Mtoto Kuzaliwa na Meno

2 Min Read

Unaweza usiamini, lakini baadhi ya watoto huzaliwa wakiwa na kati ya jino moja hadi meno matatu.

Hutokea kwa wastani wa mtoto mmoja katika kila kundi la watoto 2000 hadi 3000 wanaozaliwa. (1)

Meno haya mara nyingi huwa ni madogo kiumbo, malegevu na huwa na rangi ya njano.

Sababu

Asilimia 15 ya watoto wanaozaliwa na meno hutoka kwenye koo au familia ambao baadhi ya watu wa pale waliwahi kuzaliwa wakiwa na hali hii. (2)

Sababu za kutokea kwake huwa hazipo wazi sana.

Baadhi ya changamoto za kijenetiki kama sotos syndrome ambayo huwafanya watoto wapitie ukuaji usio wa kawaida huhusishwa na kutokea kwa hali hii.

Ugunduzi

Hugunduliwa kwa kutazama.

Daktari anaweza kufanya pia vipimo vya x rays ili kuona kama jino hili limetengenezwa kikamilifu.

Tiba

Mtoto huyu anapaswa kupelekwa hospitalini kwa uchunguzi wa kina.

Ikiwa daktari atajiridhisha kuwa meno hayo yapo imara na mizizi yake haichezi, yataachwa.

Lakini ikiwa yatakuwa hayapo imara au yanaleta changamoto zozote kwenye ulaji, upumuaji au ukuaji wa mtoto, daktari anaweza kushauri yatolewe kwa upasuaji.

Muhtasari

Wazazi wasijiamulie wenyewe wakiwa nyumbani maana meno haya yanaweza kuwa na athari kubwa kwa mtoto.

Baadhi huathiri ulimi na kumfanya mtoto ashindwe kula, pia humfanya ashindwe kupumua vizuri.

Inaweza kuwa hatari.

Share This Article