Komamanga: Virutubisho na Faida kwa Afya

7 Min Read

Komamanga ni mojawapo ya matunda yaliyodumu duniani kwa karne nyingi sana.

Tunda hili lenye historia na stori nyingi za kustajabisha kwa lugha ya kisayansi huitwa Punica granatum.

Tunda hili limebeba sifa za kipekee sana katika kuboresha afya ya binadamu.

Virutubisho

Huwa na muunganiko mkubwa wa kemikali za phenolics, flavonoids, ellagitannins, na proanthocyanidin, pamoja na madini ya potassium, calcium, phosphorus, magnesium na sodium.

Huwa pia na viondoa sumu, aina mbalimbali za sukari pamoja na kiasi cha kutosha cha aina mbalimbali za asidi.

Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), maji, nishati, protini, zinc, vitamini C, folate, copper na selenium hupatikana pia kwenye tunda hili.

1. Tezi Dume

Tafiti nyingi zilizofanyika nje na ndani ya mwili wa binadamu zinaonesha uwezo wa komamanga katika kudhibiti ukuaji, usambaaji, kujigawa pamoja na kushambulia kwa saratani za tezi dume.

Tafiti zingine zinadai kuwa kemikali zinazopatikana kwenye tunda hili huwa na uwezo wa kutengeneza taarifa zinazofanya seli zinazosababisha saratani zijiue zenyewe. (1,2)

Tunda hili pia hutibu uvimbe wa tezi dume, pamoja na kuzuia usitokee.

2. Wanaume

Kuna vipengele vingi sana vinavyohusisha nguvu za kiume, lakini nguvu ya tunda hili imejikita katika kuongeza ufanisi wa kushiriki tendo la ndoa kwa kupanua mishipa ya damu.

Aidha, huzilinda kemikali za nitric oxide (NO) ambazo ndizo huhusika katika kupanua mishipa ya damu, huongeza msukumo wa damu kwenye uume pamoja na kulinda neva na tishu za uume zisipatwe na majeraha.

Kwa namna ya kipekee kabisa, tunda hili huongezwa uzalishwaji wa vichocheo vya kiume, maarufu zaidi kama testosterone ambayo huhusika katika kuratibu kazi zote zinazohusu tabia za kiume. (3,4)

Unasubiri nini kutumia tunda hili?

3. Mfumo wa Mkojo

Husaidia kuzuia, pamoja na kupunguza utengenezwaji wa mawe kwenye figo.

Hudhibiti pia ongezeko la oxalates, calcium na phosphate kwenye damu. (5)

Hivi ni viunganishi muhimu katika kutengeneza mawe kwenye figo.

4. Uvimbe

Mwili hujilinda kwa kutengeneza aina mbalimbali za uvimbe baada ya kushambuliwa na vimelea vya magonjwa.

Uvimbe wa muda mfupi hauna athari kwa afya, lakini hugeuka kuwa mwiba baada ya kubadilika kuwa uvimbe sugu.

Ni chanzo cha magonjwa ya moyo, kisukari, magonjwa ya akili na saratani. (6,7)

Komamanga hudhibiti miamsho inayosababisha kutengenezwa kwa uvimbe mwilini, pia hupunguza athari za uvimbe.

5. Mfumo wa Damu na Moyo

Hulinda moyo na mishipa ya damu.

Hufanya hivyo kwa kudhibiti ongezeko la shinikizo la damu pamoja na kuunguza mafuta mabaya yanayojaa kwenye mishipa ya damu. (8)

Magonjwa ya mfumo wa damu na moyo huua watu wengi duniani, chukua tahadhari sasa.

6. Vimelea

Huwa na uwezo wa kupambana na vimelea vya magonjwa hasa bakteria na fangasi.

Vimelea hivi huwa ni chanzo cha maambukizi ya magonjwa mbalimbali yanayomhusu binadamu mfano UTI, kisonono, kaswende na magonjwa mengine ya mfumo wa uzazi na upumuaji.

Katika utafiti mmoja, komamanga lilithibitika kuwa na uwezo wa kupambana na bakteria wanaosababisha magonjwa ya kinywa. (9)

Tunda hili linasifiwa kwa kuwa na uwezo wa kupambana na vimelea sugu ambavyo dawa za kawaida hushindwa kuvidhibiti.

7. Mfumo wa Chakula

Mfumo wa chakula cha binadamu husaidiwa na bakteria wazuri katika kufanya kazi zake kikamilifu.

Kukosekana au kudhoofika kwa afya ya bakteria hawa hukaribisha magonjwa mbalimbali hasa kuhara, bawasiri, choo kigumu, vidonda vya tumbo pamoja na saratani mbalimbali.

Komamanga hubeba kiasi kikubwa cha nyuzilishe pamoja na ellagic acid.

Vyote hivi vimethibitishwa na tafiti kuwa na uwezo wa kuboresha mfumo wa chakula, kulinda bakteria wazuri, kuzuia magonjwa pamoja na kutibu baadhi ya changamoto za mfumo wa chakula mfano choo kigumu na bawasiri.

8. Sumu

Seli ndiyo kitovu cha uhai wa binadamu.

Uwepo wa aina mbalimbali za sumu mwilini ambazo huingia kwa kufahamu, au kutokufahamu huathiri afya ya seli za mwili.

Nyingi huanza kufa, huzeeka kabla ya wakati na nyingine huanza kuonesha tabia zisizo za kawaida kwa kusababisha magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la juu la damu, saratani na kiharusi.

Komamanga ni chanzo kizuri cha viua sumu.

Baadhi ya viua sumu hivyo vinavyofaa kwa afya ni punicalagins, anthocyanins na hydrolysable tannins. (10)

Ni tunda bora sana kwa afya yako.

9. Kisukari

Kampaundi za punicalagin, ellagic, gallic, oleanolic, ursolic, na uallic acids zimethibitishwa na tafiti kuwa na uwezo wa kutibu aina ya pili ya ugonjwa kisukari, pamoja na kupunguza changamoto zake. (11,12)

Pamoja na mambo mengine, huongeza msisimko wa vimeng’enya vya insulin katika kudhibiti ongezeko la kiwango cha sukari mwilini.

10. Ubongo

Huongeza uwezo wa ubongo kwenye kutunza kumbukumbu.

Ni tunda zuri kwa watoto, wanawake wajawazito pamoja na wazee ambao kwa kiasi kikubwa hukumbwa na tatizo la kupoteza kumbukumbu.

Kampaundi ellagitannins huulinda ubongo pamoja na kuepusha magonjwa ya akili.

11. Mazoezi na Kazi

Tunda lingine linalofaa kwa watu wanaofanya kazi ngumu na mazoezi ukiondoa tikiti maji ni komamanga.

Hurejesha uhai wa misuli pamoja na kupunguza uchovu. (13,14)

Mfano, utafiti mmoja unaonesha kuwa ulaji wa gramu 1 ya virutubisho vya komamanga dakika 30 kabla ya kuongeza uwezo wa kukimbia na kupunguza adha ya kuchoka upesi kwa asilimia 12. (15)

12. Damu

Tunda hili hutumika kutibu na kuounguza ukubwa wa changamoto zinazo husisha upotevu wa damu nyingi mwilini. (16,17)

Baadhi ya changamoto hizo ni kutokwa na hedhi nzito, kuvuja kwa damu kwenye meno pamoja na kuraha choo chenye damu.

Muhtasari

Komamanga ni tunda salama linaloweza kutumiwa na kila mtu.

Linaweza kutumika kwa kula kama tunda la kawaida, au kwa njia ya juisi.

Tumia mara kwa mara ili litoe majibu yanayo tarajiwa.

Share This Article