Hedhi ni tendo la asili na kibaiolojia analopitia mwanamke kila mwezi.
Chanzo kikubwa cha maumivu ya hedhi ni kujivuta kwa misuli ya kuta za mji wa uzazi kutokana na uwepo wa kiasi kikubwa cha vichocheo vya prostaglandin.
Kadri kuta za mji wa uzazi zinavyozidi kujivuta kwa kiwango kikubwa, ndivyo mishipa inayosambaza damu kwenye misuli husika inavyozidi kubinywa.
Matokeo yake huwa ni kukosekana kwa damu na hewa ya kutosha kwenye misuli ya kuta za mji wa uzazi ambayo huathirika kwa kiasi kikubwa hivyo kusababisha maumivu.
Maumivu ya hedhi yamegawanywa katika makundi mawili yaani maumivu ya hedhi kundi la kwanza na maumivu ya hedhi kundi la pili.
Kundi 1
Haya ni maumivu ya asili yasiyosababishwa na uwepo wa tatizo lolote kiafya.
Mara nyingi huanza siku 1-2 kabla ya hedhi na yanaweza kuendelea hadi pale hedhi itakapofikia ukomo kwa mwezi husika. Huonekana zaidi sehemu ya chini ya tumbo na kiuno, mgongoni pamoja na sehemu za nyonga.
Maumivu haya yanaweza kuambatana na shida ya kuharisha, kichefuchefu, kutapika pamoja na uchovu mkubwa.
Katika hali ya kawaida, maumivu ya aina hii huendelea kupungua kadri umri wa mwanamke unavyozidi kuongezeka na yanaweza kukoma kabisa baada tu ya mwanamke husika kupata mtoto.
Kundi 2
Haya ni maumivu yanayosababishwa na uwepo wa matatizo mengine kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamke mfano uvimbe wa aina yoyote ile, au pia uwepo wa aina fulani ya maambukizi.
Maumivu haya hudumu kwa muda mrefu zaidi tofauti na yale ya kundi la kwanza, na huendelea kuongezeka ukubwa kadri umri wa mwanamke unavyozidi kusogea.
Tiba
Changamoto hizi mbili kwa pamoja zinaweza kupunguzwa au hata kuondolewa kabisa kwa kutumia dawa za kuondoa maumivu jamii ya NSAID’s mfano ibuprofen, naproxen na mefenamic acid.
Ni lazima kwanza upate ushauri wa daktari au mfamasia kabla ya kuzitumia.
Hata hivyo, kuna baadhi ya njia mbadala zinazoweza kutumika katika kupunguza au hata kuondoa kabisa maumivu ya hedhi.
Njia hizo ni kujikandia maji ya moto ya wastani wa 104 degree F (40 degree C) sehemu ya chini ya tumbo, nyonga, kiuno na mgongo.
Kufanya massage tumboni kwa kutumia mafuta ya mimea, kuacha au kupunguza matumizi ya vyakula vinavyojaza gesi na kubakiza maji mengi hasa vile vyenye mafuta mengi na pombe.
Matumizi ya chai za mitishamba hasa tangawizi, mdalasini na binzari manjano. Pia kufanya mazoezi mara kwa mara na kuongeza matumizi ya virutubisho vyenye madini ya zinc na magnesium inaweza kusaidia.
Muhtasari
Maumivu ya hedhi kwa mwanamke ni jambo la kawaida.
Kitu pekee kinachopaswa kuleta wasiwasi ni ukubwa wa maumivu.
Ikiwa mwanamke anapata maumivu makali sana anapaswa kufika hospitalini kwa uchunguzi zaidi