Njia ya Kisasa ya Uzazi wa Mpango ya Kitanzi

5 Min Read

Vitanzi ni vifaa vidogo vyenye umbo la herufi T vinavyoingizwa kwenye mji wa uzazi wa mwanamke kupitia uke na mlango wa kizazi.

Karibia aina zote za vitanzi huwa na kamba ndogo inayoning’inia kwenye mlango wa kizazi.

Huzuia ujauzito kwa kutoa kemikali ambazo huharibu mazingira wezeshi kwa mbegu za kiume kukutana na yai.

Ufanisi

Ufanisi wa kitanzi katika kuzuia ujauzito ni mkubwa.

Ni wastani wa ujauzito mmoja tu hutokea katika kundi kubwa la wanawake 100 wanaotumia njia hii.

Aina Zake

Kuna aina kuu 2 za vitanzi ambazo ni Vitanzi vya copper, ambavyo hufanya kazi hadi miaka 12 pamoja na vitanzi vya vichocheo vya levonorgestrel ambavyo hufanya kazi kwa wastani wa miaka 3-7 kulingana na kampuni husika

    Faida

    Kitanzi cha copper

    Ukiondoa faida kuu ya kuzuia ujauzito, kitanzi kinaweza pia kusaidia katika kupunguza nafasi ya kuugua saratani ya mji wa uzazi, saratani ya mlango wa kizazi pamoja na kuhifadhiwa kwa ujauzito nje ya mji wake.

    Kitanzi cha levonorgestrel

    Husaidia kupunguza hedhi kubwa, maumivu ya hedhi pamoja na kupunguza nafasi ya kuugua saratani ya mji wa uzazi na mlango wa uzazi.

    Maudhi

    Kitanzi cha copper

    Maudhi makubwa ya njia hii ya uzazi wa mpango ni kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi, jambo ambalo huwafanya wanawake wengi watokwe na kiasi kikubwa cha damu kwenye hedhi, au kupatwa na changamoto ya kutokwa na damu katikati ya mzunguko wa hedhi.

    Ikiwa mwanamke atapata ujauzito wakati kitanzi kipo ndani ya mwili inaweza kusababisha kuharibika kwa ujauzito, kufariki kwa mtoto tumboni pamoja na kupatwa na maambukizi makubwa.

    Maambukizi ya sehemu ya juu ya mfumo wa uzazi maarufu kama PID yanaweza kutokea ikiwa wakati kinawekwa mwanamke alikuwa na klamidia, kisonono au kaswende.

      Kitanzi Cha levonorgestrel

      Aina hii ya kitanzi husababisha kukosekana kwa hedhi, kuvurugika kwa hedhi, chunusi, maumivu ya kichwa, kuwasha kwa matiti, kichefuchefu, kuongezeka kwa uzito pamoja na kubadilika kwa mihemuko ya mwili.

      Nani Anaweza Kutumia?

      Karibia kila mwanamke anaweza kutumia aina hii ya njia hii ya kisasa ya uzazi wa mpango. Baadhi ya makundi yanayoweza kutumia ni mwenye mtoto tayari, asiye na mtoto, mwenye umri wowote, hata zaidi ya miaka 40, mwanamke anayenyonyesha, mwanamke ambaye ujauzito umeharibika, una historia ya kutungisha ujauzito nje ya mji wa uzazi, mwanamke anayeshiriki kazi ngumu pamoja na mwenye VVU anayetumia au asiye tumia dawa, maambukizi yakiwa siyo makubwa sana.

        Nani Hapaswi Kutumia?

        Mwanamke mwenye mzio na copper hapaswi kutumia kitanzi cha copper, anapaswa kutumia kitanzi cha vichocheo vya levonorgestrel.

        Pia, wanawake hawa hawapaswi kutumia kitanzi

        Mwanamke mwenye magonjwa ya zinaa hasa klamidia, kisonono na kaswende. Anapaswa kusubiria hadi apone vizuri kwanza.

        Mwanamke mwenye maambukiz kwenye damu baada ya kutoa au kuharibika kwa ujauzito. Anapaswa kusubiria hadi apone vizuri kwanza.

        Mwanamke ambaye hajatimiza wiki 4 tangu ajifungue, mwanamke mwenye ujauzito tayari, mwanamke mwenye saratani kwenye sehemu yoyote ya mfumo wa uzazi na ambaye maambukizi ya VVU yamefikia hatua mbaya.

          Ni muhimu kwa wanawake walio kwenye mazingira hatarishi ya kupatwa na magonjwa ya zinaa wakashauriwa kutokutumia njia hii.

          Ni vizuri kuchagua njia nyingine kwani uwepo wa maambukizi ya magonjwa ya zinaa huongeza athari, na kusababisha changamoto kubwa zaidi.

          Ushauri

          Ikiwa mwanamke ataamua kutumia njia hii ya uzazi wa mpango atatakiwa kufahamu kuwa kitendo cha yeye kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja, au kuwa na mwanamme ambaye hushiriki mpenzi na wanawake wengi ni hatari.

          Kitanzi huhitaji ushirikiano na uaminifu mkubwa sana kwa wapenzi, vinginevyo mwanamke huyu atakuwa mhanga wa mara kwa mara wa magonjwa ya mfumo wa uzazi.

          Muhtasari

          Uwezo kwa kushika ujauzito baada ya kuacha matumizi ya kitanzi hutofautiana miongoni mwa wanawake.

          Wastani wa kawaida ni miezi 3-8, japo wengine hutumia hadi miezi 18.

          Share This Article