UHALISIA: Nanasi Haliharibu Ujauzito

3 Min Read

Umewaki kula nanasi? hili ni tunda lenye faida lukuki kwa afya.

Faida za tunda hili huanzia kwenye kuongeza kinga ya mwili, kutibu mafua, kupambana na saratani, kuondoa maumivu pamoja na kulinda moyo.

Tunda hili huhusishwa na kuharibu ujauzito mchanga kwa wanawake.

Athari hii hutokana na uwepo wa vimeng’enya vya bromelain ambavyo kiasili hupatikana kwenye nanasi pekee. Bromelain ni kundi kubwa la vimeng’enya vinavyopatikana kwenye tunda la nanasi. (1)

Kazi kubwa ya bromelain ni kusaidia mmeng’enyo wa vyakula vyenye asili ya protini.

Uhalisia

Vidonge vyenye bromelain huwa havishauriwi kumwezwa na mwanamke mjamzito kwa sababu vinaweza kumfanya apoteze damu nyingi pamoja na kuharibu ujauzito.

Vimeng’enya hivi hupatikana pia kwenye nanasi. Usalama kwa wanawake wajawazito upoje?

Bromelain inayopatikana kwenye nanasi ni chache sana kuweza kuleta athari zozote kwa ujauzito. Pia, hakuna tafiti za kisayansi zinazothibitisha madhara haya kwa binadamu.

Kwa maana hiyo, nanasi linabaki kuwa tunda bora sana kwa mwanamke mjamzito.

Faida Kwenye Ujauzito

Nanasi ni tunda ambalo limesheheni virutubisho vingi vyenye faida kubwa kwa mama mjamzito.

Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), tunda hili huwa na protini, nyuzilishe, madini ya chuma, calcium, potassium, phosphorus, sodium, zinc na copper.

Huwa pia na vitamini A, beta carotene, vitamini C na vitamini E.

Uwepo wa madini ya chuma utaongeza wingi wa damu mwilini. (2,3)

Folate husaidia kutengeneza mfumo imara wa neva za fahamu za mtoto, pamoja na kuepusha tatizo la kuzaliwa akiwa na mgongo wazi. (4)

Vitamini A husaidia kuikarisha mfumo wa kinga mwili za mtoto pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na kuhara na maambukizi ya mfumo wa upumuaji. (5)

Madini ya calcium husaidia kuboresha afya ya mifupa na meno kwa mama na mtoto. (6,7)

Madini ya potassium husaidia kudhibiti ongezeko la shinikizo la damu ambalo linaweza kusababisha kutokea kwa kifafa cha mimba pamoja na changamoto zingine za uzazi. (8,9,10)

Wanawake wajawazito huwa kwenye hatari kubwa ya kupatwa na choo kigumu na ugonjwa wa bawasiri. Uwepo wa kiasi kikubwa cha nyuzilishe husaidia kuepusha changamoto hii. Ni nzuri pia katika kuzuia saratani ya utumbo mkubwa. (11,12)

Ugonjwa wa UTI hutokea mara kwa mara wakati wa ujauzito kwa kuwa mji wa uzazi hukibana kibofu cha mkojo, huzuia kutolewa nje kwa mkojo wote pamaja na kutengeneza mazingira mengine rafiki ya kuzaliana kwa vimelea vya magonjwa. (13)

Uwepo wa vitamini C huepusha kutokea kwa changamoto hii.

Muhtasari

Maudhi pekee ya bromelain yaliyo thibitishwa na tafiti ni kusababisha maumivu ya tumbo, kuhara, kutapika na kuongezeka kwa mapigo ya moyo.

Mambo haya hutokea baada ya kutumia kiasi kikubwa cha bromelain kwa njia ya dawa au nanasi.

Kuhusu kuharibu ujauzito bado inabaki kuwa hadithi ya mtaani.

Share This Article