Ukavu Ukeni: Chanzo, Madhara na Tiba

4 Min Read

Ili tendo la ndoa liweze kufanyika vizuri ni lazima uke uwe laini kukabili msuguano wa tendo hilo. 

Kwa asili yake, uke huwa na tabia ya kuzalisha ute lainishi wakati mwanamke anapokuwa amesisimka kihisia.

Ikitokea mwanamke hawezi kuzalisha ute huu, tendo la ndoa haliwezi kufanyika vizuri.

Kwanini Uke Mkavu?

Ni lazima ifahamike kuwa hali hii sio ya kawaida, hasa kwa wanawake ambao hawajafikia umri wa ukomo wa hedhi.

Inaweza kuchangiwa na mambo kama vile unyonyeshaji, msongo wa mawazo, uvutaji wa sigara, mazoezi au kazi ngumu, matumizi ya baadhi ya dawa hasa zile za uzazi wa mpango, sonona, tabia ya kuosha uke kwa kutumia kemikali na sabuni kali, Kisukari, kutolewa kwa vifuko vya mayai pamoja na kufikia umri wa ukomo wa hedhi

    Mambo haya huufanya mwili wa mwanamke ushindwe kuzalisha kiasi cha kutosha cha vichocheo vya kike, maarufu zaidi kama estrogen.

    Vichocheo hivi ni sawa na mafuta kwenye gari, ambayo pasipo uwepo wake haiwezi kutembea. Vivyo hivyo kwa uke. Pasipo vichocheo vya kutosha vya estrogen, hauwezi kuwa mlaini.

    Maandalizi ya Tendo

    Hoja hii hatukuitaja kwenye sababu za awali zinazochangia kutokea kwa changamoto ya ukavu wa uke.

    Maandalizi kabla ya kushiriki tendo la ndoa yanaweza pia kumfanya mwanamke awe na uke laini au mkavu wakati wa kushiriki tendo la ndoa. Sio kila mwanamke mwenye ukavu huwa na changamoto kiafya. Wengine huwa hawaandaliwi vizuri.

    Ni vizuri kwa wapenzi wakitumia muda wa kutosha kuandaana kabla ya kushiriki tendo la ndoa.

    Tabia hii huongeza uzalishwaji wa ute pamoja na kuongeza utimamu wa mwili katika kufikia na kurufahia utimilifu wa furaha baada ya kufika kileleni.

    Msikurupuke, tumieni muda wa kutosha kuandaana.

    Suluhisho

    Hatua za kuchukua kwenye kulikabili tatizo hili hutegemea na chanzo chake.

    Ikiwa litakuwa litahusishwa na sababu za kitabibu, dawa sahihi hasa zenye homoni zitatolewa baada ya kufanyika kwa vipimo hospitalini.

    Kwa wale ambao hawana ugonjwa, lakini hupata changamoto hii kutokana na maandalizi hafifu wanapaswa kupunguza papara. Waandaane vya kutosha.

    Kuku ni wako, manati ya nini?

    Njia Mbadala

    Watu wengi hukimbilia kutumia mate kama kilainishi kwa kupaka, au kulamba sehemu za siri.

    Mate hayawezi kutoa jawabu la kudumu. Huufanya uke uwe mkavu zaidi baada ya muda mfupi, huongeza nafasi ya kutokea kwa michubuko pamoja na uambukizwaji wa magonjwa.

    Wengine hutumia vilainishi maalumu vinavyouzwa madukani.

    Sina maana ya kusema kuwa ni vibaya, lakini ni muhimu kwanza kujua chanzo cha tatizo ndipo uanze kuvitumia.

    Ushauri

    Sasa unao ujuzi wa kutosha kuhusu suala hili na baada ya kulitazama kwa undani, ushauri wetu umejikita kwenye mambo haya;

    Tunajua unaumia, lakini endelea kushiriki tendo la ndoa kila mara kadri unavyoweza. Msisimko wa kihisia unaozalishwa wakati huu huongeza msukumo wa damu kwenye via vya uzazi. Kuna muda utafika, changamoto hii itaisha.

    Acha tabia ya kudeki uke. Kutumia kemikali kali, sabuni kali, manukato pamoja na vitu vingine unavyoingiza ukeni huharibu mazingira ya uke. Unajiharibia mwenyewe.

    Usitumie mate kama kilainishi, nenda kwenye maduka ya dawa ujipatie vilainishi bora pia unapaswa kupima na kutumia dawa.

      Muhtasari

      Utafutaji wa suluhisho la kudumu kwenye kuikabili hali hii hugubikwa na changamoto nyingi ambazo kwa sehemu kubwa huchangiwa na mihemko ya kihisia.

      Ni kipindi cha tiba, lakini ni kipindi kilekile ambacho tendo la ndoa ni lazima lifanyike. Kuyabeba mambo haya kwa pamoja ni mtihani mzito.

      Ni muhimu kama mwanaume atahusika moja kwa moja kwenye kutafuta suluhisho kwa kuwa itampa nafasi ya kuelewa adha anazopitia mwanamke.

      Changamoto ya ukavu wa uke inatibika.

      Share This Article