Dawa za Kuzuia Maambukizi ya VVU Baada ya Kupitia Mazingira Hatarishi

4 Min Read

Pengine umewahi kuwaza, ikitokea umepata ajali, au labda umepitia mazingira yenye hatari ya kukufanya uambukiwe virusi vya UKIMWI utafanya nini?

Au pengine umewahi huwaza, kinga ya kukufanya usiambukiwe virusi vya UKIMWI ipo?

Kama ipo, inafanya vipi kazi, na ufanisi wake upoje?

Ukweli

Njia ya kukukinga usipatwe na maambukizi ya VVU baada ya kupitia mazingira au hali hatarishi ipo.

Kitaalamu huitwa Post-Exposure Prophylaxis, au kwa kifupisho PEP.

Ni njia inayohusisha matumizi ya wiki nne ya dawa za kutibu VVU kama kinga ya dharura kwenye kuzuia kutokea kwa maambukizi mapya.

Muda Sahihi

Ni njia ya dharura inayopaswa kufanyika kwa uharaka.

Mhusika hushauriwa kuanza dozi ya dawa husika ndani ya masaa 2 tangu apatwe na changamoto husika.

Inaweza pia kufanyika muda wowote ndani ya saa 72 za mwanzo.

Utaratibu Upoje?

Mhusika anapaswa kufika kwenye hospitali yoyote ya serikali ili apatiwe msaada, pamoja na kupimwa kwanza kama tayari ni muathirika wa VVU au la.

Vipimo hivi vinapaswa kufanywa haraka ili kumsaidia mhanga.

Pasipo kujali ni mazingira yapi yalifanya mhusika apatwe na hali hii, msaada wa ushauri wa kisaikolojia hupaswa kutolewa.

Kwa watu waliobakwa, taratibu za kisheria huhusishwa pia ikiwemo kupata ripoti ya polisi pamoja na taratibu zingine kama ambavyo sheria za nchi zinaelekeza.

Ufanisi

Dawa hizi hazina ufanisi wa asilimia 100 katika kuzuia VVU.

Tafiti zinaonesha kuwa huwa na ufanisi wa asilimia 81 katika kuzuia maambukizi mapya ya VVU.

Ifahamike kuwa ufanisi wa dawa hizi huendelea kupungua kadri mhusika anavyozidi kuchelewa kuanza kuzimeza hivyo ni muhimu kuanza mapema dozi ya kwanza.

Changamoto

Baadhi ya watu hupata VVU hata baada ya kumeza vidonge hivi.

Hali hii inaweza kuwa imesababishwa na mambo yafuatayo;

  • Kukawia sana kuanza kumeza dawa (1,2)
  • Kutokumeza kwenye baadhi ya siku, au kutokumaliza dozi nzima ya vidonge 28
  • Kushambuliwa na aina ya VVU ambayo ni sugu kwa aina ya dawa zilizo tumika kama kinga (3, 4)
  • Kuendelea kuwepo kwenye hali au mazingira yaleyale yenye hatari ya kuambukizwa

Mazingira Hatarishi

Baadhi ya mazingira na hali hatarishi ni kupasuka kwa kondomu wakati wa tendo la ndoa, ajali yoyote inayohusisha vifaa vyenye ncha kali kama viwembe na sindano pamoja na kubakwa.

Dawa hizi hutolewa kwa mazingira ya dharura pekee, siyo mbadala wa njia za kudumu za kujikinga na VVU na hazifai kwa watu ambao kila mara hupitia changamoto ileile inayowafanya wawe hatarini kuambukizwa.

Ikiwa wewe ni muathirika wa VVU, au unaishi kwenye mazingira yenye hatari kubwa ya kukufanya upate VVU unapaswa kuzungumza na mtoa huduma ili akupe mbadala wa njia hii.

Muhtasari

Kwa Tanzania, TDF 300mg+3TC 300mg+DTG 50mg au maarufu zaidi kama TLD ndiyo dozi ya dawa inayotumika kwa watu wazima.

Kwa watoto, AZT+3TC+LPV/r ndiyo hutumika.

Lakini, ikiwa uzito wa mtoto ni zaidi ya kilo 20, DTG inaweza kuwekwa kama mbadala huku msingi wa AZT+3TC ukibakizwa.

Aidha, dawa hizi hutolewa bure kwenye hospitali zote za serikali. Kama itawezekana, watu wote waliohusika kwenye ajali hii wanaweza kutafutwa ili wapewe msaada.

Ikiwa haitawezekana, mtu aliye tayari kupata msaada huu ndiye ashughulikiwe peke yake.

Share This Article