Umri sahihi wa Mtoto kuanza Kukaa

2 Min Read

Wazazi wengi husubiri muda huu kwa hamu kubwa ili wapunguze majukumu ya kumbeba mara kwa mara.

Muda huu huwapa pia watoto wenyewe fursa ya kucheza na kujichanganya na watoto wengine.

Kwa mujibu wa Kituo cha Udhibiti na Kinga ya Magonjwa (CDC), watoto wengi huanza kukaa pasipo usaidizi wowote wanapokuwa na umri wa miezi 6.

Tafiti zinaeleza kuwa sababu za kibaiolojia hasa zile zinazohusisha ukuaji wa mwili na ubongo, mazingira na tabia hutoa mchango mkubwa kwenye kuanzisha tabia hii mpya ya kukaa kwa mtoto. (1)

Mfano katika utafiti mmoja ilionekana kuwa, watoto wa Kenya na Cameroon hukaa mapema zaidi kuliko watoto wa Marekani, wakiwa na wastani wa miezi 5 pekee. (2)

Mambo Muhimu Kuzingatia

Mtoto aanze kukalishwa chini kwa usaidizi baada ya kujiridhisha kuwa misuli ya shingo, mgongo na sehemu ya juu ya mwili imekaza.

Huu ni wakati ambao mtoto huwa na udhibiti wa kutosha wa viungo na misuli yake.

  • Anza kumpatia usaidizi wa kukaa anapofikia umri wa miezi 4
  • Mkalishe kwenye chombo kipana au katikati ya miguu yako
  • Mkalishe walau mara 2-3 kwa siku
  • Usimuache akae kwa muda mrefu sana, ukiona anaanza kulia au kutoa miguno isiyo ya kawaida fahamu kuwa kachoka

Ni kosa kubwa kumkalisha mtoto kwa muda mrefu hasa pale anapokuwa bado hajazoea.

Aidha, usimuache peke yake pasipo uangalizi wako.

Muhtasari

Mtoto anaweza kuwahi au kuchelewa zaidi kukaa tofauti na watoto wengine.

Usilazimishe mwanao afanane na mtoto wa mtu mwingine kwenye kila kitu.

Ikiwa kuna changamoto zozote zinazomfanya akawie kukaa, fika hospitalini kwa uchunguzi na ushauri.

Share This Article