Mbinu 10 za Kupunguza Tumbo Kubwa

5 Min Read

Miaka ya zamani, tumbo kubwa lilihusishwa na utajiri, au uwepo wa mafanikio kwenye maisha.

Mambo yamebadilika. Tumbo kubwa huondoa urembo kwa wanawake, au utanashati kwa wanaume. Leo, tumbo kubwa ni mzigo.

Kwa kuwa baadhi ya aina za mafuta zinazojikusanya tumboni huwa siyo nzuri, tumbo la aina hii linaweza kuwa chanzo cha magonjwa sugu.

Ni hatari kwa afya. (1,2)

Pengine wewe ndiye unaudhika na ukubwa wa tumbo lako, au unataka kumsaidia mtu apunguze tumbo lake.

Twende pamoja.

1. Chai ya Rangi

Chai ya rangi huwa na kemikali muhimu kwa kuunguza mafuta ya tumbo, huitwa epigallocatechin gallate.

Kemikali hizi kwa miaka mingi zimekuwa zinatumika katika kutengeneza vyakula na vinywaji kwa ajili ya watu wanaotaka kupunguza tumbo. (3,4,5)

Ufanisi wake huongezeka zaidi kwa watu wanaofanya mazoezi, pia ikichanganywa na limao au ndimu.

2. Apple Cider Vinegar

Umewahi kwenda supermarket ukakutana na chupa imeandikwa kwa majina hayo?

Hiyo chupa ni chaguo sahihi kwa watu wenye tumbo kubwa.

Huwa na kemikali za acetic acid ambazo tafiti nyingi zinathibitisha uwezo wake wa kuunguza mafuta ya tumbo. (6,7,8)

Kiasi cha vijiko viwili kwa siku vilivyo changanywa kwenye maji vinatosha kabisa kuleta majibu chanya.

3. Usingizi

Asikwambie mtu, hapa hatusemi bia ni tamu kwenye kupunguza ukubwa wa tumbo pamoja na uzito mkubwa wa ujumla. Usingizi ndiyo kitu kitamu.

Ukiondoa faida zake kwenye kuboresha afya ya binadamu kwa ujumla wake, usingizi hutoa mchango mkubwa katika kutunza uzito wa mwili pamoja na kudhibiti ukubwa wa tumbo. 

Unapaswa sasa kuongeza muda wa kulala. Ukiniuliza masaa mangapi yanafaa?  (9,10)

Nitakujibu kuwa masaa yoyote ambayo baada ya kuamka hautajisikia kuwa mwili wako bado unakudai usingizi.

4. Sukari

Sukari hasa ya viwandani haijawahi kuwa rafiki mzuri wa afya ya binadamu.

Sukari ni chanzo kikubwa cha magonjwa sugu yanayoua mamilioni ya watu kila mwaka duniani. Tafiti nyingi zinahusisha pia matumizi ya sukari na kuongezeka kwa mafuta yanayojikusanya tumboni. (11,12)

Ni vizuri kuepuka matumizi makubwa ya aina hii ya sukari

5. Pombe

Sina mamlaka ya kukukataza usinywe pombe, na sitaki kusema kuwa pombe ni mbaya sana kwa afya.

Nitatumia maneno ya upole, kunywa pombe lakini usinywe nyingi sana.

Tafiti zinasema kuwa watu wanaotumia pombe nyingi huwa na nafasi kubwa ya kupatwa na tatizo la kuongezeka kwa mafuta, na kusababisha tumbo kubwa. (13)

Sikukatazi tena kunywa pombe, lakini nakushauri unywe kidogo.

6. Virutubisho

Uwanda wa kushughulikia changamoto za kiafya za binadamu kupitia tibalishe umekuwa mkubwa sana siku hizi.

Watu wengi huwaza, ni kweli vinafanya kazi? Jibu langu ni jepesi tu.

Baadhi hufanya kazi na baadhi zipo sokoni kwa ajili ya biashara.

Mojawapo ya virutubisho vilivyo thibitishwa kuwa na uwezo wa kuunguza mafuta ya tumbo na kuondoa tatizo hili ni garcinia cambogia, omega 3, uyoga mwekundu, calcium na vitamini D, mdalasini, chai ya rangi na kahawa.

7. Protini

Protini huhitajika sana katika kudhibiti uzito kwa kuwa huufanya mwili upunguze uzalishaji wa vichocheo vya njaa pamoja na hamu ya kula.

Huusaidia pia mwili katika kuongeza matumizi ya nishati. (14,15)

Aidha, watu wanaotumia kiasi kingi cha protini huhusishwa na kuwa na miili yenye mafuta machache ya tumbo pamoja na viribatumbo.

8. Mazoezi

Ni vigumu kuyakwepa mazoezi katika kuimarisha afya pamoja na kuboresha muonekano wa mwili.

Mazoezi huwa ni njia sahihi sana ya kupunguza uzito wa mwili, hasa kwa watu wenye mafuta mengi na vitambi. (16)

Mazoezi ya kukimbia, kuruka kamba pamoja na aina zingine za mazoezi zisizo husisha ubebaji wa vyuma hushauriwa kwa watu hawa.

9. Stress

Hautapunguza mafuta haya kama maisha yako kila siku yametawaliwa na stress. Unajua kwanini?

Stress huuamuru mwili uzalishe kiasi kikubwa cha vichocheo vya cortisol.

Vichocheo hivi huchochea tabia ya kula pamoja na kuufanya mwili utunze mafuta mengi kwenye sehemu ya chini ya tumbo.

Najua maisha ni magumu, hauna hela na mapenzi yanakusumbua.

Lakini, nakusihi upunguze stress.

10. Mlo

Punguza matumizi makubwa ya vyakula vya viwandani.

Ongeza ulaji wa mboga za majani na matunda. (17)

Vyakula hivi huusaidia mwili kwenye kutumia nishati zake pamoja na kusisimua vimeng’enya vya mwili hasa vile vya insulin ambavyo hutumiwa na mwili katika kudhibiti sukari.

Muhtasari

Najua tumbo hili linakutesa sana.

Naelewa pia umetumia njia mbalimbali lakini haujafanikiwa.

Chagua njia kadhaa miongoni mwa hizi. Baada ya miezi 3 rudi unipe majibu.

Share This Article