Tampon: Matumizi, usalama na ushauri

3 Min Read

Tampon hufyonza damu ikiwa ndani ya tundu la uke.

Bidhaa hii hutengenezwa kwa kutumia pamba, rayon au mjumuiko wa vyote kwa pamoja.

Usalama

Kifyonza damu kilichohifadhiwa kwenye tampon zinazouzwa mitaani hutengenezwa kwa utaratibu usio ruhusu uingizwaji wa sumu za chlorine ambazo ni hatari kwa afya ya mtumiaji pamoja na mazingira, hivyo ni salama.

Baadhi ya tampon hizi huwa na harufu au hufungwa na deodorant ndani yake ili kukata harufu.

Mwanamke atakayeamua kutumia aina hii ya tampon anapaswa kuwa makini kwani nyingi husababisha miwasho na mzio.

Muundo

Tampon inaweza kuja pamoja na kifaa saidizi kinachotumika kuizamishia ukeni ambacho mara nyingi huwa cha plastiki au inaweza kuja bila kifaa hiki, hivyo mhusika hupaswa kutumia vidole vyake kuisukuma ndani.

Zote hizi zipo vizuri, hazina tofauti.

Kama tampon husika haina kifaa cha kuiingizia ukeni, lazima mhusika asafishe vidole vyake kwanza ili kutunza usafi.

Huwa na kamba ndogo ambayo hubaki nje ikining’inia ambayo ndiyo hutumika katika kuivuta wakati wa kubadilisha na hupaswa kubadilishwa kila baada ya saa 4-8.

Tahadhari

Tofauti na jinsi ilivyo kwa taulo za kike, tampon huwa haionekani hivyo mhusika anaweza kujisahau.

Hali hii inaweza kusababisha kuvujia kwa damu kwenye nguo za ndani au hata nguo za nje.

Ikiwa wakati wa kubadili kifaa hiki utafika na usikione, hauna haja ya kupata wasiwasi.

Tampon hii bado ipo ndani, upo salama.

Ingiza vidole vyako taratibu uiondoe, japo inaweza kuchukua muda kidogo kwa kuwa pengine kamba yake itakuwa imelowa na kugandishwa na damu.

Baadhi ya wanawake hupata wasiwasi kuwa tampon inaweza kupotelea ukeni, jambo hili haliwezekani. Uke huitunza tampon hii kwenye sehemu sahihi na shingo ya mlango wa kizazi huwa ni ndogo sana kuruhusu tampon ipite na kupotelea ndani.

Ushauri

Ni vizuri kubadili tampon mara kwa mara, pia siyo salama kulala nayo usiku kucha.

Tampon iliyoachwa muda mrefu ndani ya uke haiwezi kupotea, bali inaweza kusababisha kuvujia kwa damu kwenye nguo za ndani, harufu kali na mbaya pamoja na maambukizi makali sana kwenye damu.

Dalili za uwepo wa maambukizi hayo ni kiungulia na kutapika, homa kali, kuhara, kizunguzungu, kuwewezeka pamoja na kifafa. Ni muhimu kuwa makini.

Share This Article