Nyanya: Virutubisho, faida na tahadhari zake

4 Min Read

Watu wengi hutumia nyanya kama kiungo pasipo kujua kuwa huwa na faida nyingi sana kwa afya zao.

Asili ya nyanya inatajwa kuwa ni nchi za Peru na Ecuador. (1)

Virutubisho

Ni chanzo kizuri cha vitamini C, potassium, folate, vitamini K, nyuzilishe pamoja na kampaundi za lycopene, beta carotene, naringenin na chlorogenic acid.

Huwa na faida zifuatazo kwa afya;

1. Saratani

Ugonjwa huu hutokana na kukosekana kwa udhibiti wa ukuaji wa seli za mwili.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), saratani iliua zaidi ya watu milioni 10 duniani, hii ni sawa na mtu mmoja katika kila watu 6 wanaofariki.

Kampaundi za lycopene zinazopatikana kwenye nyanya huwa na uwezo wa kupambana na aina mbalimbali za saratani hasa ile ya matiti, tezi dume, mapafu na tumbo.

Tumia nyanya ili ujikinge na saratani.

2. Damu na Moyo

Lycopene husaidia mwili kushusha shinikizo la juu la damu. (1,2)

Hufanya pia kazi ya kuharibu lehemu mbaya kwenye mishipa ya damu.

Faida hizi kwa pamoja huwa na athari chanya kwenye kuboresha afya ya mfumo mzima wa damu pamoja na moyo.

3. Kiharusi

Kiharusi ni ugonjwa mbaya unaosababisha kupooza kwa baadhi ya viungo na sehemu za mwili. Kwa nchi ya Uingereza, wastani wa watu 100,000 kila mwaka hupatwa na kiharusi. (3)

Nyanya husaidia kuimarisha afya ya mishipa ya damu, huharibu lehemu mbaya, hushusha presha pamoja na kuzuia kuganda kwa damu kwenye mishipa yake.

Tafiti zinabainisha kuwa, jamii zinazotumia nyanya kwa kiasi kikubwa huwa na visa vidogo zaidi vya kiharusi. (4,5)

4. Ngozi

Changamoto kubwa inayoathiri ubora wa ngozi ni uwepo wa mionzi mikali ya jua.

Mionzi hii husababisha saratani, kuzeeka mapema kwa ngozi pamoja na makunyanzi.

Ulaji mwingi wa nyanya, au matumizi yake kwenye urembo wa ngozi kama scrub husaidia kuepusha athari za mionzi mikali ya jua kwenye ngozi.

5. Wanaume

Huongeza ubora wa mbegu za kiume.

Katika utafiti mmoja uliofanyika kwenye kundi la wanaume 44, uwezo wa kuogelea wa mbegu za kiume uliongezeka mara dufu baada ya kutumia nyanya zenye kiasi cha 30 mg za lycopene kwa wiki 6 mfululizo. (6)

Hii inatoa maana kuwa matumizi ya nyanya, au virutubisho vyenye kiasi kikubwa cha lycopene vinaweza kusaidia kutatua changamoto ya uzalishaji wa mbegu za kiume zenye uwezo hafifu wa kuogelea.

6. Macho

Nyanya hubeba kiasi kikubwa cha lutein na zeaxanthin ambavyo hulinda macho yako yasipate upofu, pamoja na kupunguza athari za mionzi ya simu na vifaa vingine vyenye kutoa mwanga mkali ili usiyaathiri. (7,8)

Huwa pia na beta carotene ambazo hubadilishwa kuwa vitamini A.

Husaidia kuongeza uoni wa macho pamoja na kupunguza changamoto za magonjwa ya macho yanayotokana na uzee.

Tahadhari

Tafiti kadhaa zimebaini uwepo wa masalia ya viuatilifu vya DDT, methamidophos, methomyl, dimethoate, profenofos, pirimiphos-methyl difenoconazole, cyprodinil na boscalid kwenye nyanya. (9)

Hata hivyo, viuatilifu hivi vinapatikana kwenye kiwango kidogo kinacho tambulika kutokuwa na athari kwa afya. Inashauriwa kupika vizuri nyanya walau kwa dakika 15 ili kuondoa kabisa athari za masalia haya.

Ulaji wa nyanya mbichi unaweza pia kusababisha sumu ya chakula ambayo dalili zake ni kuhara, homa na maumivu makali ua tumbo.

Ni muhimu kuwa makini unapokuwa unatumia nyanya mbichi mara kwa mara.

Share This Article