Tendo la Ndoa Wakati wa Ujauzito, Faida na Tahadhari kwa Afya

4 Min Read

Ni salama kushiriki tendo la ndoa wakati wa ujauzito? Ndio.

Ni salama kabisa kushiriki tendo la ndoa wakati wote wa ujauzito kama hakuna sababu zozote hatarishi kwa afya ya mama na mtoto.

Pamoja na ukweli huu, ni wazi kuwa watu wengi huogopa kushiriki tendo hili.

Katika utafiti mmoja, asilimia 80 ya wanaume walionesha wasiwasi wao pamoja na uoga wa kushiriki tendo hili kwa kudhani kuwa kurupushani zake humuumiza mtoto. (1)

Baadhi ya jamii pia huamini kuwa tendi hili ni hatarishi kwa kuwa linaweza kuharibu ujauzito, kuleta maambukizi kwa mtoto, kufanya mji wa mimba upasuke pamoja na kusababisha maambukizi kwa mama. (2)

Msimamo wa wanawake upoje?

Wengi huwa ni waoga pia. Hudhani kuwa tendo hili ni hatari kwao. (3,4)

Tutachambua mambo haya kwa undani, twende pamoja.

Mwongozo

Tendo la ndoa ni salama kabisa kufanyika wakati wa ujauzito.

Mtoto hulindwa na kuta imara zisizo ruhusu mbegu za kiume kuigia ndani yake. Kwa ujumla wake, tendo la ndoa haliwezi kuathiri afya ya mama pamoja na mtoto kwa namna yoyote ile. (5,6)

Ni tendo salama.

Hatari

Tendo hili linaweza kufanyika muda wote wa ujauzito isipokuwa katika mazingira yanayoleta wasiwasi juu ya uwepo wa usalama wa kutosha kwa mama, au mtoto.

Ikiwa mama ataonesha dalili hizi, tendo la ndoa linapaswa kusitishwa haraka;

  • Kufunguka kwa mlango wa kizazi
  • Kuvuja kwa damu au maji ya uzazi
  • Matatizo kwenye kondo la uzazi
  • Uwepo wa maambukizi ya magonjwa ya zinaa
  • Kuvunjika kwa chupa ya uzazi
  • Kuwa na historia ya kuharibika kwa ujauzito wa awali, au kupata uchungu wa kuzaa kabla ya wakati

Mambo haya yanapaswa kutumiwa kama taa nyekundu, ishara ya kuwa kuna baadhi ya mambo hayapo sawa. (7)

Mama anapaswa kufika hospitalini haraka ikiwa ataonesha dalili yoyote mbaya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.

Daktari atachukua historia ya changamoto husika pamoja na kushauri mambo kadhaa ya kufanya.

Baadhi ya dawa za homoni hutolewa pamoja na kumshauri mama mjamzito apate muda mwingi wa kupumzika pasipo kufanya kazi na kushiriki tendo la ndoa. (8,9)

Mambo haya yanapaswa kuzingatiwa kwa umakini mkubwa.

Faida Zake

Tendo hili huwa na faida nyingi kwa mama mjamzito. Baadhi ya faida hizo ni kuleta furaha, hasa baada ya kufikia mshindo, ni sehemu ya mazoezi, huongeza kinga ya mwili, ni sehemu ya kuboresha uhusiano, hupunguza maumivu ya mwili, huboresha usingizi, hasira na wasiwasi, huandaa vyema misuli ya nyonga kwenye kuhimili zoezi kujifungua pamoja na kusaidia kuimarisha misuli ya kibofu cha mkojo, hivyo kupunguza adha ya kwenda haja ndogo mara kwa mara.

Kwanini faida zote hizi? Kwa sababu mwili wa mwanamke huzalisha vichocheo na kemikali mbalimbali wakati wa tendo la ndoa. (10)

Kemikali na vichocheo hivi hufaa kwa afya yake.

Muhimu

Tendo hili huhitaji ridhaa ya mwanamke mwenyewe, pamoja na uwezo wake wa kuhimili.

Ikiwa hakutakuwa na sababu zozote za kitabibu kulisitisha, na ikiwa mwanamke mwenyewe atakuwa na nia na utayari wa kushiriki, linaweza kuendelea kufanywa hadi siku za mwisho kabisa za ujauzito.

Tofauti na jinsi inavyoaminika mtaani, tendo la ndoa haliwezi kuanzisha uchungu wa mapema wa kujifungua.

Muhtasari

Jambo la muhimu kuzingatia ni kuhakikisha kuwa mtindo wa kufanya tendo hili hauathiri kwa namna yoyote ile mkao na usalama wa mtoto tumboni.

Baadhi ya mitindo mizuri ni mwanamke kulala upande, mwanamke kuja juu ya mwanamme au pia kushiriki tendo hili huku wote kwa pamoja mmesimama.

Hata hivyo, ukubwa wa tumbo la mwanamke, pamoja na muda wa ujauzito wenyewe ndio mambo makuu mawili yanayoweza kutumiwa katika kuamua mtindo bora wa kushiriki tendo hili muhimu kwa wanandoa.

Share This Article