Mbegu za maboga zimekuwa maarufu sana miaka ya hivi karibuni.
Zimekuwa zinatumika kwenye uandaaji wa aina mbalimbali za chakula. Pia, baadhi ya watu huzitumia baada ya kuzikaanga.
Hakuna amri inayosisitiza mbegu hizi zitumike vipi, isipokuwa ni maamuzi ya mhusika mwenyewe.
Virutubisho
Kwa mujibu wa Idara ya kilimo ya Marekani (USDA), mbegu za maboga huwa na kiasi kikubwa cha nishati, protini, mafuta mazuri, wanga, nyuzi lishe, madini ya chuma pamoja na calcium.
Madini ya potassium, copper, zinc, selenium, vitamini C, folate, niacin pamoja na viondoa sumu vingi huwepo pia.
Unataka kufahamu faida za mbegu hizi kwa afya yako?
Twende pamoja.
1. Usingizi
Mbegu za maboga ni chanzo kizuri cha tryptophan.
Unajua kazi yake? Ikiwa ndani ya mwili hubadilishwa kuwa serotonin na melatonin. Hivi ni vichocheo viwili vinavyo ongoza mfumo wa usingizi.
Ulaji wa mbegu hizi walau saa moja kabla ya kwenda kitandani husaidia upatikanaji wa usingizi wa haraka. (1,2)
Pia, hutoa mchango mkubwa katika kutibu changamoto ya usingizi kwa watu wenye shida hiyo.
2. Ujauzito
Ni muhimu kama mwanamke mjamzito atapata kiasi cha kutosha cha madini ya zinc na folate.
Zinc ni muhimu katika kutengeneza seli za mtoto pamoja na vinasaba vya urithi. Husaidia pia kupunguza changamoto nyingi za uzazi.
Folate huhitajika ili kutengeneza mfumo imara wa fahamu wa mtoto, pamoja na kumkinga na tatizo la mgongo wazi.
Mbegu za maboga zinaweza kutoa uhakika wa upatikanaji wa virutubisho hivi.
3. Kisukari
Ili vichocheo vya insulin viweze kufanya kazi yake vizuri kwenye kudhibiti ongezeko kubwa la sukari, ni lazima mwili uwe na madini ya kutosha ya magnesium.
Mbegu za maboga ni chanzo kizuri cha magnesium.
Husaidia kwenye kukinga dhidi ya ugonjwa huu, pamoja na kuleta ahueni ya afya kwa wagonjwa.
4. Watoto
Unyafuzi na udumavu wa watoto mara nyingi husababishwa na ukosefu wa protini ya kutosha.
Mbegu za maboga ni chanzo kizuri cha protini.
Huwa pia na asidi ya omega 3 ambayo huhitajika kwa ukuaji bora wa watoto, kimwili na kiakili. (3)
Aidha, uwepo wa nyuzi lishe pamoja na madini ya chuma na calcium hufaa kwa utengenezwaji wa damu na ubora wa mifupa mtawalia.
5. Moyo
Huimarisha afya ya moyo.
Hufanya hivyo kwa kupunguza nafasi ya kuugua shinikizo la juu la damu, pamoja na kuharibu mafuta mabaya yanayo ganda kwenye mishipa ya damu. (4,5)
Pambana na magonjwa haya sugu kwa kutumia mbegu za maboga.
6. Ubongo
Madini ya zinc huhitajika kwenye usafirishwaji wa taarifa za mwili.
Magnesium hutumiwa na ubongo kwenye kazi yake ya kuchakata taarifa, kufikiri na kutunza kumbukumbu.
Madini ya copper husadia kuuwezesha ubongo katika kudhibiti vyema mfumo wa taarifa zinazo tumwa ili zifanyiwe maamuzi.
Upungufu wa madini haya hudumaza uwezo wa ubongo katika kufanya majukumu yake ya msingi kila siku. Vyote hivi utavipata kwenye mbegu za maboga.
7. Kinga Mwili
Mbegu za maboga huwa na kiasi kikubwa cha viondoa sumu vinavyofaa kwa afya.
Mfano, vitamini E utaipata kwa wingi humo.
Husaidia kuongeza kinga mwili, kuzuia magonjwa sugu hasa saratani pamoja na kuharibu sumu zinazodumaza afya ya seli za mwili.
8. Mbegu za Kiume
Madini ya zinc huhitajika kwenye utengenezwaji wa mbegu za kiume.
Uchache wake huhusishwa na kupungua kwa ubora wa mbegu za kiume pamoja na uwezo wa mwanamme kwenye kurutubisha yai la mwanamke. (6,7)
Ukiondoa uwepo wa zinc, mbegu za maboga huwa pia na viondoa sumu vingi vinavyo hitajika katika kulinda ubora wa afya ya uzazi wa mwanamme.
9. Mifupa
Magnesium ni madini yanayotumiwa na mwili katika kuboresha afya ya mifupa.
Huongeza ujazo wa mifupa pamoja na kuzuia tatizo la kudhoofika na kuvunjika kwa mifupa.
10. Ngozi
Umewahi kusikia kuhusu squalene?
Ni kiambato muhimu kinacho patikana karibia kwenye kila tishu ya mwili, ambacho huhusika kwenye utengenezwaji wa mafuta mazuri ya mwili.
Huboresha afya ya ngozi kwa kukinga dhidi ya mionzi mikali ya jua, pamoja na mionzi mingine hatarishi. (8)
Aidha, huzuia uvimbe pamoja na kuondoa wekundu wa ngozi.
11. Tezi Dume
Tezi dume ni miongoni mwa viungo muhimu vinavyo unda mfumo wa uzazi wa mwanamme.
Tezi dume sio ugonjwa.
Changamoto huja pale inapo vimba, kushambuliwa na vimelea vya magonjwa au pale inapopata saratani.
Tafiti za afya zinabainisha kuwa mbegu za maboga husaidia kwenye kupambana na tatizo la kuvimba kwa tezi dume.
12. Mfumo wa Mkojo
Husaidia kwenye kurekebisha changamoto mbalimbali zinazohusisha mfumo wa mkojo.
Wanawake na wanaume wote kwa pamoja huwa na manufaa kwao.
Mfano, katika utafiti mmoja, mafuta ya mbegu za maboga zilitibu changamoto ya watu wasio weza kutunza mkojo kwa muda mrefu.
Muhtasari
Mbegu hizi zinaweza kukaangwa kisha zikatumika kwa kutafuna. Zinaweza pia kupikwa au kuchemshwa.
Kwa watoto wachanga, hufaa zaidi zikijumlishwa kwenye unga wa lishe.
Furahia chakula hiki cha asili kilicho na utajiri mkubwa wa virutubisho.