Matibabu ya Tatizo la Vidonda vya Tumbo

6 Min Read

Vidonda vya tumbo ni tatizo linalosumbua watu wengi sana.

Pamoja na uwepo wa sababu zingine chochezi, ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa husababishwa uwepo wa maambukizi ya vimelea vya bakteria jamii ya H. pylori pamoja na athari za matumizi ya dawa za kutuliza maumivu.

Hauwezi kusita kuutaja mchango wa tiba asili na tiba mbadala katika kutibu ugonjwa huu. 

Fuatilia njia hizi zinazothibitishwa na tafiti mbalimbali ili zikupe uelewa mpana wa namna ya kushughulikia ugonjwa huu kwa njia za kiasili.

1. Ndizi Mbichi

Ndiyo. Tunamaanisha ndizi mbichi, siyo ndizi mbivu.

Husaidia kuponya vidonda vya tumbo kwa kusisimua utengenezwaji wa kuta mpya za sehemu ya tumbo iliyochimbwa.

Aidha, huzilinda kuta hizi ili zisiendelee kujeruhiwa na tindikali za tumbo. 

Uwepo wa kiasi kikubwa cha pectin, leucocyanidin pamoja na phosphatidylcholine ndiko hufanikisha kazi hii. (1,2,3)

Unaweza kuzipika kama chukuchuku. Zitumie kila mara kwa kadri utakavyoona inafaa

2. Juisi ya Kabichi

Kabichi mbichi huwa na aina fulani ya kiambata kinacho fahamika kama vitamini U. 

Kiambata hiki siyo vitamini halisi japo kimepewa jina hilo. Husaidia hupunguza maumivu ya vidonda, huongeza uzalishwaji wa ute rafiki, huimarisha kuta za tumbo pamoja na kuponya vidonda kwa haraka. (4,5,6)

Unaweza kutengeneza juisi hii kisha tumia mara mbili kwa siku, asubuhi na usiku

3. Aloe Vera

Sifa za mmea huu haziishii kwenye urembo pekee.

Kwa miaka mingi sana, aloe vera imekuwa inatumika katika kutibu changamoto za vidonda kuanzia nje hadi ndani ya mwili.

Tafiti kadhaa zinabainisha pia uwezo wa aloe vera katika kutibu vidonda vya tumbo. Unaweza sasa kuiongeza kwenye tiba iwapo unakabiliwa na tatizo hili.

4. Manjano

Hauwezi kuzungumzia viungo vya chakula pasipo kutaja manjano. Aidha, hauwezi kujisifu kuwa wewe ni mjuzi wa urembo hasa ule wa ngozi pasipo kutaja manjano.

Leo nakupa kazi ya tatu, manjao hutumika pia katika kutibu vidonda vya tumbo vya aina zote. (7,8)

Sifa hii hutokana na uwepo wa kiasi kikubwa cha viondoa sumu pamoja na kemikali zingine zinazo dhibiti msisimko wa mwili kwenye kuamsha uvimbe

5. Asali

Asali ni miongoni mwa vyakula vinavyoweza kukaa kwa miaka mingi pasipo kuharibika.

Huwa na sifa ya kupambana na aina mbalimbali za bakteria na virusi, pia hudhibiti ukuaji wa aina fulani za fangasi.

Husaidia pia kutibu aina mbalimbali za vidonda, vile vya tumboni vikiwemo pia kwenye kundi hili. Haupaswi kuwa na mashaka na asali. Anza leo kuitumia, itakusaidia.

6. Vitunguu Saumu

Mojawapo ya sababu ya kutokea kwa vidonda vya tumbo ni uwepo wa maambukizi ya vimelea vya bakteria jamii ya H. pylori.

Vitunguu saumu huwa na uwezo mkubwa wa kupambana na aina hii ya bakteria.

Huongeza pia uwezo wa kuta za tumbo katika kuponya majeraha yake. Huudhibiti mwili usizalishe vichocheo vinavyosisimua kutokea kwa uvimbe. (9,10)

Vimeelezewa kwa tafiti kuwa na uwezo wa kutibu vidonda vya tumbo

7. Yogurt

Ulaji wa vyakula vyenye bakteria wanaoweza kuzalisha lactic acid mwilini husaidia katika kupambana na ugonjwa wa vidonda vya tumbo hasa vile vinavyo sababishwa na bakteria jamii ya H. pylori.

Yogurt huwa na bakteria jamii ya Lactobacillus acidophilus La5 au Bifidobacterium lactis Bb12 ambao tafiti nyingi zinabainisha uwezo wao katika kutibu vidonda vya tumbo. (11)

Acha nadharia ya kuchukulia kuwa yogurt inafaa kwa watoto pekee. Itumie pia, itakufaa

8. Broccoli

Ni mboga za majani ambazo hazipatikani kirahisi kama zilivyo zingine.

Huwa ni mboga za majani zilizobeba kiasi cha kutosha cha kemikali inayoitwa sulforaphane (SFN) ambayo hulinda kuta za tumbo, huondoa sumu, huua bakteria pamoja na kuongeza uzalishwaji wa ute unaolinda kuta za tumbo. (12,13)

Ni ngumu kuzipata, pengine hata haujawahi kuziona. Zitafute

9. Mlonge

Karibia kila sehemu ya mti wa mlonge huhusishwa katika kutibu tatizo la ugonjwa wa tumbo. Unao uwanja mpana wa kuchagua kati ya majani, matunda na mizizi.

Tafiti nyingi zinaelezea kuwa mizizi ya mti huu huonesha uwezo mkubwa zaidi kuliko majani na matunda. (14,15)

Hata hivyo wanawake wajawazito pamoja na wale wanao nyonyesha hawashauriwi kutumia mmea huu kama sehemu ya tiba

Tahadhari

Kuna uvumi mtaani kuwa unywaji wa maziwa fresh husaidia kuponya tatizo hili.

Madai haya siyo ya kweli kwani maziwa hutoa ahueni ya muda mfupi kisha baadae kusababisha maumivu makali kwa mgonjwa. Soma hapa.

Badala ya kutumia maziwa fresh, mgonjwa anashauriwa kutumia mtindi kwa kuwa hufanya kazi sawa kama zilivyo yogurt ambazo tayari tumeshaona faida zake.

Muhtasari

Kabla mgonjwa hajaamua kutumia njia hizi, ni muhimu kwanza kufika hospitalini kupima ili aina ya vidonda vya tumbo vinavyomsumbua iweze kutambulika.

Hospitalini kuna dawa nzuri zinazoweza kutibu tatizo hili ndani ya muda mfupi. Dawa hizi zipo kwenye makundi mengi kulingana na namna zinavyofanya kazi.

Mfano wake ni pantoprazole, heligo kit, omeprazole, cimetidine na rabeprazole

Usikate tamaa, vidonda vya tumbo vinatibika

Share This Article