Karanga: Virutubisho, Faida na Tahadhari kwa Afya

4 Min Read

Karanga ni zao linalopatikana kwa wingi karibia kila sehemu ya dunia.

Ukiondoa faida za kibiashara, karanga hutoa mchango mkubwa katika kuboresha afya ya binadamu.

Virutubisho

Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), karanga huwa na protini, mafuta mazuri, nishati, nyuzi lishe, madini chuma, calcium, magnesium, potassium, zinc na phosphorus.

Aidha, huwa na asidi ya mafuta ya omega 3 na 6, selenium, aina nyingi za vitamini pamoja na kemikali mbalimbali.

Karanga huwa na faida zifuatazo kwa afya;

1. Wanaume

Karanga huwa na kampaundi za resveratrol ambazo huongeza ubora wa afya ya uzazi.

Baadhi ya tafiti huihusisha kampaundi hii na uwezo wa kuboresha mbegu za kiume pamoja na kutibu changamoto ya upungufu wa nguvu za kiume. (1,2,3)

Huwa pia na amino acids zinazofahamika kwa jina la l-arginine ambazo hubadilishwa kuwa nitric oxide zikiwa ndani ya mwili.

Hupanua mishipa ya damu, huongeza hamu ya kushiriki tendo la ndoa, huongeza ubora wa mbegu za kiume pamoja na kuongeza uzalishwaji wa vichocheo vya kiume, yaani testosterone. (4,5)

Tatua changamoto za uzazi kwa kutumia karanga.

2. Moyo

Huongeza kiasi cha mafuta mazuri mwilini ambayo huwa na faida kubwa kwenye afya ya moyo.

Ni chakula kizuri kwenye kulinda moyo pamoja na kuzuia magonjwa mbalimbali ambayo huathiri kiungo hiki muhimu kwa uhai. (6,7)

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wastani wa watu milioni 19.7 hufariki kila mwaka duniani kutokana na magonjwa ya moyo.

Takwimu hizi zinatisha, chukua tahadhari.

3. Uzito

Karanga ni chakula kizuri kwa watu wanaotaka kutunza uzito wa mwili, pamoja na wale wanaotaka kupunguza uzito wao.

Tafiti nyingi za afya zinabainisha kuwa ulaji wa karanga hauongezi uzito wa mwili, bali hutengenezea mazingira rafiki ambayo hufanya uzito wake usiongezeke kupita kiasi. (8,9)

Hutaki kitambi? Tumia karanga

4. Sukari

Karanga ni chakula chenye kiwango kidogo cha sukari na wanga.

Huwa pia na kiwango kikubwa cha protini, nyuzi lishe pamoja na mafuta mazuri. (10,11)

Hufaa sana kwa watu wenye changamoto ya ugonjwa wa kisukari.

5. Sumu

Sumu huathiri seli za mwili wa binadamu.

Ni chanzo cha magonjwa makubwa hasa kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo pamoja na aina mbalimbali za saratani.

Baadhi ya viondoa sumu vinavyopatikana kwenye karanga ni coumaric acid, resveratrol, phytic acid na vitamini E. (12)

Ni chakula bora katika kuondoa na kuharibu sumu za mwili.

6. Figo

Umewahi kusikia kuhusu tatizo la mawe kwenye figo?

Karanga husaidia kwenye kulinda afya ya figo pamoja na kuzuia kutokutokea kwa tatizo hili.

Figo ndio mashine ya mwili inayochuja damu. Ilinde.

7. Ujauzito

Ukuaji bora wa mtoto tumboni hutegemea uwepo wa mambo mengi.

Mojawapo ya virutubisho muhimu ni foliki asidi ambayo huhitajika ili kuzuia tatizo la mgongo wazi kwa mtoto.

Karanga ni chanzo kizuri cha vitamini B9 au foliki asidi. Huusaidia pia mwili kwenye kutengeneza chembechembe mpya za damu pamoja na kulinda vinasaba vya taarifa za urithi.

Tahadhari

Baadhi watu hasa watoto huwa na mzio wa karanga. Mzio huu unaweza pia kutokea kwa watu wazima.

Huambatana na dalili za kuhara, maumivu makali ya tumbo, kiungulia na kutapika, wekundu wa ngozi pamoja na kuvimba kwa midomo.

Kama huwa unaonesha dalili hizi baada ya kutumia karanga unapaswa kufika hospitalini kwa uchunguzi na matibabu.

Share This Article