Kabla hata mwanamke hajapata uthibitisho wa kipimo cha mkojo kinacho patikana kirahisi sana mtaani, au kwa vipimo vya damu na ultrasound vinavyofanyika hospitalini, dalili za awali za ujauzito zinaweza kuwa tayari zimeshaanza kuonekana.
Umri wa ujauzito mara nyingi huaza kuhesabiwa tangu tarehe ya kwanza ya hedhi ya mwisho hivyo kufahamu dalili za mapema za uwepo wake ni jambo la msingi.
Kila mwanamke yupo tofauti, lakini pamoja ja uwepo wa utofauti huu, hizi ni dalili za kawaida zinazoonekana kwa wanawake wengi.
1. Kunusa
Mimba changa huja na tabia mpya ya kuongezeka kwa uwezo wa mwili kwenye kutambua na kunusa harufu.
Uwepo wa harufu ndogo tu kwenye eneo husika, iwe ya manukato au chakula huwa ni lazima itambulike.
2. Matiti
Tofauti na siku zote, chuchu za matiti huanza kuwa nyeusi. Pia, miwasho huanza kumsumbua mwanamke.
Kwa baadhi ya wanawake, matiti kwa ujumla wake huongezeka msisimko wake, ukubwa wa maumbo na mara chache huanza kutoa majimaji.
3. Uchovu
Mwili huwa umeingiliwa na kiumbe kipya hivyo ni lazima uwe unasita katika kufanya baadhi ya mambo kama ulivyokuwa umezoea.
Nguvu zake nyingi huzitumia kwenye kujenga mazingira rafiki ya ukuaji wa mtoto.
Uchovu wakati huu huwa hauhusishwi na kazi, unaweza kutokea hata asubuhi na mapema baada tu ya kuamka.
4. Damu
Baada ya kutungwa kwa ujauzito, kijusi huhitaji kujishikiza kwenye mji wa uzazi ili kihifadhiwe hapo. Ili kitunzwe, ni lazima kichimbe kuta za sehemu hiyo.
Kitendo hiki hutokea kati ya siku ya 7-14 tangu ujauzito utungwe.
Hapa mwanamke anaweza kutokwa na matone machache ya damu ambayo huwafanya wengi wadhani kuwa ni hedhi.
Damu hii inaweza kuonekana kwa kati ya siku 1-4.
5. Haja Ndogo
Vichocheo vya ujauzito huongezeka sana wakati huu ambavyo huwa na tabia ya kuongeza msukumo na usafirishwaji wa damu kwenye figo.
Pia, mji wa uzazi huanza kuweka mgandamizo kwenye kibofu cha mkojo hivyo kukifanya kipingue ukubwa. Ndiyo maana unakojoa mara kwa mara.
6. Kiungulia, Kichefuchefu na Kutapika
Ni jambo la kawaida sana kutokea wakati huu.
Huwekwa kwenye mjumuisho wa hali ambazo kwa pamoja hupewa jina la magonjwa ya asubuhi, japo zinaweza kutokea muda wowote wa siku ukiondoa asubuhi pekee.
7. Chuki na Hasira
Wengi huanza kuwa na chuki na hasira zisizo elezeka. Hufanya hivi pasipo kupenda.
Tabia hii husababishwa na ongezeko kubwa la vichocheo vya estrogen na progesterone ambao huufanya mwili uanze kuonesha tabia ambazo kwa mhusika huwa hazina madhara, japo kwa wengine huwa ni kikwazo kikubwa.
Hata hivyo, wanawake hushauriwa kuwa makini na tabia hizi.
Zinaweza kuwafanya wapate sonona, changamoto zingine kwa afya pamoja na kuathiri afya ya mtoto.
8. Kutema Mate
Ni tabia ambayo kwa wanawake wengi huonekana ujauzito ukiwa mkubwa, walau baada ya wiki 4.
Kwa baadhi ya wanawake hii huwa tofauti. Kuanza kuonekana mapema sana, siku za mwanzo kabisa za kutungwa kwa ujauzito.
9. Vyakula
Ukiona umeanza kupenda sana aina fulani ya chakula kabla hata tarehe za hedhi hazijafika, au umeanza kuchukua chakula fulani bila sababu, ambacho kabla ulikuwa unapenda unaweza kuwa na uhakika kuwa pengine ujauzito umetunga.
Hali hii kwa baadae inaweza kwenda mbali zaidi kwa kuanza kupenda vitu kama udongo, karatasi, barafu.
Kitaalamu, hali hii huitwa pica.
10. Choo Kigumu
Baada ya kutungwa kwa ujauzito, vichocheo vya progesterone huongezeka sana kwenye damu.
Vichocheo hivi huufanya mfumo wa chakula upunguze miondoko ya chini ya misuli yake pamoja na kuchelewesha utolewaji wa choo kupitia haja kubwa.
11. Chunusi
Nuru ya uso huongezeka.
Ongezeko la ghalfa la damu pamoja na vichocheo vya mwili kwa baadhi ya wanawake kufanya chunusi zifumuke usoni.
Kwa baadhi ya wanawake, mabaka meusi huanza kutokea usoni.
12. Uzito
Ni ngumu kujua kuwa uzito umeongezeka hasa wiki za mwanzo kabisa.
Ongezeko hili huchangiwa sana na ukuaji wa matiti, mji wa uzazi, kondo la uzazi, maji ya uzazi, damu pamoja na mafuta.
Uzito huu huendelea kuongezeka kadri umri wa ujauzito unavyozidi kuwa mkubwa.
Muhtasari
Kwa baadhi ya wanawake, joto la ndani ya mwili huongezeka sana wakati huu.
Ikitokea mwanamke ameweka kipima joto kwenye uke, ataona kuwa wiki za mwanzo za ujauzito joto limeongezeka kwa walau nyuzijoto 1.
Pia, unyevu wa mlango wa kizazi huongezeka ukichagizwa na uzalishwaji wa ute mweupe unaofanana na ule unao onekana siku za hatari.
Ili kuhakiki kuwa tayari ujauzito umeingia, ni muhimu kusubiri walau siku 14 kufanya kipimo ili kuwa na uhakika wa majibu.