Malaria: Dalili, Kinga na Matibabu

4 Min Read

Malaria ni ugonjwa hatari.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2020 ugonjwa huu uliathiri zaidi ya watu milioni 241 duniani, huku watu 627000 wakipoteza uhai.

Bara la Afrika ndilo hubeba mzigo mkubwa wa ugonjwa huu kwa kuchukua asilimia 95 ya wagonjwa na asilimia 96 ya vifo vyote duniani. (1)

Vimelea Vyake

Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vinavyoitwa Plasmodium ambavyo husambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia mbu jike aitwaye Anopheles.

Kuna aina kuu 5 za vimelea vya plasmodium ambavyo ni;

  • Plasmodium falciparum
  • Plasmodium vivax
  • Plasmodium ovale
  • Plasmodium malariae
  • Plasmodium knowlesi.

Vifo vingi vya binadamu husababishwa na P. falciparum.

Aidha, kwakuwa vimelea vya ugonjwa huu hujishikiza kwenye chembechembe nyekundu za damu, mtu anaweza pia kuupata ugonjwa huu kwa kupokea damu, upandikizwaji wa viungo au kwa kushirikiana vitu vyenye ncha kali hasa sindano zilizo na mabaki ya damu ya mgonjwa.

Aidha, Vimelea vya P. falciparum na P. vivax ndiyo hatari zaidi.

Dalili

Huanza kuonekana kati ya siku 10-15 tangu kuingia mwilini kwa vimelea vyake.

Vimelea hivi vinaweza pia kukaa mwilini kwa muda mrefu pasipo kuonesha dalili yoyote.

Hata hivyo, dalili za malaria ni kutetemeka kwa mwili, kuhara, homa kali, kutokwa na jasho, maumivu ya kichwa, kichefuchefu na kutapika.

Dalili zingine za ugonjwa huu ni kupungukiwa na damu, maumivu kwenye maungio ya mifupa, manjano, kuvimba kwa ini  pamoja na kujisaidia choo chenye damu. (2)

Maambukizi ya vimelea vya P. falciparum huenda mbali zaidi kwa kuathiri ubongo, kushusha sukari, kujaa kwa maji kwenye mapafu, kuvimba kwa mirija ya damu, kupoozesha viungo vya ndani ya mwili hasa ini na figo, kuzimia pamoja na degedege.

Athari hizi hutokea ndani ya muda mfupi sana. Mgonjwa anaweza kupoteza maisha ndani ya saa 24 ikiwa msaada wa matibabu ya haraka hautatolewa.

Makundi Hatari

Watoto chini ya umri wa miaka 5, wanawake wajawazito, watu wenye VVU pamoja na wale wanao hamia kwenye maeneo yenye maambukizi makubwa huwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kuathiriwa na ugonjwa huu kuliko wengine.

Ni muhimu wakilindwa kwa umakini mkubwa. Daktari atauliza maswali kadhaa. Ili kuthibitisha uwepo wa ugonjwa huu, uchunguzi wa njia ya hadubini utafanyika. 

Kipimo cha haraka kinaweza pia kufanyika ambacho hutoa majibu ndani ya muda mfupi.

Tiba

Mwongozo wa sasa kuhusu matibabu ya ugonjwa wa malaria nchini Tanzania unasisitiza matumizi ya dawa za Artemether lumefantrine (ALU) maarufu zaidi kama dawa mseto kama chaguo la kwanza.

Vidonge vya dihydroartemisinin piperaquine au sindano za artesunate na artemether zinaweza pia kutumika.

Hata hivyo, kuna dawa nyingi za kutibu ugonjwa wa malaria.

Kila nchi huweka utaratibu wake katika kushughulikia ugonjwa huu.

Kinga

Kuna namna tatu za kujikinga na ugonjwa huu

  • Kudhibiti vimelea kwa kutumia viuatilifu pamoja na kutumia neti
  • Matumizi ya dawa za kinga. Mfano ni unywaji wa SP kwa wanawake wajawazito
  • Kupitia chanjo ya malaria inayoitwa RTS,S/AS01 ambayo iligunduliwa mwaka 2021.

Muhtasari

Wastani wa kifo cha mtoto mmoja hutokea kila baada ya dakika 2 kwenye bara la Afrika kutokana na ugonjwa wa malaria. (3)

Kwa takwimu za dunia nzima, wastani wa watoto 750 wenye umri chini ya miaka 5 hufariki kila siku.

Malaria inazuilika. Tujikinge.

Share This Article