Mwili wa binadamu hauwezi kuzalisha wala kuhifadhi vitamini C kwa ajili ya matumizi ya baadae.
Unajua sababu ni nini? Hii ni vitamini inayounganika na maji, haiunganiki na mafuta. Mwili wa binadamu huhifadhi vitamini na virutubisho vyenye sifa ya kuungana na mafuta na siyo maji.
Kwa maana hii, binadamu huhitaji kuipata kila siku kupitia vyakula na virutubisho.
Vyanzo
Vitamini hii unaweza pia kuiita ascorbc acid.
Mboga za majani na matunda ni vyanzo bora sana vya vitamini C.
Mfano ni matunda yenye uchachu hasa limao, ndimu na machungwa, broccoli, kabichi, nyanya pamoja na mapera.
Aidha, inaweza kupatikana kutoka kwenye virutubisho maalumu vinavyouzwa madukani ambavyo hutengenezwa au kuongezewa vitamini hii.
Mahitaji kwa Siku
Watoto wenye umri wa miezi 0-6 hupaswa kutumia walau 40 mg za vitamini C kila siku.
Uhitaji huu huongezeka kadri ya umri wa mhusika.
Kwa ujumla wake, mwanamme mwenye umri wa miaka 19 na kuendelea anapaswa kutumia 90 mg kwa siku huku wanawake wenye umri huo wakishauriwa kutumia kiasi cha 75 mg kwa siku.
Hii ni kwa mujibu wa taasisi ya afya ya NIH. Uhitaji huu huongezeka zaidi wakati wa ujauzito na kunyonyesha.
Kazi Zake
Ndiyo kiini cha uponyaji wa vidonda na majeraha ya mwili. Huhitajika sana kwa kazi hii. (1,2)
Ili mwili wa binadamu uweze kufyonza na kutumia vizuri madini ya chuma ambayo huhitajika kwenye kutengeneza na kusafirisha damu, ni lazima uwe na kiasi cha kutosha cha vitamini C.
Husaidia kupambana na changamoto ya upungufu wa damu. (3)
Vitamini C husaidia pia katika kuukinga mwili dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na magonjwa sugu kama kisukari, presha, saratani na magonjwa ya moyo.
Hufanya hivyo kwa kuboresha na kuimarisha mfumo wa kinga za mwili pamoja na kuharibu au kuua sumu chochezi. (4,5,6)
Umewahi kusikia ugonjwa wa gauti?
Vitamini C huusaidia mwili kwenye kupunguza kiasi cha uric acid kilichopo kwenye damu ambayo ndiyo husababisha kutokea kwa ugonjwa huu.
Aidha, ni mojawapo ya virutubisho vinavyoweza kutumika katika kujikinga na ugonjwa huu. (7)
Hulinda seli za mwili ambazo ndiyo kitovu cha uhai, ni muhimu kwa afya ya ngozi, mishipa ya damu, mifupa na gegedu, huboresha afya ya macho pamoja na kutibu mafua. (8,9)
Ni vitamini muhimu sana kwa afya yako.
Upungufu
Unaweza kusababisha kuvimba kwa maungio ya mwili, kudhoofika kwa mifupa, ukavu wa ngozi, uchovu, upungufu wa damu pamoja na kuugua mara kwa mara kutokana na kupungua kwa kinga ya mwili. (11,12)
Changamoto nyingine kubwa ya upungufu wa vitamini C ni kuvuja kwa damu kwenye sehemu za wazi za mwili, matatizo ya meno, kuishiwa na pumzi pamoja na uchovu usio wa kawaida.
Ikiwa changamoto hizi hazita shughulikiwa mapema, mhusika anaweza kupoteza maisha.
Kwa lugha ya kitaalamu huitwa kiseyeye. (13)
Tatizo hili linaweza kutokea kwa kila mtu lakini zaidi kwa jamii ambazo hazitumii kabisa matunda na mboga za majani.
Muhtasari
Unakumbuka ile siku uliyokula machungwa mengi jinsi ambavyo tumbo lako lilianza kuunguruma, kujaa gesi au kuhara?
Hizo ni dalili za kuwa umetumia kiasi kikubwa cha vitamini C kuliko kile ambacho mwili wako unahitaji kila siku.
Haina madhara kwa afya, jitahidi usile mengi sana wakati mwingine.