Baadhi ya wanawake hutumia dawa za Metronidazole au maarufu kwa jina la kibiashara kama Flagyl kuzuia ujauzito kama njia mbadala ya uzazi wa mpango.
Uhalisia
Metronidazole (flagyl) haiwezi kuzuia ujauzito kwa namna yoyote ile kwa kuwa hushughulika na vimelea vya magonjwa na si vinginevyo.
Metronidazole haijatengenezwa kwa homoni, haina sifa ya kusisimua mji wa uzazi, pia haiwezi kuingilia mfumo wa vichocheo vya mwili wa mwanamke ambavyo huongoza utengenezwaji wa ujauzito. (1,2,3)
Ujauzito siyo bakteria wala kimelea kingine chochote cha ugonjwa.
Matumizi mabaya ya dawa hii kwa sababu zisizo za kitabibu huleta athari kubwa ya usugu wa vimelea vya magonjwa. (4,5)
Hufanya wahusika wapitie kipindi kigumu cha kupona pale wanapougua magonjwa ya kawaida mfano UTI na PID.
Njia Sahihi
Kama mwanamke anataka kuzuia ujauzito, ni muhimu akafuata taratibu sahihi za njia za kisasa za uzazi wa mpango kama kitanzi, vijiti, depo provera au majira.
Kwa ujauzito wa dharura, dawa kama levonorgestrel hufaa kwa kazi hii.
Muhtasari
Metronidazole ni dawa iliyo na ufanisi mkubwa katika kutibu magonjwa mengi.
Imeanza kutumika tangu mwishoni mwa miaka ya 1950.
Unashauriwa kufuata ushauri na taratibu sahihi za matumizi ya dawa hii ili kuepuka athari mbaya zinazoweza kutokea kwa afya yako.