Kujadili mada kama hizi huhitaji kuweka pembeni hisia na misukumo yote ya kiimani ili kuweza kuelewa vizuri.
Tendo la ndoa wakati wa hedhi hubeba faida na madhara kadhaa, pia linapaswa kufanywa kwa tahadhari kubwa.
Ufanye au usifanye? Ni uamuzi wako mwenyewe.
Takwimu
Tafiti kadhaa zinathibitisha kuwa jambo hili hufanyika kwa baadhi ya watu, na wengine huwa hawapo tayari kufanya kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kidini, usafi na uoga. (1)
Kufanya tendo la ndoa wakati wa hedhi huwa na faida zifuatazo;
1. Hedhi Fupi
Tendo la ndoa wakati wa hedhi hufupisha muda wa hedhi.
Mwanamke anapofika kileleni husisimua kuta za mji wa uzazi ambazo huongeza kiasi cha kujikaza na kuvutika.
Hii hurahisisha utolewaji wa haraka wa mazao yote ya hedhi.
2. Tumbo
Tendo la ndoa huufanya mwili uzalishe kemikali za furaha, maarufu kama endorphins.
Aidha, kusisimka kwa kuta za mji wa uzazi baada ya kufika kileleni huhusishwa na kupunguza ukubwa wa maumivu ya hedhi. (2,3,4)
3. Maumivu ya Kichwa
Ukiondoa changamoto ya maumivu ya tumbo, baadhi ya wanawake hukabiliwa pia na maumivu makali ya kichwa.
Baadhi ya tafiti zinadai kuwa tendo la ndoa husaidia kupunguza maumivu haya ya kichwa. (5)
Faida nyingine za tendo hili ni kupunguza stress na kuboresha usingizi. (6,7)
Madhara
Kama ilivyo kwa wakati mwingine wa kawaida kabisa, tendo la ndoa ni chanzo namba moja cha usambazwaji wa magonjwa ya zinaa.
Vimelea vya magonjwa hayo hukaa kwenye damu pamoja na majimaji ya mwili, hivyo ni rahisi sana kuvipata wakati wa hedhi.
Baadhi ya magonjwa hayo ni kisonono, kaswende, klamidia na VVU. (8,9)
Aidha, magonjwa ya fangasi na bakteria yanaweza pia kuambukizwa kirahisi wakati huu.
Usafi ni changamoto nyingine kubwa ya kushiriki tendo la ndoa wakati wa hedhi.
Damu inaweza kuchafua kitanda au hata wahusika wenyewe.
Hii inaweza kuwa changamoto kubwa hasa kwa wanawake wenye hedhi nzito.
Tahadhari
Ukiondoa kupata magonjwa ya zinaa, unaweza pia kupata ujauzito kwa kushiriki tendo la ndoa wakati wa hedhi.
Hii inaweza kutokea hasa kwa wanawake wenye mizunguko mifupi yenye wastani wa siku 21-24 kwa kuwa utoaji wa mayai yaliyopevuka hutokea ndani ya siku za hedhi. (10)
Hivyo mwanamke mwenye mizunguko hiyo anapaswa kuwa makini ikiwa ataamua kushiriki tendo la ndoa wakati wa hedhi.
Ushauri
Ni matakwa yako mwenyewe kuamua kama utafanya au la.
Ikiwa utaamua kufanya, unapaswa kuzingatia mambo yafuatayo;
- Badili tampon au taulo zako za kike mara kwa mara ili kuzuia bakteria wasizaliane kwa wingi
- Tumieni kinga
- Oga kwanza kabla ya kushiriki tendo la ndoa
- Oga tena baada ya tendo la ndoa kabla haujavaa tampon au taulo yako
- Mnaweza kuamua kushiriki tendo hili bafuni, ili kama kuna jambo lolote litatokea iwe rahisi kujisafisha
Muhtasari
Siyo jambo la ajabu kushiriki tendo la ndoa wakati wa hedhi. Pamoja na ukweli huu, baadhi ya imani za kidini hupinga jambo hili.
Sisi hatupo huko, tunazungumzia upande wa sayansi wa jambo hili. Uamuzi ni wako.