Tango: Virutubisho na Faida kwa Afya

6 Min Read

Kuna aina nyingi za matango duniani.

Ukuaji na upatikanaji wa aina hizi hutegemeana na ukanda wa kijiografia pamoja na hali ya hewa ya eneo husika.

Virutubisho

Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), zaidi ya asilimia 95 ya tango huwa ni maji. Hubeba pia nishati, protini, wanga, nyuzilishe, viondoa sumu pamoja na sukari kidogo.

Huwa pia na madini chuma, calcium, zinc, selenium, magnesium, phosphorus, potassium, sodium pamoja na vitamini C, vitamini B6, thiamin, riboflavin na folate.

Faida za tunda hili afya zipo nyingi, baadhi yake ni hizi;

1. Chanzo cha Maji

Maji huchukua asilimia 75 ya uzito wa watoto na wastani wa asilimia 55 kwa watu wazima.

Ni msingi wa uhai wa binadamu kwa kuwa huhitajika kwenye kuwezesha kazi za kila mfumo wa mwili wa binadamu.

Kama ambavyo usipokula utakufa, hali ipo hivyo pia kwa maji. Mwili ukiishiwa maji utakufa.

Unakumbuka kiasi cha maji kilichopo kwenye tango? 

Ni asilimia 95 ya tango zima.

2. Urembo

Ni tunda lenye faida kubwa kwa urembo.

Umuhimu huu hutokana na uwepo wa vitamini A, vitamini C, silica na Sulfur ambavyo huhitajika kuboresha afya ya ngozi, kucha na nywele.

Ni tunda ambalo halipaswi kukosa ndani kwa mtu yeyote anayependa urembo.

3. Kisukari

Uwepo wa cucurbitacins huhusishwa na sifa ya kuongeza ufanisi wa vimeng’enya vya insulin kwenye kudhibiti ongezeko la sukari mwilini.

Kwenye orodha ya vyakula vyenye kiasi kidogo cha sukari, tango pia lipo.

Nyuzilishe zinazopatikana kwenye tango huwa na faida kubwa hasa kwa watu wenye aina ya pili ya kisukari. (1,2)

Una kisukari, au unataka kujikinga na ugonjwa huu? Tumia tango.

4. Saratani

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, mwaka 2018 kulikuwa na visa vipya milioni 18.1 vya saratani duniani na wastani wa vifo milioni 9.5.

Mwaka 2040 idadi ya visa vipya inatazamiwa kufikia milioni 29.5 na huku vifo vikifikia milioni 16.4 kwa mwaka.

Virutubisho vya cucurbitacin vimebainishwa kuwa na uwezo wa kupambana na saratani, pamoja na kuzuia ukuaji wake. (3)

Aidha, tafiti kadhaa zinafafanua uwezo wa nyuzilishe kwenye kupambana na saratani ya utumbo mkubwa. (4,5)

Vyote hivi utavipata kwenye tango.

5. Uvimbe

Tango hupoozesha kemikali na taarifa za mwili zinazosababisha kutokea kwa uvimbe.

Sukari zake zenye asili ya protini zinazoitwa idoBR1 ndiyo hutajwa kuhusika moja kwa moja katika kufanikisha kazi hii. (6)

Uvimbe unaoanzia ndani ya mwili huwa na athari hasi kwa afya.

Huufanya mwili utengeneze taarifa mbaya ambazo hufanya baadhi ya viungo vyake vianze kushambuliwa.

Uvimbe sugu hurahisisha kutokea kwa magonjwa kama kisukari, magonjwa ya moyo, saratani na baridi yabisi.

Jikinge na magonjwa haya kwa kula matango.

6. Moyo

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2019 magonjwa yanayohusishwa na mfumo wa damu na moyo yalichukua asilimia 32 ya vifo vyote vilivyotokea duniani.

Tango huwa na mjumuisho wa vitu vinne venye faida kubwa kwa mifumo husika. Huwa na magnesium, potassium, cucurbitacins na nyuzilishe.

Vyote hivi vimethibitishwa na tafiti kuwa na uwezo wa kulinda mfumo wa mzunguko wa damu na moyo.

7. Mifupa

Madini ya calcium na vitamini K hufanya kazi kwa pamoja katika kuimarisha afya ya mifupa.

Aidha, vitamini K huhusika pia katika kuratibu mfumo wa kuganda kwa damu mwilini baada ya kupatwa na jeraha.

Ulaji wa tango utakupa uhakika wa kupata virutubisho hivi muhimu kwenye kuongeza uimara na ujazo wa mifupa pamoja na kuganda kwa damu.

8. Mfumo wa Chakula

Tango huwa na kiasi kikubwa cha nyuzilishe na maji.

Husaidia kuboresha mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, kuongeza idadi ya bakteria wazuri tumboni pamoja na kuondoa tatizo la choo kigumu.

9. Uzito

Kuna faida mbili za kula tango.

Kwanza, husaidia kulinda uzito wa mwili ili usiongezeke kupita kiasi.

Pili, husaidia kupunguza uzito kwa watu wenye changamoto ya kuwa na uzito uliozidi kiasi.

Ili uweze kutunza vizuri uzito wako, au ili uzito huo uweze kupungua, ni lazima nishati unayoingiza mwilini iwe ndogo kiasi, au ilingane na uhitaji wa nishati ya mwili mzima.

Tango ni tunda lenye nishati ndogo sana.

Tango moja huwa na wastani wa calories 45 tu huku gramu 100 za unga wa mahindi zikiwa na calories zaidi ya 360.

Tafiti zinabainisha kuwa ulaji wa vyakula vyenye kiasi kikubwa cha maji na nishati ndogo husaidia kupunguza uzito wa mwili. (7,8)

10. Sumu

Kujaa kwa sumu mwilini ni mojawapo ya vyanzo vya kuongezeka kwa vifo vya mapema duniani.

Sumu hizi huua seli za mwili ambazo ni kitovu cha uhai.

Aidha, sumu hizi ni chanzo cha magonjwa sugu ya moyo na mfumo wa damu, kisukari, saratani na kiharusi.

Tango huwa na mjumuiko wa viondoa sumu vingi hivyo linafaa sana kwa afya yako.

Muhtasari

Hauna kisingizio chochote cha kukufanya usinunue tunda hili.

Kama haulipendi kwa ladha yake basi walau lipende kwa faida zake kwa afya.

Ni rafiki yako mzuri.

Share This Article