Njia na Dawa za Kufanya Upate Watoto Mapacha

4 Min Read

Miaka ya hivi karibuni, idadi ya watoto mapacha wanaozaliwa duniani imeongezeka sana tofauti na zamani.

Takwimu hizi zimeongezeka zaidi kuanzia miaka ya 1980, kutoka uzao wa mapacha 9 katika kila wanawake 1000 hadi kufikia uzao wa mapacha 12 katika kila wanawake 1000 wanaojifungua.

Katika ongezeko hili, mapacha wasiofanana ndiyo wamekuwa wengi zaidi ikilinganishwa na mapacha wa kufanana.

Kubadilika kwa mitindo ya maisha pamoja na uwepo wa mbinu kadhaa za kisayansi zinazoongeza uwezekano wa kupata ujauzito wa watoto mapacha ndizo sababu kuu mbili zinazo husishwa na hali hii. (1,2,3)

Utapataje Mapacha?

Hili ni swali maarufu sana mitaani.

Hakuna njia inayoweza kukupa uhakika wa kupata ujauzito wa watoto mapacha kama inavyodaiwa na watu wengi.

Njia zote zilizopo huongeza tu uwezekano wa kufanikisha jambo hili, lakini hazitoi uhakika kwa asilimia 100 katika kukupa majibu sahihi.

1. Dawa

Baadhi ya dawa kama clomiphene citrate maarufu kama Clomid au Serophene hutumika kutatua tatizo la ugumba kwa wanawake.

Huongeza uzalishwaji wa vichocheo vinavyowezesha ukuaji na upevushwaji wa mayai.

Katika mzingira fulani, dawa hii hutumiwa na wanawake wanaotaka kupata ujauzito wa watoto mapacha. (4,5)

Kama nilivyosema, dawa hizi hazitoi uhakika katika kufanikisha kazi hii, pia inapaswa kutumiwa kwa kuzingatia dozi na masharti sahihi yanayotolewa na mtaalamu wa afya.

2. Mtindo wa Sex

Kuna mitindo ya kufanya mapenzi inayozungumzwa sana, ambayo hutajwa kuwa na uwezo wa kusababisha ujauzito wa watoto mapacha.

Hii siyo kweli, huwezi kufanikisha jambo hili kwa kufanya mapenzi kwa mtindo fulani.

3. Vyakula

Hakuna vyakula au virutubisho vinavyoweza kufanikisha kutokea kwa ujauzito wa watoto mapacha.

Kuwa makini unapotoa pesa yako mitaani.

4. Historia

Kila mwanamke anao uwezo wa kupata ujauzito wa watoto mapacha. Pia, historia ya ukoo huchukua nafasi kubwa sana katika kuamua hali hii.

Watu wanaotoka kwenye koo zilizo na historia hii huwa na nafasi kubwa zaidi ya kupata watoto mapacha kuliko wale wasio na historia ya uwepo wake. (6,7)

5. Asili ya Afrika

Wanawake wenye asili ya Afrika huwa na nafasi kubwa zaidi ya kupata ujauzito wa watoto mapacha kuliko wanawake wa asili nyingine.

Mfano, jamii za Igbo-Ora zinazopatikana Afrika Magharibi zimebeba rekodi ya dunia, zikiwa na uwiano wa uwezo wa wanawake kupata ujauzito wa watoto mapacha mara 4 zaidi kuliko jamii zingine zote duniani. (8,9)

6. IVF

Kuna njia moja ya gharama kubwa sana, inaitwa In Vitro Fertilization (IVF).

Ni urutubishwaji wa mayai ya mwanamke nje ya mwili wake, kwenye maabara.

Baada ya urutubishwaji huu, mayai ya mwanamke hurudishwa kwenye mji wa uzazi ili utunzwaji wa ujauzito uendelee.

Njia hii huchukua walau wastani wa wiki 3 kuikamilisha.

Hutumika kusaidia wanawake wenye changamoto za uzazi, kuzuia urithishwaji wa vinasaba visivyofaa kwa mtoto kutoka kwa wazazi na baadhi huitumia katika kujaribu kupata watoto mapacha.

Njia hii pia haitoi uhakika wa kukupa ujauzito wa watoto mapacha pamoja na ukweli kuwa ni ghali sana kuifanikisha.

Ushauri

Baadhi ya maneno huwa ni magumu sana kuyakiri kwenye lugha za kisayansi.

Mojawapo ya maneno hayo ni “bahati”.

Sitasita kulitaja neno hilo kwenye makala hii kwa kuwa hakuna namna nyingine ya kuonesha usahihi wa tendo hili.

Bahati huchukua nafasi kubwa sana kwenye kupata aina hii ya ujauzito kuliko uwekezaji wa juhudi binafsi.

Nakukumbusha kuwa hakuna njia yenye uhakika wa asilimia 100 kukupa ujauzito wa watoto mapacha.

Share This Article