Kuna taarifa nyingi sana kwenye vitabu pamoja na internet zinazoeleza namna gani unaweza kupata ujauzito uliobeba changuo la jinsia ya mtoto wako.
Changamoto kubwa ya njia hizi ni matumizi ya gharama kubwa kuzifanikisha, kutokuwa na uhakika mkubwa wa kutoa majibu chanya, ukosefu wa taarifa sahihi za kisayansi zinazothibitisha ufanisi wake pamoja na baadhi yake kuwa na athari fulani kwa afya ya mwanamke. (1)
Njia ninayotaka kuielezea hapa ni ndefu kidogo.
Unaweza kuchukua kalamu na karatasi ili utunze kumbukumbu zako. Siyo vibaya pia ukijaza maji kwenye glasi yako. Twende sasa.
Njia ya Shettles
Hii ndiyo njia rahisi zaidi na inayotoa uhakika mkubwa kuliko njia zingine, pia haina gharama wala athari zozote kwa afya ya mama.
Ni salama kwa asilimia 100 hivyo binafsi ninapenda kushauri kila anayesoma makala hii ajaribu kuifuata.
Njia hii ilifanyiwa utafiti mkubwa sana miaka ya 1960 na Dr. Landrum B. Shettles. (2,3)
Nadharia hii imejikita katika msingi wa tofauti ya kimaumbile, muda wa kuishi pamoja na uthabiti wa afya ya mbegu za kiume aina X ambazo huamua jinsia ya kike pamoja na mbegu za kiume aina Y ambazo ndizo huamua jinsia ya kiume.
Mbegu za Kiume
Mwanamme huzalisha mbegu za kiume zilizobeba aina mbili tofauti za taarifa. Mbegu za kiume huwa na taarifa X au taarifa Y.
Taarifa X ndizo huamua jinsia ya kike huku taarifa Y zikiamua jinsia ya kiume.
Ikitokea mbegu ya kiume iliyobeba taarifa X ikakutana na yai la mwanamke ambalo pia huwa na taarifa X, ujauzito wa jinsia ya kike upatikana, yaani XX.
Ikiwa mbegu ya kiume iliyobeba taarifa Y ikakutana na yai la mwanamke ambalo mara zote huwa na taarifa X, ujauzito wa jinsia ya kiume upatikana, yaani XY.
Kwa maana hiyo, mwanamme ndiye mwamuzi wa jinsia za watoto kwenye familia kwa kuwa mbegu zake huwa na taarifa zilizobeba jinsia zote yaani X na Y tofauti na wanawake ambao mayai yao yote huwa na taarifa za jinsia moja tu ambayo ni X. (4,5,6)
Hata hivyo, kuna tafiti nyingi pia zimefanyika tangu nadharia hii igunduliwe, nyingi zikitoa maboresho kadhaa kwenye kuongeza ufanisi wa njia hii.
Hivyo, tutaunganisha maelezo ya tafiti mpya kama sehemu ya kuboresha na kuweka usahihi wa mada hii (7,8)
Mbegu Y
Aina hii ya mbegu ambayo hubeba chembeuzi (chromosome/kromosomu) Y huwa na sifa za kuamua jinsia ya kiume, zina kasi kubwa ya kuogelea, umbo lake ni dogo, ni dhaifu na hufa mapema pia huathirika zaidi na joto, sigara, sumu na aina mbalimbali za madawa.
Mbegu X
Aina hii ya mbegu ambayo hubeba chembeuzi (chromosome/kromosomu) X huwa na sifa za kuamua jinsia ya kike, zina kasi ndogo ya kuogelea, umbo lake ni kubwa, ni imara, zina nguvu na huishi kwa muda mrefu pia haziathiriwi sana na joto, sigara, sumu na aina mbalimbali za madawa.
Kwa kuzingatia sifa na tabia hizi zilizopo miongoni mwa aina mbili tofauti za mbegu za kiume ambazo tumeziona, nadharia hii ya Dr. Shettles inaamini katika kushiriki tendo la ndoa kwenye muda sahihi kwa kufuata mzunguko wa hedhi ya mwanamke husika.
Kupata Jinsia ya Kiume
Ili upate mtoto mwenye jinsia ya kiume, tendo la ndoa lifanyike karibu kabisa na siku ya ovulation, au siku husika ya ovulation.
Mwanamme anashauriwa pia kutokushiriki kabisa tendo la ndoa na mwanamke wake tangu kuisha kwa hedhi hadi siku yenyewe ya ovulation. Hii itatoa nafasi kwa mwanamme husika kuzalisha mbegu nyingi za kutosha. Kwa kuwa jambo hili ni gumu kuvumilika, mwanamme anaweza kujizuia kushiriki tendo la ndoa walau kwa muda wa siku 4 kuamkia siku ya ovulation. Tendo la ndoa linaweza kuendelea kufanyika baada ya siku ya ovulation bila tatizo lolote.
Joto huathiri afya ya mbegu za kiume hasa zile zinazotunga ujauzito wa jinsia ya kiume, yaani mbegu za kiume aina Y. Mwanamme anashauriwa kuepuka mazingira yanayoongeza joto la sehemu zake za siri.
Aidha, ni vizuri kama mwanamke atafikishwa kileleni wakati wa tendo la ndoa.
Mbegu za kiume aina Y zinazohitajika kwenye utungwaji wa ujauzito wa jinsia ya kiume huwa dhaifu, pia hufa mapema zaidi.
Kutokana na ugumu wa mazingira yaliyopo kwenye uke, mbegu hizi hushindwa kupambana kikamilifu.
Mwanamke anapofika kileleni hutoa majimaji yenye kiasi kingi ya alkali ambayo hupunguza tindikali inayopatikana kwenye uke, hivyo kurahisisha zaidi utungwaji wa ujauzito uliobeba jinsia ya kiume.
Pia, Mtindo wa kushiriki tendo la ndoa ni muhimu sana.
Mwanamme anashauriwa kutumia mbinu zitakazofanya uume wake uzame ndani ya uke kwa kiasi kikubwa.
Kitendo hiki kitasababisha mbegu za kiume zimwagwe karibu zaidi na mlango wa kizazi hivyo zitakuwa na umbali mdogo tu wa kusafiri kuelekea kwenye mirija ya uzazi ili kutunga ujauzito. Mfano, doggy-style.
Kupata Jinsia ya Kike
Ili upate mtoto mwenye jinsia ya kike, tendo la ndoa lifanyike siku 2-3 kabla ya ovulation, kisha lisifanyike tena hadi siku 2 baadae, wakati ambao muda wa ovulation utakuwa tayari umeshapita.
Mwanamme anashauriwa kushiriki tendo la ndoa mara kwa mara baada tu ya kukoma kwa hedhi ya mwanamke hadi siku 2-3 kabla ya siku ya ovulation.
Siku moja kabla ya ovulation, siku yenyewe ya ovulation hadi siku 2 baada ya ovulation, mwanamke na mwanamme hawashauriwi kushiriki tendo la ndoa. Ikiwa wataamua kushiriki, shahawa zisimwagwe ndani ya uke.
Aidha, ni vizuri kama mwanamke hatafikishwa kileleni wakati wa tendo la ndoa.
Mbegu za kiume aina X zinazohitajika kwenye utungwaji wa ujauzito wa jinsia ya kike huwa imara sana, pia huishi muda mrefu zaidi.
Kutokana na ugumu wa mazingira yaliyopo kwenye uke, mbegu hizi huwa na uwezo mkubwa wa kupambana kikamilifu hivyo hazihitaji usaidizi wa alkali inayozaliswa pindi mwanamke afikapo kileleni.
Pia, mtindo wa kushiriki tendo la ndoa ni muhimu sana.
Mwanamme anashauriwa kutumia mbinu zitakazofanya uume wake usizame ndani ya uke kwa kiasi kikubwa.
Kitendo hiki kitasababisha mbegu za kiume zimwagwe mbali kidogo na mlango wa kizazi hivyo zitakuwa na umbali mrefu zaidi wa kusafiri kuelekea kwenye mirija ya uzazi ili kutunga ujauzito. Mfano, kifo cha mende.
Mafanikio
Ikiwa mambo haya yote yatazingatiwa na kufuatwa, uhakika wa kupata ujauzito wenye jinsia ya kiume huwa ni asilimia 80-85 wakati jinsia ya kike ikiwa ni asilimia 75-80.
Faida
Uzuri wa njia ya hii ni kuwa haihitaji gharama yoyote, inafanyika kwa usiri ndani ya nyumba yako bila kushirikisha mtu mwingine yeyote, haihitaji matumizi yoyote ya usaidizi wa njia mbadala hasa madawa hivyo ni salama kwa asilimia 100.
Changamoto
Lazima mwanamke awe na uelewa mkubwa wa mzunguko wake wa hedhi, hasa katika kujua siku sahihi ya ovulation.
Njia hii inaweza kuwa ngumu kwa watu wasiojua mzunguko wap, pia wale wenye mzunguko unaobadilika kila mara.
Aidha, haitoi uhakika kwa asilimia 100 kukupa jinsia unayotaka, inaweza kuleta majuto, kupunguza mapenzi kwa mtoto pamoja na changamoto zingine za kisaikolojia kwa wazazi ikiwa hawatafanikiwa kupata mtoto mwenye jinsia waliyoikusudia.
Pia, baadhi ya imani na madhehebu mbalimbali kidini hayaafikiani na utaratibu huu unaotajwa kuwa na mlengo hasi wa kuingilia kazi ya Mungu.
Muhtasari
Njia hii huhitaji uelewa mkubwa wa matumizi ya kalenda inayoongoza mzunguko wa hedhi ya mwanamke. (9,10)
Hivyo, kwa wanawake wasio na uelewa mkubwa wa kufuata kalenda wanapaswa kujifunza kwanza ili iwe rahisi kwao.
Ni muhumu kusisitiza tena kuwa njia hii haitoi uhakika wa asilimia 100 kwenye kukupa mtoto wa jinsia yako pendwa.