Maana ya aina Mbalimbali za Uchafu Unaotoka Ukeni

5 Min Read

Najua leo sio mara yako ya kwanza kuingia kwenye mtandao ukitafuta sababu za uke kutoa uchafu mweupe.

Aidha, nafahamu kuwa unayo hamu pia ya kufahamu maana ya uchafu huu. Twende pamoja.

Uke ni miongoni mwa viungo vyenye sifa ya kipekee sana.

Kimetunukiwa uwezo wa kujisafisha kuanzia ndani, kisha kuutoa uchafu wote nje kila siku. Ni viungo vichache sana vyenye uwezo kama huu. Mfano wa kiungo kingine ni sikio.

Mbali na kutoa uchafu, uke hutoa pia ute mzuri, pamoja na majimaji ambayo mengine huwa mazuri kwa afya, huku mengine yakiwa na maana mbaya kwa afya.

1. Uchafu Mweupe

Kama maziwa, mzito

Uchafu wa aina hii huwa na maana tatu.

  • Ujauzito
  • Siku zenye uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ujauzito
  • Magonjwa

Mwanamke anapokuwa na ujauzito, mwili wake huanza kutengeneza namna mbalimbali za kujilinda.

Mojawapo ya njia hizo ni kutengeneza ute mzito wa aina hii ili kuhakikisha usalama wa mtoto. Hauna maana mbaya kwa afya, pia mara nyingi huwa hauna harufu kali au mbaya. Ni kawaida.

Hivyo ute huu ukitoka huku unatoa harufu kali, au ukiwa na rangi za manjano, kijani au brown unapaswa kwenda hospitalini haraka. Hii ni hatari.

Baadhi ya wanawake huuona uchafu wa aina hii pia wawapo kwenye siku zenye uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ujauzito kila mwezi. Wanapaswa kufahamu kuwa hali hii ni kawaida kwao, ikiwa haiambatani na miwasho, rangi au harufu mbaya.

Maana ya tatu ya uwepo wa aina hii ya uchafu ni uwepo wa maambukizi hasa ya bakteria.

Huambatana na harufu kali na miwasho. Hali hii haipaswi kupuuzwa, siyo kiashiria kizuri kwa afya.

Kama unga, unapukutika au umeganda

Uke siyo ghala la mahindi au nafaka za aina yoyote ile. Uchafu wa aina hii haupaswi kutoka kabisa wakati wowote ule.

Ni ishara ya uwepo wa maambukizi ambayo mara nyingi husababishwa na fangasi jamii ya Candida albicans.

Kwa lugha maarufu zaidi mtaani hujulikana kama yeast infection.

Mara nyingi uchafu wa aina hii huambatana na miwasho ukeni, kuvimba kwa mashavu ya uke, maumivu wakati wa kukojoa pamoja na maumivu wakati wa kushiriki tendo la ndoa.

Uchafu huu unaweza kuwa mkavu sana kama unga, unaweza pia kubadilika rangi kuwa wa kijani au manjano baada ya muda fulani.

Ni muhimu kufanya vipimo ili dawa sahihi ziweze kutolewa. Magonjwa mengine pia hasa PID huwa na dalili hii.

2. Aina Nyingine za Uchafu

Kama yai, unavutika

Ute wa aina hii huwa hauna maana mbaya. Ni ishara ya uimara wa afya ya uke, pamoja na mfumo mzima wa uzazi wa mwanamke.

Unaweza kuonekana kwenye siku zenye uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ujauzito, au siku chache kabla ya hedhi. 

Husaidia pia kusafisha mfumo wa uzazi kwa kutoa bakteria na vimelea vingine vya magonjwa ambavyo ni hatari kwa afya. 

Kama maji, mwepesi

Ni kawaida. Unaweza kutokea muda wowote kwenye mzunguko wa hedhi.

Kwa baadhi ya wanawake huonekana kwa kiasi kikubwa baada ya kazi ngumu, au pale wanapokuwa wanafanya mazoezi.

Brown au damu

Kama uchafu huu unatokea baada ya hedhi ni sawa. Ni mabaki ya damu na uchafu.

Ikiwa itatokea katikati ya mzunguko wa hedhi inaweza kuwa ni ishara ya uwepo wa ujauzito au kuharibika kwa ujauzito ambao pengine ulitungwa pasipo uelewa wa mwanamke mwenyewe.

Katika mazingira machache kabisa, inaweza kuwa ni ishara ya uwepo wa saratani ya mji wa uzazi au mlango wa uzazi, pia uvimbe wa aina yoyote kwenye mfumo wa uzazi.

Manjano au kijani

Siyo ishara nzuri. Inaweza kuwa ni dalili ya kisonono, kaswende, klamidia, trichomoniasis pamoja na magonjwa mengine ya zinaa.

Huambatana na harufu kali ambazo humfanya hata mgonjwa mwenyewe apate wakati mgumu kuzivumilia.

Ute au uchafu wa aina hii unaweza kuwa unavutika kama kamasi, mwepesi kiasi kama maji au unaweza kuwa mzito. Siyo sawa.

Muhtasari

Mwili wa binadamu huwa na namna nyingi za kuzungumza ili kuonesha kuwa baadhi ya mambo hayapo sawa.

Mojawapo ya njia hizo ni kutoa uchafu, au ute wenye rangi mbalimbali pamoja na harufu kali.

Mazingira yoyote yanayojengwa na uchafu au ute huu yanayokufanya upoteze uhuru wako lazima yatiliwe mashaka. 

Huo ni wakati sahihi wa kupima na kupata tiba sahihi. 

Share This Article