Dalili, Kinga na Matibabu ya Ugonjwa wa Mpox (Monkeypox)

7 Min Read

Mwaka 1958, nyani wawili waliokuwa wanafugwa kwa ajili ya shughuli za kitafiti walipatwa na tatizo la kutokwa na vipele vikubwa mwilini.

Aina hii ya vipele inafanana na ile ya ugonjwa wa ndui na tetekuwanga.

Hii ndiyo sababu iliyofanya ugonjwa huu ukaitwa ugonjwa wa virusi vya nyani, au monkeypox disease. Kisa cha kwanza cha maambukizi ya ugonjwa huu kwa binadamu kiliripotiwa mwaka 1970 huko Congo, DRC.

Kusambaa Duniani

Baada ya hapo, ugonjwa huu umesambaa kwenye nchi nyingi za Afrika ya Kati na Magharibi ikihusisha Sierra Leone, Liberia, Nigeria, Gabon, Ivory Coast na Cameroon.

Katika nyakati kadhaa, nchi zingine duniani zimeripoti pia kutokea kwa visa vya ugonjwa huu mfano Marekani, Uingereza na Singapore.

Sababu kuu inatajwa kuwa ni usafirishaji wa wanyama pamoja na safari za kawaida za binadamu.

Sifa za Virusi

Virusi vya monkeypox vipo kwenye kundi la viral zoonosis, ikimaanisha kuwa ni aina ya virusi inayomuambukiza binadamu kutoka kwa wanyama wengine.

Ni kirusi chenye sifa ya kubeba vinasaba vya DNA.

Ni jinasi Orthopoxvirus inayopatikana kwenye familia ya Poxviridae. (1,2)

Hadi sasa, imethibitika kuwa kuna jamii mbili za virusi vya ugonjwa wa monkeypox ambavyo ni jamii ya Afrika ya kati na jamii ya Afrika Magharibi. (3)

Virusi vyenye asili ya Afrika ya kati ndiyo husababisha maambukizi makali zaidi, huwa pia na sifa ya kusambaa kwa kasi zaidi.

Uambukizwaji

Binadamu hupata vimelea vya ugonjwa huu kwa kukutana moja kwa moja na damu, majimaji au kupitia ngozi iliyo wazi ya mnyama aliye athirika.

Inaaminika kuwa, ulaji wa nyama isiyo iva vizuri au mazao mengine ya wanyama walio athirika na ugonjwa huu inaweza kuwa njia nyingine ya kupata maambukizi.

Binadamu mmoja anaweza pia kumuambukiza mwingine kupitia hewa, ute na majimaji yanayozalishwa na mfumo wa upumuaji, vidonda, michubuko na sehemu zingine za ngozi iliyo wazi au pia kupitia vitu vilivyo achiwa masalia ya virusi hawa baada ya kuguswa au kutumiwa na mgonjwa.

Njia ya mwisho ya kuambukizwa ugonjwa huu ni ile ya mama kwa mtoto kupitia kondo la uzazi pia wakati na baada ya kuzaliwa.

Dalili

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huu hutumia siku 6-13 kuanza kuonesha dalili za uwepo wake.

Hata hivyo, kwa baadhi ya watu hutumia siku 5-21.

Dalili za ugonjwa huu zimegawanyika kwenye makundi mawili kutokana na hatua ya ugonjwa kwa wakati huo.

1. Hatua ya Kwanza

Hatua hii hufahamika zaidi kama kipindi cha uvamizi.

Huonekana kwa siku 5 mfulilizo kuanzia siku ya kwanza tangu vimelea viingie mwilini.

Huambatana na dalili za homa, maumivu makali ya kichwa, maumivu makali ya mgongo, maumivu ya misuli, kudhoofika, kuishiwa nguvu pamoja na kuvimba kwa tezi za lymph ambazo nyingi hupatikana shingoni, kifuani, chini ya tumbo na sehemu ya kwapa.

    2. Hatua ya Pili

    Hatua hii huanza kuonekana siku 1-3 baada ya kuisha kwa homa.

    Ngozi huanza kutokwa na vipele vikubwa vikianzia usoni.

    Husambaa kwenye mikono, kinywa, sehemu za siri, macho na kisha kuonekana mwili mzima.

    Vipele hivi huanza vikiwa vikavu, kisha hutengeneza majimaji, baadae usaha na hatimaye hukauka na kusababisha mabaka na ugumu wa ngozi.

    Ugonjwa huu siyo hatari sana kwa maana ya kuua.

    Kwa mujibu wa Kituo cha Udhibiti na Kinga ya Magonjwa (CDC), ni wastani wa mtu mmoja pekee katika kila wagonjwa 10 ndiye hufariki.

    Dalili za ugonjwa huu hupotea zenyewe tu baada ya wiki 2-4.

    Makundi Hatari

    Watu wenye kinga duni za mwili, watoto wadogo pamoja na watu wenye umri chini ya miaka 40-50 wanaweza pia kuwa kwenye hatari ya kupatwa na ugonjwa huu kutokana na kupungua kwa kinga za ugonjwa huu. (4)

    Ifahamike kuwa, kupitia chanjo ya ugonjwa wa ndui ambayo kila mtu alipata akiwa mtoto mchanga, ugonjwa huu unaweza pia kukingwa kwa maana virusi hivi hupatikana kwenye kundi moja.

    Kwa watu wachache sana, ugonjwa huu unaweza kusababisha nimonia kali, maambukizi ya damu, maambukizi ya ubongo pamoja na kupungua kwa uoni wa macho au upofu. (5,6)

    Tiba

    Hakuna tiba ya ugonjwa huu. Huisha wenyewe tu ndani ya wiki 2-4 tangu mgonjwa aanze kuonesha dalili za kwanza za uwepo wake.

    Baadhi ya dawa zinaweza kutolewa ili kupunguza maumivu na athari za ugonjwa zinaoweza kuwa zinaonekana kwa wakati huo.

    Kinga

    Kwa mujibu wa CDC, chanjo ya ugonjwa wa ndui imebeba ufanisi wa zaidi ya asilimia 85 katika kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa monkeypox.

    Chanjo hii inapaswa kutolewa kabla ya kupatwa na maambukizi ya ugonjwa.

    Hata hivyo, chanjo hii inaweza pia kutolewa ndani ya siku 1-4 baada ya kuambukizwa ugonjwa huu ili kuzuia muendelezo wa kukua kwa ugonjwa.

    Ikiwa chanjo hii itatolewa kati ya siku ya 4-14 tangu maambukizi yatokee, haitazuia kutokea kwa ugonjwa bali itapunguza ukubwa wa dalili.

    Muhtasari

    Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa monkeypox vinapatikana kwenye kundi moja ambalo hubeba pia virusi vya ugonjwa wa ndui ambao WHO ilitangaza kuutokomeza duniani mwaka 1980 baada ya kuwekeza nguvu kubwa ya utoaji wa chanjo iliyotengenezwa na Edward Jenner mwaka 1796.

    Ugonjwa huu ulidumu kwa zaidi ya miaka 3000 duniani na unatajwa kuwa miongoni mwa magonjwa ya hatari zaidi kuwahi kuwepo kwenye uso wa dunia.

    Ugonjwa wa monkeypox unataka kufanana na huu kwa muonekano, japo kasi ya usambaaji na hatari ya kusababisha vifo ni ndogo sana ukilinganisha na ile ya ugonjwa wa ndui.

    Ni muhimu kufuatilia taarifa za mara kwa mara zinaoonesha maeneo yaliyo thibitika kuwa na ugonjwa huu ili uweze kuchukua tahadhari zote za kujikinga.

    Kutokana na uwepo wa viashiria vya unyanyapaa, ugonjwa huy kwa sasa unafahamika kwa jina jipya la mpox.

    Share This Article