Limao: Virutubisho na Faida kwa Binadamu

6 Min Read

Limao au ndimu ni tunda linalotumika kwa kazi nyingi.

Tunda hili linalopatikana kirahisi karibia kila sehemu ya dunia huwa na virutubisho vingi vyenye umuhimu mkubwa kwa afya.

Virutubisho

Kwa mujibu wa Idara ya Chakula ya Marekani (USDA), kwenye kila gramu 100 za limao au ndimu, asilimia 89 ya uzito wake huwa ni maji.

Huwa pia na nishati, protini, wanga, nyuzilishe, madini ya calcium, magnesium, phosphorus, potassium, sodium, zinc, copper, selenium na kiasi kidogo cha sukari.

Aidha, huwa na vitamini C, citric acid, vitamini B12, folate pamoja na viondoa sumu vya carotene, vitamini E, lutein na zeaxanthin.

Mjumuiko wa virutubisho hivi huleta faida zifuatazo kwa afya;

1. Huongeza Damu

Madini ya chuma huhitajika kwenye kutengeneza damu mwilini.

Unaweza kuyapata kupitia mlo au kwa kutumia virutubisho na dawa zenye madini haya.

Ili mwili uweze kufyonza vizuri madini ya chuma kutoka kwenye vyakula, vitamini C na citric acid huhitajika ili kurahisisha zoezi hilo.

Ni wazi ule msemo wa kuwa limao hupunguza damu siyo sahihi, upuuze. (1,2)

Tunda hili huusaidia mwili kutengeneza damu.

2. Saratani

Kemikali za D-limonene zinazopatikana kwenye limao huhusisishwa na kuzuia pamoja na kupambana na aina mbalimbali za saratani mwilini.

Utafiti mmoja unaonesha kuwa kemikali hii inaweza kuingilia taarifa za ukuaji wa seli za saratani ya mapafu kwa kuzifanya zijidhuru na kujiua zenyewe. (3)

Aina zingine pia za saratani zinaweza kudhibitiwa na ulaji wa tunda hili.

3. Kinga

Mwili huwa na askari wake wanaosaidia kwenye kuulinda kila siku, mchana na usiku. Askari hawa hupaswa kuwa tayari muda wote kukabiliana na mashambulizi ya vimelea vya magonjwa.

Kwa kuwa hufanya kazi hii pasipo kupumzika, ni lazima nguvu ya ziada itumike kwenye kuwapatia msaada wa nguvu za ziada.

Limao ni tunda lenye zinc na vitamini C nyingi ambayo hutumiwa na mifumo ya mwili katika kuimarisha kinga yake kwenye kupambana na magonjwa. (4,5)

Ongeza kinga ya mwili wako kwa kutumia limao au ndimu.

4. Kiharusi

Vyakula vyenye kiasi kikubwa cha flavonoids huwa na sifa kubwa ya kuukinga mwili dhidi ya shambulio la kiharusi.

Ugonjwa huu unaosababishwa na kuganda kwa damu, au kupasuka kwa mishipa ya damu husababisha kupooza kwa mwili.

Hufanya hivyo kwa kuzuia shinikizo la juu la damu, kuimarisha mishipa ya damu pamoja na kuzuia kuganda kwa damu kwenye mishipa yake. (6,7)

Husaidia pia kwenye kupambana na magonjwa ya mfumo wa damu na moyo.

5. Presha

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), walau watu bilioni 1.28 wanakabiliwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.

Watu hawa wana wastani wa umri kati ya miaka 30-79.

Baadhi ya tafiti zinaelezea uwezo wa limao kwenye kuzuia ongezeko la shinikizo la damu mwilini.

Hata hivyo, tafiti nyingi zaidi zinahitajika kufafanua zaidi madai haya.

6. Uzito

Kuna nadharia nyingi mtaani zinazoelezea uwezo wa limao kwenye kupunguza uzito wa mwili.

Hata hivyo, ni ukweli kuwa hakuna tafiti pamoja na majaribio mengi yaliyofanyika kwa binadamu kuthibitisha madai haya. (8)

Ili madai haya yaweze kupata mashiko kisayansi ni lazima tafiti za ziada zifanyike ili kuweka sawa taarifa hizi.

7. Ini

Ini la binadamu hufanya kazi zaidi ya 500 mwilini.

Aina mbalimbali za vimelea vya magonjwa hasa virusi pamoja na baadhi ya vinywaji mfano pombe husababisha kuharibika kwa kiungo hili muhimu kwa afya ya binadamu.

Utafiti uliofanyika kwenye panya unaonesha kuwa juisi ya limao inaweza kutibu athari za ini lililoharibiwa kwa pombe. (9)

Faida hii inaweza kuwa ipo pia kwa binadamu.

8. Figo

Figo ni mashine za mwili zinazochuja damu na kutengeneza mkojo.

Zikiharibika hufanya mhusika augue ugonjwa wa figo ambao usipopata tiba sahihi kwa haraka, huwa sugu na kufanya mhusika aishi kwa kutegemea mashine ya nje ya kufanya kazi za figo.

Hatua hii ni mbaya, hatari na huongeza uwezekano wa kupoteza maisha ya mgonjwa.

Changamoto nyingine ya viungo hivi ni kutengenezwa kwa mawe ndani yake ambayo huathiri ufanisi wa kazi zake, na kuongeza uwezekano wa kuugua ugonjwa wa figo.

Kemikali za citric acid na lemonade zimebainishwa na tafiti kuwa na uwezo wa kuzuia utengenezwaji wa mawe kwenye figo. (10,11)

Linda figo zako kwa kunywa juisi ya limao.

9. Kisukari

Aina kuu ya nyuzilishe zinazopatikana kwenye limao huitwa pectin.

Miongoni wa faida za pectin ni kuboresha mfumo wa chakula na kupunguza matumizi ya sukari na wanga mwilini.

Ni tunda zuri sana kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari.

Hata hivyo, ili uipate pectin hii inafaa ule sehemu nyeupe ya tunda hili inayofuata baada ya magada yake ya nje.

10. Urembo

Pengine umewahi kuona aina nyingi za lotion, mafuta au sabuni zilizo na kipeperushi kinachoonesha kuwa zimetengenezwa kwa kutumia limao au ndimu.

Hawakuwa wanakudangaya.

Hutumika kuboresha afya ya ngozi kwa kuongeza mng’ao wake, kuponya majeraha na makovu pamoja na kuondoa chunusi. (12)

Endeleza urembo wako sasa kwa kutumia limao.

Muhtasari

Unawezaje kula nyama choma pasipo kuongeza limao au ndimu ili ikuongezee ladha?

Ni wazi kuwa ukiondoa faida zake kwa afya, limao ni tunda pendwa katika kuongeza ladha ya vyakula.

Tumetumia maneno limao na ndimu kwa pamoja kwa kuwa vyote hufanya kazi sawa.

Share This Article