Ni wazi kuwa ulipokuwa mtoto mdogo wazazi wako walikukataza kula limao au ndimu kwa maelezo kwamba inakausha damu.
Kama haukupata karipio hili pengine wewe ni mtoto wa miaka ya 2000.
Madai haya yapo sahihi?
Virutubisho
Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), kwenye kila gramu 100 za limao au ndimu, asilimia 89 ya uzito wake huwa ni maji.
Huwa pia na nishati, protini, wanga, nyuzilishe, madini ya calcium, magnesium, phosphorus, potassium, sodium, zinc, copper, selenium na kiasi kidogo cha sukari.
Aidha, huwa na vitamini C, citric acid, vitamini B12, folate pamoja na viondoa sumu vya carotene, vitamini E, lutein na zeaxanthin.
Uhalisia
Madini ya chuma huhitajika kwenye kutengeneza damu mwilini.
Unaweza kuyapata kupitia mlo au kwa kutumia virutubisho na dawa zenye madini haya.
Ili mwili uweze kufyonza vizuri madini ya chuma kutoka kwenye vyakula, vitamini C na citric acid huhitajika ili kurahisisha zoezi hilo.
Ni wazi ule msemo wa kuwa limao hupunguza damu siyo sahihi, upuuze.
Tunda hili huusaidia mwili kutengeneza damu. (1,2)
Folate na vitamini B12 hufanya kazi kwa pamoja katika kutengeneza chembechembe nyekundu za damu pamoja na kuboresha utendaji kazi wa madini ya chuma. (3)
Muhtasari
Hakuna uhusiano wowote uliopo kati ya limao na kumaliza damu mwilini.
Kama tulivyoona, limao halimalizi damu bali huongeza uwezo wa mwili kwenye kuizalisha na kuitumia.
Tumia limao pasipo kuogopa.