Miongoni mwa mambo yanayosumbua wazazi ni kuona meno mazuri yaliyokuwa yameanza kupendezesha kinywa cha mtoto yanaanza kuoza.
Ni kitendo ambacho huacha maswali mengi yakihusisha sababu zake.
Chanzo
Vyanzo vikuu vya kuharibika au kuoza kwa meno ya watoto ni sukari na bakteria.
Bakteria wa kinywani hubadili sukari kuwa asidi ambayo ndiyo huhusika moja kwa moja katika kuharibu meno.
Watoto hupata sukari hizi kupitia mlo wa kawaida wenye kiwango kikubwa cha wanga, soda, maziwa ya unga au ya mama, juisi mbalimbali pamoja na vitafunwa vyenye sukari za nyongeza.
Meno Yapi Huathirika?
Kuharibika kwa meno kunaweza kutokea kwenye meno yoyote yale.
Kwa kiasi kikubwa, huonekana kwenye meno ya mbele sehemu ya juu kisha huanza kusambaa sehemu zingine.
Vihatarishi
Kila mtoto huwa na bakteria kinywani mwake, lakini wale wenye sifa hizi huwa hatarini zaidi;
- Kiwango kikubwa cha bakteria wanaosababisha kuoza kwa meno
- Kiwango kidogo cha mate kinywani
- Wasio safishwa vinywa vyao
- Wanaokula na kunywa vitu vyenye wanga na sukari nyingi
- Wanaokunywa maji yenye kiasi kidogo cha fluoride, au wasiopata kabisa fluoride.
Watoto wanaosinzia na chupa za maziwa zikiwa mdomoni, au wale wanaobembelezwa kwa kupatiwa vitu vyenye sukari huwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kupata changamoto hii kuliko wengine.
Madhara
Meno huongeza urembo na utanashati wa watoto.
Kuharibika kwa meno kwenye umri huu mdogo huwa ni pigo kubwa.
Changamoto hii inaweza kuharibu mpangilio wa kudumu wa meno, maumivu, kufanya meno yawe na rangi ya brown pamoja na kusababisha maambukizi ya kinywa ikiwa tiba sahihi haitatolewa. (1,2)
Aidha, inaweza kusababisha mtoto awe na wakati mgumu katika kuzungumza pamoja na kutafuna vyakula.
Uzuiaji
Tumeona sababu zinazofanya kutokea kwa tatizo hili.
Ili kuzuia lisitokee, mzazi unapaswa kutomruhusu mtoto alale na chupa ya maziwa au juisi, simpe vyakula vyenye sukari za nyongeza hasa soda, pipi na keki, mtoto chini ya mwaka mmoja usimpatie juisi, iwe ya matunda au ya viwandani.
Pia, safisha meno yake asubuhi na jioni kabla hajalala kwa kitambaa na maji safi ikiwa bado ana tabia ya kumeza kila kitu, kama unaweza kumwambia ateme kitu kisha akatii, safisha meno yake ya mswaki mdogo wenye dawa ya meno ya fluoride. Hakikisha anatema mapovu hayo, kisha msafishe kwa maji safi pamoja na kunguza muda wa matumizi ya nyonyo bandia.
Acha tabia ya kutumia kijiko kimoja na mtoto pamoja na kutafuna kwanza vyakula ndipo unampatia yeye ili avitumie.
Kitendo hicho kinaweza kusafiririsha bakteria wabaya kwa mtoto hivyo kufanya meno yake yaharibike.
Tiba
Hutegemeana na ukubwa wa tatizo kwa wakati huo.
Ikiwa tatizo limekuwa kubwa sana, meno haya huondolewa na sehemu husika kuzibwa ili kuondoa athari zilizo sababishwa na uwepo wa tatizo hilo.
Muhtasari
Ni muhimu kufuatilia tabia za mtoto hasa kwenye vitu anavyokula na kunywa.
Vitu hivi kwa kiasi kikubwa huchangia sana kutokea kwa tatizo hili.
Watoto wasafishwe pia meno yao pasipo kujali yapo mangapi. Hata jino moja linapaswa kusafishwa.