenye vitamini hii ili kuwakinga na tatizo la degedege.
8. Figo
Uwepo wa chumvi nyingi kwenye figo huwa ni chanzo kikubwa cha kutokea kwa mawe kwenye kiungo hiki.
Utafiti mmoja uliofanyika kwa wanawake unaonesha kuwa vitamini B6 husaidia kwenye kuzuia kutokea kwa mawe kwenye figo. (22)
9. Sonona
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), asilimia 5 ya watu wazima duniani wanakabiliwa na tatizo hili.
Aidha, zaidi ya watu 700,000 duniani hujiua kila mwaka kutokana na changamoto hii ya sonona.
Ugonjwa huu wa akili humfanya mtu awe mnyonge sana, asijione kuwa na umuhimu wowote duniani na hufikiria kujiua kama njia pekee ya kuondokana na matatizo ya duniani.
Vitamini B6 huhusika katika kuzalisha na kuratibu vichocheo vya furaha na hisia hasa GABA, dopamine na serotonin.
Watu wenye sonona huhusishwa na uchache wa vitamini B6. (23,24)
Ongeza matumizi yake, jikinge na sonona.
Upungufu Wake
Watu wasiopata kiasi cha kutosha cha vitamini B6 huwa na dalili za kupungukiwa damu, mabaka ya ngozi yanayowasha, kukauka kwa ngozi ya mdomo pamoja na kuvimba kwa ulimi.
Aidha, husababisha sonona kwa watu wazima na degedege kwa watoto.
Muhtasari
Matumizi makubwa yanayozidi kiasi cha kawaida cha vitamini hii husababisha mwili ukose udhibiti hasa kwenye miondoko ya misuli.
Inaweza pia kusababisha kiungulia, kichefuchefu na kuungua kwa macho wakati wa jua kali.
Athari hizi huwa siyo za kudumu.
Huisha ndani ya muda mfupi baada ya kuacha au kupunguza kutumia vitamini hii.