Yogurt: Virutubisho, Faida na Tahadhari kwa Afya

7 Min Read

Yogurt ni chakula kilichoanza kutumiwa na binadamu tangu enzi za kale.

Inaaminika kuwa neno yogurt limetoholewa kutoka kwenye lugha ya kituruki-yoğurmak likimaanisha kugandisha au kufanya kitu kiwe kizito.

Katika uwanda wa tiba na matumizi ya yogurt kwa ajili ya kuboresha afya ya binadamu, machapisho yanaeleza mtindi kuanza kutumika tangu miaka ya 6000 KK nchini India.

Virutubisho

Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), yogurt hubeba mjumuiko wa maji, nishati, protini, mafuta pamoja na madini chuma, calcium, zinc, magnesium, phosphorus, potassium, sodium na selenium.

Huwa pia na riboflavin, vitamini A, B6 na B12 pamoja na choline.

Utengenezwaji

Yogurt hutengenezwa kwa kuongeza aina fulani ya bakteria kwenye maziwa.

Utaratibu huu hupaswa kufanyika kwenye mazingira yaliyodhibitiwa.

Katika kufanikisha hili, bakteria wenye uwezo wa kuzalisha lactic acid ndiyo hutumika. Mfano wa bakteria hao ni Streptococcus thermophilus na Lactobacillus bulgaricus.

Fahamu sasa faida za yogurt;

1. Saratani

Bakteria wanaozalisha lactic acid huharibu kemikali zinazosababisha saratani ya utumbo mkubwa.

Aidha, huongeza kinga ya mwili kwenye kupambana na saratani hii, hujishikiza kwenye kemikali hatari na kuziharibu pamoja na kuongeza idadi ya bakteria wazuri kwenye mfumo wa chakula.

Tafiti kadhaa za afya zinabaibisha kuwa yogurt pamoja na aina nyingine za vyakula ambavyo hutengenezwa na jamii ya bakteria wazuri hasa wale wanaozalisha lactic acid hufaa kwenye kukinga saratani ya utumbo mkubwa. (1,2)

Tumia yogurt ujikinge na saratani.

2. Mfumo wa Fahamu

Aina mbalimbali za kundi kubwa la vitamini B huboresha afya ya ubongo.

Huongeza uwezo wa kutunza kumbukumbu na kufikiri. Pia, hutoa kinga dhidi ya aina mbalimbali ya magonjwa ya akili.

Kwa mwanamke mjamzito, huboresha afya ya mtoto kwa kumfanya azaliwe akiwa na mfumo bora wa fahamu, pia humuepusha na changamoto kadhaa za kuzaliwa na mapungufu kwenye viungo vya mwili ikiwemo kuzaliwa akiwa na mgongo wazi. (3,4)

Tumia yogurt ili ikusaidie.

3. Mifupa

Madini ya calcium huhitajika mwilini kwenye kutengeneza meno pamoja na mifupa imara.

Moyo, mfumo wa fahamu pamoja na misuli mwili vyote huhitaji madini ya calcium ili vifanye kazi kikamilifu.

Kopo moja dogo la yogurt linatosha kabisa kukupa zaidi ya asilimia 50 ya mahitaji yako ya calcium kila siku.

4. Kuhara na Choo Kigumu

Tendo la kuhara humfanya mhusika apoteze kiasi kikubwa cha maji na chumvi chumvi za mwili.

Choo kigumu husababisha maumivu makali wakati wa kujisaidia. Kinaweza pia kuleta athari kadhaa kwa afya ikiwemo kutokea kwa ugonjwa wa bawasiri. (5)

Yogurt husaidia kutibu changamoto hizi, hasa ikiwa zimesababishwa na maambukizi ya bakteria, au matumizi ya dawa za antibayotiki.

5. Vidonda vya Tumbo

Sababu kubwa ya kutokea kwa ugonjwa wa vidonda vya tumbo ni uwepo wa maambukizi ya bakteria wa H. pylori au athari za matumizi ya dawa za kuondoa maumivu.

Ulaji wa vyakula vyenye bakteria wanaoweza kuzalisha lactic acid mwilini husaidia katika kupambana na ugonjwa wa vidonda vya tumbo hasa vile vinavyo sababishwa na bakteria jamii ya H. pylori.

Yogurt huwa na bakteria jamii ya Lactobacillus acidophilus La5 au Bifidobacterium lactis Bb12 ambao tafiti nyingi zinabainisha uwezo wao katika kutibu vidonda vya tumbo. (6)

Kama unaumwa jaribu uone. Inaweza kukusaidia.

6. Damu na Moyo

Yugurt husaidia kuongeza kiasi cha lehemu nzuri ndani ya mwili.

Lehemu hii huulinda moyo pamoja na kuupa kinga dhidi ya aina mbalimbali ya magonjwa yanayoweza kuuathiri.

Aidha, huboresha afya ya mishipa ya damu na kupunguza nafasi ya kutokea kwa shinikizo kubwa la damu.

7. Maambukizi ya Uke

Yogurt huwa na bakteria wazuri wanaoitwa Lactobacillus.

Bakteria hawa huishi kwenye uke, mfumo wa chakula pamoja na mfumo wa mkojo.

Hufanya kazi ya kulinda afya ya viungo na mifumo husika, ikiwemo kupambana na vimelea vya magonjwa.

Kwa upekee kabisa, bakteria huwa huwa na uwezo wa kuua na kudhibiti ukuaji wa fangasi wabaya wanaosababisha maambukizi mbalimbali ya uke.

Kwa mujibu wa tafiti, kupaka kiasi kidogo cha yogurt iliyochanganywa na asali kwenye uke husaidia kutibu maambukizi ya fangasi jamii ya candida. (7,8)

Pamoja na uwepo wa faida hii kwa afya, ni lazima yogurt halisi yenye bakteria jamii ya lactobacillus itumike.

Yogurt nyingi zilizopo mtaani huwa na viambato vya nyogeza vyenye rangi na sukari mbadala. Hivi ni hatari kwa afya. Hutengeneza mazingira rafiki yanayoongeza uzalianaji wa fangasi, hivyo kufanya tatizo liwe kubwa zaidi.

8. Uzito

Kwa watu wenye uzito mkubwa, ulaji wa yogurt husaidia kupunguza uzito wa mwili, kuondoa mafuta mabaya pamoja na kupunguza mzingo wa kiuno. (9)

Aidha, huwa na kiasi kikubwa cha protini na calcium ambavyo hufanya kazi kwa pamoja kuongeza uzalishwaji wa vichocheo vinavyoondoa hamu ya kula mara kwa mara. (10)

Chakula hiki hutoa faida ya kumpa mhusika virutubisho vingi kwa wakati mmoja pamoja na kiasi kidogo cha nishati chenye manufaa kwa afya. (11)

9. Mfumo wa Kinga

Huongeza kinga ya mwili kwa wazee na watu wenye magonjwa sugu.

Uweo wa calcium, zinc, aina mbalimbali za vitamini B na protini hufaa kwenye kuongeza kinga ya mwili ya kila binadamu. (12)

Kwa mujibu wa tafiti, bakteria wazuri wanaopatikana kwenye yogurt husadia kutibu changamoto za sehemu ya juu ya mfumo wa hewa hasa mafua.

10. Ngozi

Huboresha afya ya ngozi kutokana na uwepo wa lactic acid.

Kufanya scrub au kujisafisha uso kwa kutumia yogurt husaidia kuondoa seli mfu, kutakatisha mabaka pamoja na kuondoa mikunjo ya ngozi.

Tahadhari

Baadhi ya watu huwa hawana vimeng’enya vinavyoitwa lactase, ambavyo hutumiwa na mwili kwenye kuvunja sukari zilizopo kwenye bidhaa za maziwa.

Baada ya kula bidhaa yoyote ya maziwa, watu hawa wanaweza kupatwa na dalili za tumbo kujaa gesi, kiungulia, kuhara pamoja na maumivu ya tumbo. Watu hawa wanapaswa kuwa makini na matumizi ya yogurt.

Aidha, baadhi ya yogurt huwa na kiasi kikubwa cha sukari za nyongeza ambazo siyo nzuri kwa afya ya binadamu.

Chakula hiki kinaweza kisiwe kizuri sana kwa watu wenye changamoto ya ugonjwa wa kisukari.

Muhtasari

Yogurt ni chakula kinachopatikana karibia kila sehemu.

Huwa na faida kubwa sana kwa afya ya binadamu, pia inafaa kwa urembo wa ngozi.

Ifanye kuwa sehemu ya mlo wako wa kila siku.

Share This Article