Dawa za Kuzuia Maambukizi ya VVU Kabla ya Kupitia Mazingira Hatarishi

4 Min Read

Kama ambavyo mtu anaweza kumeza dawa ili ajikinge na VVU baada ya kupitia mazingira au hali hatarishi inayoweza kumfanya aambukizwe, hali ipo hivyo pia kwa upande mwingine wa kuzuia maambukizi haya kabla mhusika hajapitia mazingira hatarishi.

Njia hii huitwa PrEP, au Pre-Exposure Prophylaxis.

Ni matumizi ya kila siku ya dawa za VVU kwa watu wasio na VVU ili kuwakinga wasipatwe na ugonjwa huu baada ya kujiingiza kwenye mazingira hatarishi.

Hutumiwa kila siku na watu wasio na VVU ili kuwapunguzia nafasi ya kupata maambukizi.

Ufanisi

PrEP huwa na ufanisi wa asilimia 99 katika kuzuia maambukizi yatokanayo na tendo la ndoa.

Kwa watu wanaotumia madawa pamoja na kujichoma sindano, huwa na ufanisi wa asilimia 74.

Aidha, ufanisi wake hupungua inapotumika pasipo kufuata masharti sahihi.

Vilevile hutoa kinga ya VVU pekee hivyo kondomu inaweza kutumiwa ili kutoa kinga ya magonjwa mengine ya zinaa pamoja na kuongeza kinga kwa watu wasiofuata masharti sahihi ya matumizi yake.

Masharti ya Kutumia

Muongozo wa Serikali ya Tanzania unataka mhusika awe na miaka 15 na kuendelea, asiwe na VVU pamoja na ulazima wa kuwa kwenye mazingira hatarishi.

Pia, mhusika anatakiwa akubali kutii masharti yote yanayohusisha matumizi ya dawa hizi pamoja na kuwa na uwezo wa kutoa creatinine kwa kiasi kinachozidi 60 ml kwa dakika.

Makundi haya kwa mujibu wa mwongozo wa serikali ya Tanzania hayakidhi masharti ya kutumia dawa hizi.

  • Umri chini ya miaka 15
  • Watu wasio na uwezo wa kutoa creatinine kwa kiasi kinachozidi 60 ml kwa dakika
  • Watu wasio na makazi maalumu, au wale wanaohama hama kutoka sehemu moja kwenda nyingine
  • Wasiokuwa tayari kumeza dawa hizi kila siku
  • Wenye mzio na dawa hizi

Mazingira Hatarishi

Mazingira au hali hatarishi inayoweza kukidhi masharti ya matumizi ya dawa hizi inaweza kuwa miongoni mwa makundi haya;

  • Una mwenzi mwenye maambukizi ya VVU, iwe anajulikana au kama nakala za virusi hazionekani tena kwenye kipimo
  • Unajichoma madawa ya kulevya
  • Unashiriki ngono ya kawaida ya uke au sehemu ya haja kubwa pasipo kutumia kondomu kwa mtu zaidi ya mmoja
  • Kama unatumia PEP
  • Kama ni mwanamke anaishi na mwanamme mwenye VVU na anataka kubeba ujauzito
  • Unashirikiana vifaa vyenye ncha kali na kundi kubwa la watu
  • Umegunduliwa kuwa na maambukizi mapya ya ugonjwa wowote wa zinaa miezi 6 ya nyuma

Dawa Husika

Kwa mujibu wa serikali ya Tanzania, Emtricitabine200mg+Tenofovir Disoproxil Fumarate300mg ndiyo chaguo linalotumika.

Nchi zingine huwa na miongozo yao pia.

Siku za hivi karibuni, sindano mpya inayoitwa Apretude inayotoa kinga kwa miezi 2 imethibitishwa na FDA kutumika.

Kusitisha Matumizi

Watu wanaotumia PrEP hupaswa kufuatiliwa mara kwa mara ili kuona kama kuna athari zozote za kiafya wanazopitia.

Dawa hizi zinaweza kusitishwa ikiwa mhusika atapa maambukizi ya VVU, wakiondoka kwenye mazingira hatarishi au wakipata njia mbadala ya kuepuka maambukizi.

Kabla ya kuachiwa matumizi, mhusika atapatiwa vidonge 28 vya ziada ili viendelea kumpa kinga.

Baada ya kumaliza dozi hii anapaswa kurudi hospitalini kwa ajili ya uchunguzi ili kuhakiki hali ya maambikizi.

Share This Article