Curcumin ni kemikali yanye rangi ya manjano inayopatikana kwenye kundi kubwa la familia ya mimea Zingiberaceae.
Ni kemikali kuu inayopatikana kwenye binzari manjano.
Binzari manjano ni mzizi unaotumika kwa kazi nyingi zinazohusisha urembo, tiba mbadala na utengenezaji wa aina mbalimbali za vyakula.
Faida nyingi za binzari manjano husababishwa na uwepo wa kemikali za curcumin, hivyo mjadala wetu kwenye makala hii kwa kiasi kikubwa utaangazia kemikali hii kwa sehemu kubwa.
Virutubisho
Kwa mujibu wa Idara ya Chakula ya Marekani (USDA), binzari manjano hubeba mjumuisho wa nishati, maji, protini, nyuzilishe, sukari pamoja na madini ya chuma, potassium, sodium, calcium, magnesium, phosphorus, potassium, zinc, copper na selenium.
Huwa pia na folate, choline, betaine, niacin, riboflavin na vitamini B6.
Virutubisho na madini haya vyote kwa pamoja hufaa kwa afya ya mwili.
1. Saratani
Kuna zaidi ya aina 200 za saratani.
Huu ni ugonjwa hatari unaotokana na kukosekana kwa udhibiti kwenye taarifa za ukuaji wa seli za mwili.
Curcumin hudhibiti kutokea kwa saratani mwilini, lakini huenda mbali zaidi kwa kuzifanya seli husika zife, hupunguza utengenezwaji wa mishipa mipya ya damu kwenye maeneo yenye saratani pamoja na kudhibiti usambaaji kutoka sehemu moja ya mwili kwenda sehemu nyingine.
2. Sumu
Siyo lazima unywe sumu ya kununua dukani ndiyo mwili wako upate madhara.
Kuna baadhi ya sumu huwepo mwililini ambazo hutokana na mazao ya kemikali na mifumo ya mwili.
Sumu hizi huathiri afya ya mwili kwa ujumla, husababisha magonjwa sugu, uzee na kufa kwa seli za mwili.
Binzari manjano huwa na viondoa sumu vingi ambavyo huboresha afya ya mwili kwa kuharibu sumu hizo.
3. Uvimbe
Hudhibiti mwamsho wa taarifa za mwili zinazo sababisha uvimbe.
Kwa miaka mingi, sehemu kadhaa za mzizi huu zimekuwa zinatumika kama malighafi katika kutengeneza virutubisho na dawa mbalimbali.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa aina nyingine pia za virutubisho, majibu yake huchukua muda mrefu kuonekana, na inapaswa itumiwe mara kwa mara.
4. Moyo
Moyo huanza kufanya kazi tangu siku ya 22 baada ya kutungwa kwa ujauzito.
Huendelea kufanya kazi hii hadi sekunde ya mwisho ya uhai inapofika.
Moyo huwa na mfumo wake wa kufanya kazi unaoufanya usichoke wala kusimama.
Hata hivyo, changamoto za kimazingira, tabia, mtindo wa maisha, vyakula na vinywaji tunavyotumia pamoja na mashambulizi ya vimelea vya magonjwa huudumaza moyo huu.
Curcumin inayopatikana kwenye binzari manjano huboresha afya ya moyo na mishipa ya damu, hudhibiti shinikizo la damu pamoja na kupambana na visababishi mbalimbali vya magonjwa ya moyo. (1,2)
Ni kiungo kizuri katika kulinda na kutunza afya ya moyo.
5. Macho
Wastani wa watu bilioni 2.2 duniani wanakabiliwa na changamoto za uoni hafifu.
Matatizo ya macho yanatazamiwa kuendelea kuongezeka kila mwaka duniani kama jithada za haraka hazitafanyika kwenye kuchukua hatua sahihi za kujikinga.
Kwa hatua ya sasa, usihangaike kutafuta jawabu la kinga ya magonjwa haya.
Tumia binzari manjano, zina uwezo wa kukinga pamoja na kutibu changamoto nyingi zinazohusisha magonjwa ya macho.
6. Figo
Kazi kuu ya figo ni kuchuja damu na uchafu pamoja na kutengeneza mkojo.
Ugonjwa sugu wa figo huondoa uwezo wa viungo hivi katika kufanya kazi yake kikamilifu.
Hii ni hatua mbaya na kubwa zaidi ya uharibifu wa viungo hivi.
Binzari manjano kupitia kemikali zake za curcumin huzilinda figo kwa nguvu kubwa. Aidha, husaidia kuleta ahueni kwa watu ambao tayari wanao ugonjwa wa figo. (3,4)
Tiba ya kudumu ya ugonjwa sugu wa figo ni kupata huduma ya dialysis au kupandikizwa figo mpya.
Unataka ufike huku? Tumia mzizi huu.
7. Baridi Yabisi
Ugonjwa huu kwa kiingereza huitwa arthritis.
Husababisha kuvimba na uwepo wa maumivu makali kwenye maungio ya mwili.
Katika utafiti mmoja, matumizi ya curcumin kwa watu wenye ugonjwa huu yalionesha majibu mazuri zaidi kuliko kundi la watu waliokuwa wanatumia dawa za kawaida za hospitalini. (5)
Tafiti nyingine pia zinabainisha uwepo wa kemikali hii kwenye kutibu ugonjwa wa baridi yabisi. (6,7)
8. Urembo
Pengine ulidhani mzizi huu huwa na faida kwa ngozi pekee kwa kuwa huwa unatumia unga au scrub yake kwa ajili ya kazi hiyo.
Ni kweli haujakosea. Binzari manjano huwa na faida kubwa kwenye ngozi.
Husaidia katika kuondoa makunyazi, mabaka, uvimbe, chunusi pamoja na kuongeza mng’ao wa ngozi.
9. Magonjwa ya Akili
Magonjwa ya akili yamekuwa yanaongezeka siku hadi siku.
Baadhi ya magonjwa hata hutokana na sababu zinazoweza kuzuilika, na baadhi hutokana na mambo yaliyo nje ya uwezo wa mhusika.
Kemikali za curcumin zinazopatikana kwenye binzari manjano zimeelezewa na tafiti kuwa na uwezo wa kuulinda ubongo, kuongeza uwezo wa kutunza kumbukumbu pamoja na kuzuia magonjwa ya akili hasa yale yanayotokana na uzee.
10. Vidonda vya Tumbo
Ugonjwa wa vidonda vya tumbo husababishwa na maambukizi ya vimelea vya bakteria jamii ya H. pylori.
Binzari manjano inaweza kusaidia katika kutibu ugonjwa huu hasa ambao chanzo chake ni maambukizi ya vimelea vya H. pylori.
11. Kisukari
Mwaka 2019, kisukari ulikuwa ni ugonjwa wa tisa unaoongoza kwa kuua watu duniani. Hii ni sawa na wastani wa vifo milioni 1.5 (8)
Curcumin hudhibiti wingi wa sukari kwenye damu pamoja na kupunguza changamoto zingine zinazotokana na ugonjwa huu. (9,10)
Hufanya hivyo kwa kuongeza msisimko wa vimeng’enya vya insulin kwenye kuweka sawa uwiano wa sukari, pamoja na kuamsha mifumo mingine ya mwili inayosaidia na kuratibu matumizi ya sukari.
Muhtasari
Matumizi ya mzizi huu yanakadiriwa kuanza zaidi ya miaka 4000 iliyopita kwenye tamaduni za Vedic nchini India.
Inadhaniwa kuwa mzizi huu ulianza kutumiwa nchini China mwaka 700, Afrika Mashariki mwaka 800, Afrika Magharibi mwaka 1200 na Jamaika kwenye karne ya 18. (11)
Wewe siyo wa kwanza kutumia, wazee waliona faida zake kabla yako.