Sababu, Dalili na Matibabu ya Kidole Tumbo (Appendicitis)

4 Min Read

Kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa historia ya mabadiliko ya viumbe hai utakuwa siyo mgeni wa nadharia ya Lamarckism.

Huelezea jinsi matumizi ya mara kwa mara ya kiungo fulani cha mwili yanavyo kifanya kizidi kuimarika zaidi na zaidi, huku ikielezea kuwa viungo visivyotumika hudumaa, wakati mwingine hupotea kabisa au kukosa kazi yoyote ya kufanya mwilini.

Mfano ni kuacha kupaa kwa ndege aina ya mbuni, kutoweka kwa twiga wenye shingo fupi na kutokea kwa kidole tumbo kwenye mwili wa binadamu.

Kwa miaka mingi sana, imeaminika kuwa kidole tumbo ni kiungo kisicho na faida yoyote mwilini, lakini tafiti za sasa zinapinga madai haya.

Kidole tumbo husaidia kutunza na kuwalinda bakteria wazuri wanaohitajika kwenye kuboresha mfumo wa chakula.

Huhusika pia kwenye kuongeza ulinzi wa mfumo wa chakula pamoja na kuzuia usipatwe na magonjwa ya aina mbalimbali.

Kwa hoja hizi mpya, kidole tumbo hakijulikani tena kama kiungo kisicho na faida mwilini. Tukione kwa undani.

Kidole Tumbo ni Nini?

Ni sehemu ya mwisho kabisa ya utumbo mpana, inayopatikana upande wa kulia wa tumbo. 

Hufanana na kidole, ndio maana ikapewa jina la kidole tumbo.

Huitwa pia appendix.

Chanzo cha Tatizo

Kidole tumbo kama kiungo cha mwili hakina madhara yoyote kwa afya.

Changamoto hutokea pale kinapopata maambukizi ya vimelea vya magonjwa hasa bakteria.

Hii hukifanya kijae usaha, kivimbe pamoja na kujiziba. Kisipotibiwa husababisha maumivu makali, kufa kwa seli za eneo husika pia kinaweza kupasuka.

Ikiwa kitapasuka, kasi ya maambukizi kwenye sehemu ya chini ya tumbo huwa kubwa sana, inaweza pia kusababisha athari za kudumu kwenye afya pamoja na kifo.

Kidole tumbo kinaweza pia kusababishwa na Choo kigumu, kujaa kwa minyoo pamoja na ajali.

Dalili

Ikiwa mtu atakuwa na maambukizi kwenye kidole tumbo chake, dalili zifuatazo zitaonekana.

  • Maumivu makali sehemu ya chini ya tumbo hasa upande wa kulia
  • Maumivu ya tumbo wakati wa kucheka, kupiga chafya au kukohoa
  • Kukosa hamu ya kula
  • Homa
  • Kutokea kwa uvimbe sehemu ya chini ya tumbo
  • Kwa baadhi, huanza kuhara sana au kupatwa na choo kigumu

Tatizo hili haliambukizwi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.

Ugunduzi

Daktari huchukua historia ya mgonjwa pamoja na kufuatilia dalili zake.

Ikiwa ataona inafaa, vipimo vya mkojo, ujauzito na damu vitafanyika ili kuthibitisha kutokuwepo wa hali zinazoweza kuwa na dalili sawa kwa mgonjwa.

Ultrasound, CT scan na MRI hutumika ili kuthibitisha uwepo wa tatizo la kidole tumbo.

Tiba

Msingi wa tiba ya kidole tumbo hujikita kwenye mambo mawili ambayo ni Upasuaji wa dharura pamoja na matumizi ya dawa za viuavijasumu (antibayotiki)

    Matibabu haya huenda pamoja na hupaswa kufanyika kwa haraka sana ili kuepusha hatari kubwa zaidi inayoweza kujitokeza kwenye afya ya mgonjwa.

    Hivyo, mgonjwa hapaswi kupuuzia aina yoyote ya tiba kwa kudhani kuwa tatizo hili ni dogo.

    Nini Ufanye Ukiwa Nyumbani?

    Baada ya kugulika kuwa na tatizo hili, unapaswa kufanya mambo yafuatayo ili kupunguza maumivu na kuzuia kuongezeka kwa tatizo;

    • Acha kufanya kazi na mazoezi magumu
    • Ukitaka kukohoa, kucheka au kupiga chafya weka mto sehemu ya chini ya tumbo ili kupunguza maumivu
    • Pata muda wa kutosha wa kupumzika

    Ushauri

    Kwenye kila kundi la watu 100, wastani wa watu 5-9 kwenye kipindi fulani cha maisha yao hupatwa na changamoto hii.

    Lengo la kukupa takwimu hizi ni kutaka kukufanya uelewe kuwa hili sio tatizo jipya, na ikiwa wewe ndiye mhusika unapaswa kufahamu kuwa halijaanzia kwako.

    Changamoto hii inatibika. Usiogope.

    Share This Article