Ukuaji na tabia za watoto hutofautiana sana.
Kama ilivyo kwenye kuota meno au kukaa, muda wa kuanza kuzungumza huwa haufanani kwa watoto wote.
Hata hivyo, kuna miongozo kadhaa tunayoweza kuitumia katika kujadili muda unaodhaniwa kuwa wa kawaida, ambao hutokea kwa watoto wengi.
Tafiti
Kwa mujibu wa tafiti, watoto wengi huanza kuzungumza baadhi ya maneno wakiwa na umri wa miezi 7-12 na huanza kutengeneza sentensi za kueleweka wakiwa kwenye umri wa kati ya miaka 2-3.
Mwongozo wa taasisi ya National Institute of Health (NIH) hutoa mwelekeo huu kwenye hatua za kuanza kuzungumza kwa mtoto.
- Miezi 0-3, watoto husikia na kuelewa sauti za wazazi wao. Hutoa miguno au sauti kuashiria kuwa wanaelewa kinachoendelea
- Miezi 4-6, Macho yao huanza kufuata muelekeo wa sauti
- Miezi 7 hadi mwaka mmoja, wanaweza kuelewa maneno ya kawaida, kuzungumza kwa ishara ya mikono pamoja na kutaja maneno ya kawaida kama ba-ba, ma-ma na da-da. Wanaweza pia kuelewa majina yao wakiitwa
Maendeleo makubwa kwenye kuzungumza huanza kuonekana baada ya mwaka mmoja.
Watoto huanza kuelewa mambo mbalimbali wanayoelekezwa na wazazi wao.
Wanapofikisha miaka miwili huwa na uwezo wa kuzungumza sentensi fupi yenye walau idadi ya maneno mawili hadi manne.
Mfano mama kwaheri, maziwa yangu, mama kojoa na huanza pia kujifunza maneno mapya.
Sababu za Kuchelewa
Baadhi ya watoto huchelewa kuanza kuzungumza.
Kama mzazi, haupaswi kuogopa kwa kuwa mtoto wa mwingine kaanza kuzungumza mapema kuliko mwanao.
Tunaendelea kusisitiza kuwa tabia na ukuaji wa watoto hutofautiana sana.
Baadhi ya sababu zinazoweza kufanya mtoto achelewe kuzungumza ni uwepo wa matatizo ya kusikia, kuzaliwa na degedege, matatizo ya kiakili, usonji, mapungufu kwenye mfumo wa koromeo na kinywa pamoja na kuzaliwa kwenye jamii zinazozungumza lugha nyingi. (1,2)
Ushauri
Ikiwa mzazi unapata wasiwasi kuhusu sababu zinazofanya mwanao akawie kuanza kuzungumza ni vyema ukaenda hospitalini kwa uchunguzi na ushauri.
Kumbuka pia, watoto hawafanani.