Asili ya tunda la nanasi inasemekana kuwa ni bara la Marekani Kusini.
Mtembezi na mtafiti wa mambo ya kihistoria bwana Christopher Columbus ndiye mzungu wa kwanza kugundua matunda haya baada ya kufika kwenye bara hilo mwaka 1493.
Alipokuwa anarudi Ulaya alibeba matunda haya, ndiyo ukawa mwanzo wa kusambaa duniani kote.
Unaipenda historia? Tuwaachie wanahistoria wenyewe.
Virutubisho
Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), nanasi huundwa kwa maji, nishati, protini, wanga, nyuzilishe, aina mbalimbali za sukari na folate.
Huwa pia na vitamini C pamoja na madini ya chuma, calcium, potassium, sodium, magnesium pamoja na phosphorus.
Fahamu faida za nanasi kwa afya yako.
1. Bromelain
Unajua kuwa nanasi ndiyo tunda pekee duniani lenye vimeng’enya vya bromelain?
Huchukua zaidi ya asilimia 90 ya vimeng’enya vyote vinavyopatikana kwenye nanasi. (1)
Vimeng’enya hivi vinavyotumika katika kuvunja protini mwili huwa na faida nyingi kwa afya.
Husaidia kutibu changamoto za mfumo wa upumuaji kwa kupambana na maambukizi ya bakteria na virusi. Huondoa mafua. (2,3)
Husaidia kuondoa maumivu mwilini hasa yale yanayotokea kwenye maungio ya mifupa, kuvimba kwa tishu pamoja na baridi yabisi. (4,5)
Hupambana na aina mbalimbali za uvimbe joto mwilini. (6,7)
Huzuia kuongezeka kwa shinikizo la juu la damu, kiharusi, shambulio la moyo pamoja na kuzuia kuganda kwa damu kwenye mishipa. (8,9,10)
Hutibu tatizo la pumu ya mfumo wa hewa. (11)
Hudhibiti ukuaji na usambaaji wa seli zinazosababisha saratani. Inaweza kutumika katika kutibu ugonjwa huu. (12,13,14)
Hupambana na aina mbaya za bakteria hasa wale wanaosababisha magonywa ya kinywa, uzazi na mfumo wa chakula. (15,16)
Hutibu vidonda vinavyosababishwa kuungua moto kwa kuondoa tishu mfu. (17,18)
Hutumiwa viwandani kwenye kuandaa nyama. Hulainisha nyama hizi ili zifae kwa matumizi ya kawaida ya binadamu. (19)
2. Urembo
Ulaji wa nanasi, au kupaka moja kwa moja kwenye ngozi hufaa katika kupunguza makunyanzi, kuongeza mng’ao wa ngozi pamoja na kupambana na mionzi mikali ya jua.
Muunganiko wa vitamini C pamoja na vimeng’enya vya bromelain ndiyo hufanikisha kazi hii. (20)
Husaidia pia katika kutibu changamoto ya uwepo wa chunusi.
3. Mfumo wa Chakula
Tunda hili huwa na faida tatu kwenye mfumo wa chakula.
Moja, uwepo wa maji na nyuzilishe husaidia kupambana na changamoto ya choo kigumu. (21,22)
Bromelain hutumika kumeng’enya vyakula vya protini pia huzuia misisimko ya uvimbe inayoweza kuathiri mfumo wa chakula.
Husaidia kukinga ili saratani ya utumbo mkubwa isitokee. Hii inatokana na uwepo mwingi wa nyuzilishe.
4. Kinga
Huwa na kiwango kikubwa cha vitamin C na zinc inayohitajika katika kuongeza ubora wa mfumo wa kinga mwili. (23,24)
Ongeza ulaji wa nanasi ili usahau kuugua kwa mara kwa mara.
5. Uzazi
Mjumuisho wa vitamini C, beta carotene, zinc na copper husaidia kuboresha afya ya uzazi kwa wanawake na wanaume.
Mfano, zinc kwa wanawake huboresha mzunguko wa hedhi na kusaidia upevushaji wa mayai. Kwa wanaume huongeza ubora wa afya ya mbegu za kiume. (25,26)
6. Sumu
Sumu za mwili hupoozesha mfumo wa kinga, huua seli za mwili na kuongeza uwezekano wa kuugua magonjwa sugu hasa kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na saratani.
Nanasi hubeba kiasi kikubwa cha viua sumu vinavyopatikana kwenye kampaundi mbili za phenolic na flavonoids. (27,28)
Hivi vinafaa kwa afya katika kuua na kuondoa sumu hatari kwa afya.
7. Upasuaji
Vimeng’enya vya bromelain husaidia kupambana na aina mbalimbali za uvimbe, hupunguza maumivu ya mwili pamoja na kurahisisha uponaji wa vidonda vikubwa vya mwili. (29,30)
Mtu aliyefanyiwa upasuaji huwa na mambo haya yote.
Ni tunda muhimu sana kwa watu hawa.
Nanasi kwa Wanawake Wajawazito
Vidonge vyenye bromelain huwa havishauriwi kumwezwa na mwanamke mjamzito kwa sababu vinaweza kumfanya apoteze damu nyingi pamoja na kuharibu ujauzito.
Vimeng’enya hivi hupatikana pia kwenye nanasi. Usalama kwa wanawake wajawazito upoje?
Bromelain inayopatikana kwenye nanasi ni chache sana kuweza kuleta athari zozote kwa ujauzito. Pia, hakuna tafiti za kisayansi zinazothibitisha madhara haya kwa binadamu.
Kwa maana hiyo, nanasi linabaki kuwa tunda bora sana kwa mwanamke mjamzito.
Uwepo wa madini ya chuma utaongeza wingi wa damu mwilini. (31,32)
Folate husaidia kutengeneza mfumo imara wa neva za fahamu za mtoto, pamoja na kuepusha tatizo la kuzaliwa akiwa na mgongo wazi. (33)
Virutubisho vingine pia hufaa kwa afya ya mama mjamzito pamoja na mtoto tumboni.
Muhtasari
Tunda hili pia hufaa sana kwa watu wanaofanya mazoezi yanayohitaji matumizi ya nguvu nyingi. Husaidia kupunguza maumivu ya misuli pamoja na kuondoa uchovu. (34)
Kwa wagonjwa wa kisukari, tunda hili hushauriwa litumike kwa kiasi ili kuepusha ongezeko kubwa la sukari mwilini.
Unajua kwanini baada ya kula nanasi mdomo huwa mchungu ikiwa utaamua kunywa maji?
Ni kazi ya bromelain.

