Kuna mambo mengi ambayo mama mjamzito hushauriwa afanye kama sehemu ya maandalizi yake katika kufanikisha zoezi la kujifungua salama.
Miongoni mwa mambo hayo ni kufanya mazoezi mepesi yasiyoumiza.
Kuinama sana wakati wa ujauzito kuna madhara gani? Ni swali ambalo wanawake wengi hujiuliza. Kuinama ni sehemu ya kawaida ya mazoezi ya mwili.
Inaweza kufanyika kama sehemu ya mazoezi rasmi, au kupitia majukumu ya kila siku kama kufua, kudeki na kupika.
Vipi kuhusu usalama wake?
Mwongozo
Mwanamke anashauriwa kutokuinama kwa muda mrefu ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwake binafsi, pamoja na mtoto aliye tumboni.
Ikiwa mwanamke atainama kwa sababu za kimazoezi, mfano ubebaji wa vitu vizito, anashauriwa kufanya mambo yafuatayo;
- Asiiname zaidi ya nusu saa
- Asibebe vitu vizito pasipo kukunja magoti ili kuepuka kuumiza mishipa ya fahamu ya mgongoni
- Baada ya kukunja magoti, mzigo uwe karibu kabisa na mwili wake, kisha anyanyue huku akisimama taratibu
- Aepuke matumizi ya nguvu nyingi
Kama ilivyo kwenye kunyanyua vitu vizito, au kuinama kwa muda mrefu, mwanamke mjamzito hashauriwi pia kusimama kwa muda mrefu.
Mambo haya kwa pamoja huongeza nafasi ya kutokea kwa changamoto nyingi za ujauzito ikiwemo kuharibika kwa ujauzito, kujifungua kabla ya wakati pamoja na kupatwa na changamoto kubwa za maumivu ya misuli na maungio ya mifupa. (1,2,3)
Ni muhimu kuwa makini na kufanya mambo haya kwa kiasi.
Tahadhari
Hii isiwe sababu ya mwanamke kutokufanya kabisa mazoezi, au pia kushiriki kwenye majukumu mbalimbali ya nyumbani.
Uzembe wa kufanya kazi yoyote inayoongeza utimamu wa mwili huufanya mwili uvimbe hasa sehemu ya miguu, uso na mikono.
Aidha, huongeza nafasi ya kuugua kifafa cha ujauzito, kuongezeka kwa uzito usio sahihi, shinikizo la juu la damu, kisukari pamoja na kuongeza changamoto zingine nyingi wakati wa kujifungua. (4,5)
Kuna tatizo kubwa la kuganda kwa damu kwenye mishipa midogo ya damu linaloitwa Deep Vein Thrombosis (DVT).
Linaweza pia kutokea wakati huu.
Ushauri
Pande zote za stori zina madhara yake.
Ni muhimu kukumbuka kuwa kila jambo linahitajika kufanyika kwa kiasi.
Fanya mazoezi, inama, nenda kazini. Itakusaidia kuweka sawa afya yako. Lakini, hakikisha kuwa vyote vinafanyika kwa kiasi. (6)
Pale unapohisi maumivu ya aina yoyote ile, au unapoona baadhi ya mambo hayapo sawa wakati au baada ya kufanya mambo hayo unapaswa kuacha mara moja kisha fika hospitalini kwa ushauri, uchunguzi na tiba.
Dakika 30 za mazoezi kwa siku 5 kila wiki hutosha kabisa.
Hii ni sawa na dakika 150 kwa wiki.