Calcium: Faida 6 Muhimu kwa Afya ya Binadamu

4 Min Read

Uti wa mgongo wa binadamu ndiyo kiunzi kinacho shikilia mifupa yote ya mwili.

Mifupa hii huupa mwili muonekano wake halisi pamoja na kulinda baadhi ya viungo vya mwili.

Aidha, mifupa hufanya kazi ya kutunza baadhi ya madini ya mwili, pia ni sehemu ambayo damu hutengenezwa.

Tumezungumza kuhusu mifupa kwanza kwa sababu zaidi ya asilimia 99 ya madini ya calcium hutunzwa humo.

Uhitaji

Kwa mujibu wa taasisi ya National Institutes of Health (NIH), hiki ndicho kiasi cha calcium ambacho kila umri huhitaji kupata kila siku;

  • Miaka 19–50 ni 1000 mg
  • Miaka 51–70 ni 1000 mg kwa wanaume na 1200 mg kwa wanawake
  • Miaka 71 na zaidi ni 1200 mg

Uhitaji wa madini haya unaweza kuongezeka wakati wa ujauzito, kwa wanawake waliofikia umri wa ukomo wa hedhi pamoja na watu wasiotumia kabisa nyama.

Madini haya huwa na faida kubwa sana kwa afya.

1. Mifupa na Meno

Asilimia 99 ya mifupa na meno hufanywa kwa madini haya.

Huongeza ubora wa afya ya mifupa, kuunganisha mifupa, kuongeza ujazo wake pamoja na kupunguza changamoto za kuvunjika kwa mifupa. (1,2)

Huongeza ubora wa meno. Watu wenye kiasi kidogo cha calcium hukumbwa na matatizo ya kupoteza meno yao kuliko wale wenye kiasi cha kutosha cha calcium.

2. Hedhi

Kabla ya kutokea kwa hedhi, wanawake hupatwa na dalili nyingi ikiwemo kutokwa na chunusi, kuongezeka kwa mihemko, mafua, kuvimba kwa matiti pamoja na kupendelea baadhi ya vyakula.

Hizi ni dalili chache tu kati ya nyingi.

Madini ya calcium husaidia kwenye kupunguza ukubwa wa dalili hizi. (3)

Wanawake wanashauriwa kutumia virutubisho vyenye wingi wa madini haya ili wanufaike na faida hii.

3. Presha

Madini ya calcium husaidia kwenye kudhibiti ongezeko la juu la msukumo wa damu yaani presha.

Hufaa kwa kila mtu, lakini zaidi kwa watu wenye ugonjwa huu.

4. Saratani

Saratani ni ugonjwa mbaya sana.

Mwaka 2020, ugonjwa huu ulisababisha vifo vinavyokaribia milioni 10 duniani. (4)

Tafiti zinabainisha uwezo wa madini ya calcium katika kuzuia saratani ya utumbo mkubwa. (5,6)

Jikinge na saratani kwa kutumia virutubisho hivi kwa wingi.

5. Misuli

Madini ya calcium husaidia kuratibu na kuboresha mijongeo ya misuli ya mwili.

Pasipo uwepo wa madini haya, misuli isingekuwa na uwezo wa kukamilisha mijongeo yake inayohusisha kutanuka na kusinyaa.

6. Mfumo wa Damu na Moyo

Utaratibu wa kuganda kwa damu baada ya kupatwa na jeraha huwa na hatua nyingi.

Mojawapo ya hatua hizo huhitaji uwepo wa calcium ili iweze kufanikiwa.

Ni muhimu katika kugandisha damu. (7,8,9)

Madini haya huhitajika pia kwenye kuwezesha misuli ya moyo katika kufanikisha kazi zake.

Vyanzo

Yogurt pamoja na bidhaa zingine za maziwa huwa ni vyanzo vizuri vya calcium.

Hupatikana pia kwenye cheese, samaki, almonds, bamia, maharage ya soya na broccoli.

Siku za hivi karibuni kumekuwa na virutubisho vingi vinavyouzwa vikiwa na madini haya. Unaweza pia kuvitafuta. Hata hivyo, matumizi ya kiwango kikubwa husababisha kujaa kwa gesi tumboni pamoja na choo kigumu.

Inaweza pia kusababisha kutengenezwa kwa mawe kwenye figo.

Muhtasari

Baada ya kufikia umri wa ukomo wa hedhi, wanawake hukabiliwa na changamoto nyingi za mifupa ikiwemo kuvunjika kirahisi pamoja na maumivu ya maungio yake.

Virutubisho hivi vina maana kubwa sana kwao.

Aidha, madini ya calcium hufaa zaidi yakitumiwa pamoja na virutubisho vya vitamini D ili kuongeza ufanisi wa kazi zake.

Share This Article