Muda wa kuongea, kukaa na kuota meno kwa watoto huwa haufanani.
Hii inatonakana na ukweli huwa ukiachia afya ya mtoto husika, sababu za kurithi, lishe, magonjwa na aina ya jamii anayotoka huchangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha mabadiliko haya.
Mtoto huanza kutembea akiwa na umri gani?
Kwa mujibu wa Kituo cha Udhibiti na Kinga ya Magonjwa (CDC), muda wa kawaida kwa mtoto kuanza kutembea ni wastani wa umri wa miezi 12-18
Hatua Zake
Mtoto hawezi kuanza kutembea moja kwa moja pasipo kupitia baadhi ya michakato yenye lengo la kumuimarisha kwaza kuelekea zoezi hili.
Kuna hatua nne ambazo mtoto hupitia kabla hajaanza kutembea.
- Miezi 6, huwa ni muda wa kukaa mwenyewe
- Miezi 6-9, muda wa kutambaa
- Miezi 9-12, muda wa kujivuta na kusimama kwenye vyombo na vifaa mbalimbali
- Miezi 12-18, kuanza kutembea
Hii siyo sheria inayomfanya kila mtoto apitie humo.
Baadhi yao huchelewa, na wengine huwahi sana kuliko muda huu wa kawaida.
Unaweza kumsaidia mwanao katika kumfanya awahi kutembea kwa kucheza naye, pamoja na kumshika mikono ili kumpa nguvu ya kutembea.
Hii itasaidia kuimarika kwa misuli yake na kumfanya atembee kwa urahisi zaidi.
Ushauri
Katika utafiti mmoja uliofanyika nchini Norway, asilimia 75 ya watoto huanza kutembea wakiwa na umri wa miezi 14.
Hii itoshe kukupa picha kuwa watoto huwa hawafanani, na haimaanishi kuwa yule aliyeanza kutembea chini ya miezi 14 au zaidi ya miezi 14 ana matatizo ya kiafya.
Mwanao ni tofauti, acha kumlinganisha na watoto wengine.
Lakini, ikiwa kuna baadhi ya mambo yanakupa wasiwasi fika hospitalini kwa uchunguzi na ushauri.