Kazi za Damu Kwenye Mwili wa Binadamu

5 Min Read

Damu ni kimiminika chenye muunganiko wa vitu vinne ambavyo ni plasma, chembe nyekundu, chembe nyeupe pamoja na chembe sahani.

Kila sehemu ya muunganiko huu huwa na kazi yake maalum.

Plasma

Hii ndio sehemu kubwa inayotengeneza kiminimika cha damu. Huchukua walau asilimia 55 ya kiasi chote cha damu.

Huundwa kwa maji, sukari, mafuta na chumvi chumvi.

Hufanya kazi ya kusafirisha seli, virutubisho, kinga mwili, uchafu, protini za kugandisha damu, vichocheo vya mwili pamoja na aina zingine za protini zinazosaidia kuweka uwiano sawa wa vimiminika vya mwili kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Husaidia pia kwenye kulinda na kutunza joto sawa la mwili.

Chembe Nyekundu

Karibia asilimia 40 ya damu yote mwilini hufanywa kwa chembe nyekundu.

Ndio hufanya damu ionekane ikiwa na rangi nyekundu kutokana na uwepo wa protini inayoitwa hemoglobin ndani yake.

Huwa na umbo la mduara uliobonyezeka katikati.

Kiasi cha kawaida cha chembe nyekundu za damu kwenye kila microlita ya damu ni seli milioni 4.7- 6.1 kwa wanaume, milioni 4.2-5.4 kwa wanawake na milioni 4.0-5.5 kwa watoto.

Hufanya kazi ya kubeba hewa safi ya oxygen kutoka kwenye mapafu kwenda sehemu zingine za mwili pamoja na kurudisha hewa ya carbondioxide kwenye mapafu ili iweze kutolewa nje kupitia upuamuaji wa kawaida.

Huwa na wastani wa siku 120 pekee za kuishi, na baada ya hapo hufa na kutolewa nje kupitia ini na wengu.

Chembe Nyeupe

Hufanya kubwa ya kuulinda mwili dhidi ya aina mbalimbali za maambukizi ya magonjwa.

Zipo chache sana mwilini, huchukua walau asilimia 1 tu ya kiasi chote cha damu.

Kiasi cha kawaida cha chembe nyeupe za damu kwenye kila microlita ya damu ni seli 4000-10,000. (2)

Chembe nyeupe za damu hugawanyika kwenye makundi yafuatayo;

  • Granulocytes (neutrophils, eosinophils na basophils)
  • Monocytes
  • Lymphocytes (T seli na B seli)

Neutrophils

huchukua zaidi ya nusu ya kiasi chote cha chembe nyeupe za damu.

Ni seli za kwanza kabisa ambazo hutambua uwepo wa hatari hasa baada ya kushambuliwa na virusi au bakteria.

Huzipa pia taarifa aina zingine za chembe nyeupe za damu juu ya uwepo wa mashambulizi, hivyo kuzifanya zije kushirikiana kwenye kuulinda mwili. Ni aina ya seli inayopatikana kwenye usaha.

Muda wake wa kuishi huwa ni masaa 8 tu hivyo ni lazima mwili uzalishe seli hizi kila siku.

Wastani wa neutrophils bilioni 1 huzalishwa kila siku.

Eosinophils

Huhusika pia katika ulinzi wa mwili hasa kwenye kupambana na bakteria na minyoo.

Zinafahamika zaidi katika kuufanya mwili uitikie mzio.

Huchukua walau asilimia 5 tu ya kiasi chote cha chembe nyeupe za damu.

Basophils

Huchukua walau asilimia 1 tu ya kiasi chote cha chembe nyeupe za damu.

Huhusika wakati wa mzio na katika nyakati ambazo pumu inakuwa imeamshwa.

Hufanya kazi ya kuamsha msisimko wa uvimbe pamoja na kubana njia za mfumo wa hewa.

Lymphocytes

Huwepo za aina mbili;

Seli B, huhusika na ulinzi wa mwili unaohusisha mfumo wa kinga mwili. Huzifanya kinga mwili zikumbuke aina husika za maradhi au vimelea, ili ikitokea kwa baadae tena vimetokea iwe rahisi kukumbuka na kupambana navyo.

Seli T, huhusika katika ulinzi wa mwili kwa kushambulia aina mahsusi ya vimelea vya maradhi. Hukumbuka vimelea vyote ili ikitokea vimeingia mwilini kwa mara nyingine ziweze kuvishambulia kirahisi.

    Monocytes

    Hufanya kazi ya kukusanya uchafu wote unaotengenezwa na mfumo wa kinga za mwili.

    Walau asilimia 5-12 ya kiasi chote cha chembe nyeupe za damu ni monocytes.

    Kazi yake kuu ni kusafisha na kuondoa seli mfu mwilini.

    Chembe Sahani

    Tofauti na chembe nyekundu au nyeupe za damu, chembe sahani sio seli kamili bali ni vipande vya seli. Hujikusanya kwenye sehemu ya jeraha na kuifanya damu igande kwenye eneo husika

    Kiasi cha kawaida cha chembe sahani ni 150,000-450,000 kwa kila microlita ya damu.

    Zikiwa chini ya 150,000 hufanya damu ikawie kuganda hivyo kuongeza uwezekano wa kupoteza damu nyingi kutokana na ajali, pamoja na kuishiwa damu mara kwa mara.

    Ikitokea zimekuwa nyingi zaidi ya 450,000 husababisha damu iwe inaganda mwilini bila sababu pamoja na kuongeza uwezekano wa kuugua magonjwa mbalimbali hasa kiharusi.

    Aidha, inaweza pia kusababisha uchovu mwingi, kuvuja damu puani pamoja na kujisaidia choo chenye damu.

    Muhtasari

    Pamoja na kukua kwa sayansi ya afya na tiba shirikishi, dunia bado haijaweza kuzalisha damu mbadala zaidi ya ile inayotokana na mwili wa binadamu.

    Wanawake wanaojifungua, watoto wachanga, watu wanaofanyiwa upasuaji pamoja na majeruhi wa ajali ndiyo hutumia kiasi kikubwa cha damu.

    Changia damu kuokoa uhai.

    Share This Article